Thursday, October 7, 2010

Upepo wageuka Pemba

TAMBO, vijembe, kejeli na hata vurugu zilizokuwa zikitokea wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu visiwani hapa siku za nyuma, havipo tena katika uchaguzi wa mwaka huu na inadaiwa kupunguza nguvu ya CUF.

Hali hiyo imetokana maridhiano ya kisiasa na uamuzi wa CCM kumteua Dk Ali Mohamed Shein ambaye ni mzaliwa wa hapa, kuwa mgombea urais wa Zanzibar. Dk. Shein amezaliwa kijiji cha Chokocho, Mkanyageni, Kusini Pemba.

Baadhi ya wakazi wa hapa waliozungumza na HABARILEO katika viwanja vya Fire Chanjaani mjini hapa, muda mfupi kabla ya mgombea urais wa CCM Tanzania, Rais Jakaya Kikwete, kuhutubia mkutano wa kampeni juzi jioni, walisema maridhiano ya kisiasa na kuteuliwa kwa Dk. Shein kumepunguza nguvu ya CUF Pemba.

Maridhiano ya kisiasa yalifikiwa baada ya Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kufanya mazungumzo na kukubaliana kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, inayojumuisha vyama hivyo vyenye ushawishi mkubwa wa
kisiasa baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu.

Makubaliano hayo yalibarikiwa na Halmashauri Kuu za Taifa za vyama hivyo na Baraza la Wawakilishi na kisha kupelekwa kwa wananchi kupitia kura ya maoni, ambapo asilimia kubwa ya wananchi waliafiki na maridhiano hayo kukubalika rasmi.

Akizungumza wakati akimkaribisha Rais Kikwete kuhutubia mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mbelwa Hamad Mbelwa, alisema: “Mheshimiwa Mwenyekiti (Rais Kikwete), Pemba ya juzi si Pemba ya leo.

“Napenda kukufahamisha kuwa CCM sasa Pemba ina hali nzuri, usalama na amani vimeongezeka sana.

Miaka ya nyuma wakati kama huu wa kampeni ilikuwa ni hatari sana, lakini sasa ni amani na utulivu na hii inatokana na maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa hivi karibuni,” alisema Mbelwa.

Mkazi wa Mtambile, Ally Hamad Seif, akizungumza na gazeti hili bila kutaja ni mwanachama wa chama gani, alisema: “Mimi naona CCM ndio wamefaidika zaidi na maridhiano, maana kwa miaka mingi Pemba ni ngome ya CUF.

“Naona sasa kama vile CUF wamevunjwa nguvu kiasi na haya maridhiano na ni kama vile wamerudi nyuma, wakati kwa upande mwingine naona kama CCM wanakuja juu zaidi na kushika kasi huku Pemba,” alisema Seif.

Mkazi wa Wete, Zuhura Majid Mbarouk, alisema nguvu ya CUF Pemba kwa kiasi kikubwa inatokana na ushawishi mkubwa wa kisiasa alionao Maalim Seif na hivyo hatua ya kiongozi huyo kusimamia maridhiano ya kisiasa na Rais Karume, kumefanya Wapemba wengi kumwunga mkono na kujenga umoja na mshikamano baina ya CCM na CUF.

“Miaka ya nyuma wakati kama huu ilikuwa ni vurugu sana, tulikuwa hatuwezi kuzikana hata tunapofiwa. Sasa ni amani na utulivu, ni kama vile mwezi huu hakuna uchaguzi, maana Pemba imepoa sana hata nashangaa.

“Nadhani nguvu kubwa ya CUF iko kwa Maalim Seif, sina hakika na nguvu za chama hiki, Maalim Seif akistaafu siasa,” alisema.

Akizungumza katika mkutano huo, Rais Kikwete alijisifu kwa kusimamia maridhiano hayo na kusema ni ahadi aliyoitoa alipohutubia Bunge mara ya kwanza Desemba 30, 2005 baada ya kuchaguliwa kuwa Rais ambapo alieleza kutoridhishwa na mpasuko wa kisiasa baina ya Zanzibar na Pemba.

Alisema hatua hiyo ndiyo ilimfanya asimamie mazungumzo ya kutafuta suluhu ambayo yalikabiliwa na vikwazo vya hapa na pale kabla Rais Karume na Maalim Seif hawajahitimisha na kufanikisha kufikiwa kwa maridhiano ya kisiasa, yanayovifanya visiwa hivi sasa kuwa

na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, baada ya uchaguzi mkuu ujao. “Leo hii nyie ni mashahidi wa namna Pemba ilivyo na amani na utulivu.

Leo mwana CCM anavaa sare yake ya chama bila woga wa kufanyiwa vurugu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Kampeni ni za amani na utulivu. Msione vinaelea vimeundwa,” alisema Rais Kikwete.

Kikwete ambaye aliwasili hapa juzi akitokea Songea, Ruvuma, ambako alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za Siku ya Walimu Duniani, aliwataka wagombea wa CCM kutembea kifua mbele.

Mgombea huyo alisema wagombea wa CCM hawana sababu ya kuendesha kampeni zao kinyonge, kwa sababu CCM imefanya mengi Pemba, kama ilivyo katika maeneo mengine nchini.

“Pambaneni, msibabaike wala kutishika kwa sababu hakuna kisichowezekana,” aliwaambia wagombea hao wa ubunge, uwakilishi na udiwani kupitia CCM.

Katika mkutano wake na wagombea hao juzi mjini hapa, alisema mazingira ya kisiasa yamekuwa bora zaidi Pemba na yanatoa fursa nzuri kwa wagombea wa CCM kupata ushindi.

“Mazingira ni mazuri sasa. Mazingira yamekuwa tulivu na mnaweza kusikilizwa sasa. Naambiwa sasa kuwa picha ya mgombea wa chama kimoja inaweza kubandikwa kwenye nyumba ya shabiki wa chama kingine bila kubanduliwa au kuchanwa.

“Sisi lazima tuendeshe kampeni zetu kwa nguvu moja – tumefanya mengi. Uhodari wenu ni katika kuwaeleza wananchi mafanikio hayo.

“Hatuna unyonge, kwa sababu kama barabara tumejenga, kama skuli (shule) zipo, kama umeme tumeleta, kama maji yanapatikana, kama ni afya hakuna mkazi wa Pemba anayetembea zaidi ya kilometa tano kusaka huduma za afya,” alisema.

Akiwa katika kampeni Unguja katika Uwanja wa Demokrasia maarufu kama Kibanda Maiti, mkoani mjini Magharibi, Rais Kikwete alisisitiza umuhuimu wa kuendeleza Mapinduzi ya Zanzibar na kuleta maendeleo zaidi.

Alisema ataleta maendeleo zaidi katika miaka mitano ijayo na kwamba atashangaa kama wananchi watashindwa kumpigia kura nyingi.

Rais Karume ambaye alikuwepo katika msafara huo, alimuombea kura Rais Kikwete na Dk. Shein.

No comments: