Wednesday, September 29, 2010

UZINDUZI WA ILANI YA UCHAGUZI YA WAPIGA KURA 2010 KWA MAANDISHI YA NUKTA NUNDU

TANZANIA GENDER NETWORKING PROGRAMME (TGNP)
P.O. Box 8921, Dar es Salaam, TANZANIA; Gender Resource Centre, Mabibo Road, Adjacent to the National Institute of
Transport (NIT) Tel. 255 22 244.3450/ 244.3205/ 244.3286; Mobile 255 7 0754 784050/ 0754 788706; Fax 255 22 244.3244; Email
tgnp@tgnp.co.tz; Website www.tgnp.co.tz


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

UZINDUZI WA ILANI YA UCHAGUZI YA WAPIGA KURA 2010 KWA MAANDISHI YA
NUKTA NUNDU

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) unatarajia kuzindua Ilani ya Uchaguzi ya Wapiga Kura 2010 kwa maandishi ya nukta nundu, maalum kwa ajili ya wasioona, kesho Jumatano tarehe 29 Septemba 2010 kuanzia saa nne asubuhi katika viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo, karibu na Chuo cha Usafirishaji.

Ilani ya Uchaguzi ya Wapiga Kura 2010 ilizinduliwa rasmi mwezi Juni mwaka huu, kutokana na madai ya wapiga kura na kwa kutambua umuhimu wa ushiriki wa wenzetu wasioona, TGNP ikishirikiana na Sauti ya Wanawake wenye Ulemavu Tanzania ( SWAUTA) wametoa nakala za Ilani ya Wapiga Kura 2010 kwa maandishi ya nukta nundu ili nao waweze kutoa sauti zao, washiriki na kuchangia mijadala mbalimbali ya uchaguzi inayoendelea nchini kote.

Kuzinduliwa kwa Ilani kwa maandishi ya nukta nundu kutasaidia kuboresha ufikiaji na kufahamika kwa madai ya wapiga kura katika uchaguzi mkuu ujao hususan kwa makundi ya walemavu wasioona.

Aidha ilani hii itawezesha wenzetu wasioona, kutumia haki yao ya msingi kuweza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi mkuu ujao mwezi Oktoba kwa kuhoji sera za wagombea; kutoa madai yao katika kampeni na midahalo inayoendelea nchini kote; na kuweka mikakati ya kufuatilia na kudai uwajibikaji wa serikali na viongozi watakaoingia madarakani katika kuhakikisha haki , usawa na kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu wa aina zote.

TGNP inakuwa mojawapo ya mashirika machache sana kuandaa nyaraka muhimu kama hizi katika mfumo wa maandishi ya nukta nundu ukiacha vitabu vya kufundishia vinavyoandaliwa na serikali kwa ajili ya kutumika mashuleni. Aidha huu ni mwendelezo wa mipango ya TGNP ya kuyafikia na kushirikiana zaidi na makundi yaliyoko pembezoni katika ujenzi wa tapo la harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi.

Wanajamii wote wanahamasishwa kushiriki katika tukio hili la kihistoria.

Imendaliwa na Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP)
Na kusainiwa na Mkurugenzi wa TGNP – Usu Mallya
28 Septemba 2010

No comments: