SIKU chache kabla ya kupiga kura Jumapili ijayo, wagombea watatu wa urais wanaochuana, Jakaya Kikwete wa CCM, Dk. Willibrod Slaa wa CHADEMA na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, wamekuwa na vigezo vinavyotofautiana mbele ya macho ya wapiga kura wengi, Raia Mwema imebaini.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kete kubwa ya Dk. Willibrod Slaa inayovutia wengi ni uadilifu, umakini na uwajibikaji kama alivyojipambanua akiwa mbunge kwa miaka 15, wakati Jakaya Kikwete wa CCM kampeni zake tofauti na mwaka 2005 zimetegemea zaidi mtandao wa chama hicho na kivuli chake cha urais. Hali hiyo ni tofauti na mwaka 2005 alipokuwa na mvuto zaidi kuliko chama hicho.
Wachambuzi wa mambo wanasema umaarufu wa Kikwete umeshuka kinyume cha 2005 kutokana na wananchi kujua upande wake wa pili kiutendaji kama Rais wa Tanzaia. Lakini wakati hali ikitajwa kuwa hivyo kwa Dk. Slaa na Kikwete, kwa upande wa Profesa Ibrahim Lipumba anavutia zaidi wapiga kura wanaomuunga mkono kutokana na kigezo cha usomi wa taaluma inayoaminika kuhitajika zaidi kwenye nchi inayodaiwa ni masikini kama Tanzania. Mtazamo wa wapiga kura wengi ni kama ifuatavyo.
Dk. Willibrod Slaa
Kabla ya kampeni kuhitimishwa Jumamosi, Dk. Willibrod Peter Slaa amezidi kujipambanua kama kiongozi mwenye nia ya dhati kusimamia maadili, uadilifu, umakini na uwajibikaji. Inaelezwa kuwa amekiinua mno chama chake ikilinganishwa na wagombea urais wengine kutoka kambi ya upinzani.
Kwa mfano, mwaka 1995, chama kilichokuwa na mvuto zaidi kilikuwa NCCR-Mageuzi na ndicho kilichotia changamoto zaidi CCM lakini kilianza kupoteza mvuto kwa kadiri miaka ilivyosogea kikitoa nafasi kwa Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kilitwaa nafasi ya chama kikuu cha upinzani hasa katika chaguzi za mwaka 2000 na 2005.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, CHADEMA kinaonekana kung’ara zaidi kisiasa kuliko hata CCM. Vyama vingine hasa CCM vimekuwa vikizidi kupoteza mvuto wakati CHADEMA ikijiongezea umaarufu. Wengi wanaamini mchango wa Dk. Slaa ni mkubwa katika kukinyanyua chama hicho.
Ni mtu mwenye kupenda kujisomea zaidi na hasa kusoma taarifa mbalimbali zinazohusu nchi na mataifa mengine. Itakumbukwa Dk. Slaa ndiye aliyebaini kuwa Rais Kikwete ambaye anagombea urais kwa tiketi ya CCM alitia saini Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa mbwembwe bila kujua kuwa alichosaini sicho kilichopitishwa bungeni. Ni kiongozi anayependa kutafiti kabla ya kutoa kauli zake.
Dk Slaa alizaliwa Oktoba 29, mwaka 1948 wilayani Karatu. Alipata elimu ya msingi katika shule za Karatu na Kwermusi (Mbulu) kati ya mwaka 1958 na 1965.
Alisoma elimu ya sekondari katika Shule za Dung’unyi Seminari na Itega Seminari kati ya mwaka 1966 na 1971.
Ni kiongozi mwenye stashahada tatu pamoja na shahada ya Uzamivu (PhD). Anayo Shahada ya Uzamivu (PhD ) katika Sheria ya kanisa kutoka Chuo Kikuu cha St. Urban, Rome. Pia anastashahada ya Theolojia kutoka Kipalapala Seminari, Stashahada ya falsafa kutoka Kibosho Seminari, Stashahada ya Afya ya Macho kutoka Kituo cha Kimataifa cha Macho.
Amewahi kuwa padri wa Kanisa Katoliki kuanzia mwaka 1977 hadi 1991, akishika nafasi za kiutawala katika kanisa pia. Amepata kuandika vitabu vitatu ambavyo ni Utimilifu wa Msichana (1977), Utimilifu wa Mvulana (1977) na Expediency and exigency Liturgical Legislation (1981). Ni mzungumzaji wa Lugha nane kwa ufasaha; ambazo ni Kiswahili, Kiingereza, Kilatini, Kiitaliano, Kijerumani, Kihispania, Kireno na Kifaransa.
Jakaya Kikwete
Tofauti na wagombea wenzake, Kikwete anaweza kupimwa katika miaka mitano ya urais. Mwaka 2005, aliongoza kampeni za CCM na kushinda kwa asilimia 80.28, wabunge 206 kati ya 232, sawa na asilimia 88.79 na udiwani walishinda kwa asilimia 91.46.
Ingawa washiriki wa kampeni za Kikwete wanaamini amefanya mambo makubwa na hasa ujenzi wa miundombinu na elimu, mbele ya macho ya wananchi nje ya CCM, anaonekana ni mtu mwenye uvumilivu wa kukosolewa. Hat ahivyo, kwa sehemu nyingine uvumilivu huo unatajwa kuvuka mipaka kiasi cha kuruhusu malumbano miongoni mwa viongozi wa CCM na hata serikalini.
Kikwete pia anatajwa kupoteza dira katika vita dhidi ya ufisadi ikifafanuliwa kuwa kama angekuwa na nia ya dhati ya kupambana na ufisadi hasingeweza kuruhusu watu wanaozongwa na mazingira ya ufisadi kuteuliwa na chama chake kuwania uongozi na baadaye kuwanadi jukwaani kuwa ni watu safi huku akitambua kuwa baadhi amewafikisha mahakamani.
Hapa wanarejea mfano wa Mwalimu Julius Nyerere ambaye hakusubiri uamuzi wa Mahakama kujitenga na mafisadi. Katika vita hiyo Mwalimu alijipambanua na msemo maarufu wa “kustaafishwa kwa manufaa ya umma.” Ushahidi wa mazingira ulitosha kumpumzisha kiongozi na kama ushahidi zaidi ulijitosheleza mhusika alifikishwa kortini.
Jakaya Kikwete alizaliwa Oktoba 7, mwaka 1950 katika Kijiji cha Msoga, Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani. Alipata elimu ya msingi (darasa la kwanza hadi la nne) mwaka 1958-1961 katika Shule ya Msingi Lugoba na Shule ya Kati ya Lugoba (darasa la tano hadi la nane) mwaka 1962-1965. Mwaka 1966-1969 alisoma Shule ya Sekondari ya Kibaha, kidato cha kwanza mpaka cha nne, na mwaka 1971-1972 alisoma kidato cha tano na cha sita Shule ya Sekondari ya Tanga.
Mwaka 1972-1975 alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alihitimu Shahada ya Kwanza ya Uchumi. Alipata mafunzo ya Uofisa wa Jeshi katika Chuo cha Uongozi wa Jeshi Monduli, mwaka 1976-1977 na kupata Kamisheni ya kuwa Luteni. Baadaye mwaka 1983 – 1984 alipata mafunzo ya Ukamanda wa Kombania katika chuo hicho hicho.
Prof. Ibrahim Lipumba
Huyu ni mgombea urais wa CUF, aliyezaliwa Juni 6, 1952. Mtanzania mtaalamu mbobeaji wa uchumi, mwanasiasa na mwenyekiti wa CUF. Amehitimu shahada yake ya uzamivu katika chuo kutoka Chuo Kikuu cha Stanford na baadaye kuwa Profesa wa Uchumi. Amewahi kushika nyadhifa mbalimbali zinazohusisha taaluma, kwa mfano amekuwa profesa katika Marekani na hapa nchini. Pia amewahi kuwa mtaalamu huru wa uchumi na kupata kuwa mshauri wa uchumi kwa Serikali ya Uganda mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Amekuwa kiongozi mzoefu katika uongozi wa chama katika nafasi ya siasa kuliko wenzake. Amekuwa mwenyekiti wa CUF tangu mwaka 1995 hadi sasa. Ni mzoefu pia katika kuwania urais wa Tanzania kuliko wenzake, akianza safari hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi uliosisiwa tena miaka ya 1990. Ameanza kuwania urais tangu mwaka 1995, akishika nafasi ya tatu akipata asilimia 6.43 ya kura. Mwaka 2000 alishika nafasi ya pili akitanguliwa na Benjamin Mkapa. Katika uchaguzi huo Lipumba alipata asilimia 16.26 ya kura, akijiongezea asilimia takriban 10 ya kura ikilinganishwa na mwaka 1995.
Katika Uchaguzi wa Desemba 14, mwaka 2005 alishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 11.68 ya kura, akitanguliwa na mmoja wa washindani wake wa sasa, Jakaya Kikwete. Mbali na kujishughulisha na siasa, Lipumba ameendelea kutumikia taaluma yake kama mchumi huru, akigawa sehemu ya muda kwenye siasa na taaluma.
Profesa Lipumba anaonekana kung’ara zaidi kwenye kampeni kama msomi wa kiwango cha juu zaidi ikilinganishwa na wagombea wenzake wawili wakubwa, yaani Dk. Willibrod Slaa na Jakaya Kikwete. Kutokana na nchi kuwa na matatizo ya kiuchumi na hasa mfumuko wa bei ukiwaumiza wananchi masikini, taaluma ya Profesa Lipumba kama itatumika kigezo pekee cha kumpigia kura mgombea basi atashinda kwa kishindo.
Hata hivyo, Prof. Lipumba anaweza kuwekwa sehemu moja na Serikali ya CCM katika baadhi ya nyanja kutokana na kuwahi kufanya kazi za Serikali kama mshauri wa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi. Nyanja hizo ni pamoja na masuala ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma.
Kwa mfano, mwaka 1991 hadi 1993, Prof. Lipumba alikuwa Kamishna wa Tume ya Rais wa Kurekebisha Mashirika ya Umma. Mwaka 1992 hadi 1993, alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Bima la Taifa na mwaka huo huo, aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kuchunguza mgogoro wa menejimenti katika shirika hilo ambalo hadi sasa hali yake ni taaban.
Mwaka 1992, Prof. Lipumba pia aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya kuchunguza ufisadi katika Chama Cha Ushirika Shinyanga (SHIRECU) ambacho hakina unafuu hadi sasa na katika kampeni za mwaka huu, Kikwete ameahidi kulipa madeni ya fedha zilizoibwa bila kuahidi kuwachukulia hatua wahusika.
Kwa upande mwingine, Prof. Lipumba amewahi kuongoza, kuteuliwa au kusimamia shughuli mbalimbali za kimataifa kama mtaalamu gwiji wa uchumi. Amewahi pia kuwa mshauri wa uchumi wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni. Lakini wakati hali ikiwa hivyo kwa wagombea hao watatu wa urais, mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa inazidi kutoa picha tofauti kwa kadiri siku ya kupiga kura inavyokaribia.
Ukiacha mchuano huo wa wagombea urais, mbio za kuwania ubunge nazo ni kali kama ambavyo Paul Sarwatt anavyoripoti kutoka Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara kuwa vyama vinavyochuana vikali huko ni CCM, CHADEMA, NCCR-Mageuzi na TLP kwa mbali.
Kilimanjaro kwenye majimbo tisa CCM inachuana vikali na CHADEMA. Majimbo hayo ni Moshi Mjini, Moshi Vijijini, Vunjo, Rombo, Hai, Siha, Mwanga, Same Mashariki na Same Magharibi.
Kati ya majimbo hayo CCM inaweza kushinda kirahisi Moshi Vijijini, Mwanga na Same Magharibi, kwingine utabiri ni mgumu.
Moshi Vijijini Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyrill Chami anayepewa nafasi kubwa ya kushinda, anachuana na Anthony Komu wa CHADEMA. Mwanga; Waziri Profesa Jumanne Maghembe mambo yake si mabaya kama ilivyo kwa Naibu Waziri, Dk. David Mathayo anayegombea Same
Magharibi.
Majimbo ambayo ushindani ni mkali na lolote linaweza kutokea ni mchuano ambako mchuano ni kati ya CHADEMA, TLP na CCM. John Mrema (CHADEMA), Chrispin Meela (CCM) na Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, karibu wananguvu sawa, ingawa inaelezwa kuwa John Mrema ameanza kuwazidi maarifa wenzake.
John Mrema anapewa nafasi zaidi kutokana na mgombea wa CCM, Crispin Meela na wa TLP Agustine Mrema kulumbana mara kwa mara hasa baada ya Mrema wa TLP kuanza kumnadi mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete. Inaelezwa kuwa hali hiyo inampa nafasi nzuri John Mrema kujipambanua kwa wananchi kuwa ndiye bora.
Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo wa CHADEMA anaendelea kumburuza mpinzani wake, Justine Salakana wa CCM anayepewa nafasi finyu kushinda hasa kutokana na kukosa ushirikiano wa kutosha kutoka kwa washindani wake katika kura za maoni. Kwenye kura za maoni alishika nafasi ya tatu.
Kutoka Hai, uchunguzi unabainisha kuwa Freeman Mbowe, mwenyekiti wa CHADEMA hana upinzani mkali kutoka kwa Mbunge aliyemaliza muda wake, Fuya Kimbita wa CCM. Watani wa kisiasa jimboni humo wanasema Mbowe anasubiri kuapishwa tu.
Wagombea wa CCM kwenye Jimbo la Rombo, Basil Mramba na Aggrey Mwanri (Siha), Anne Kilango (Same Mashariki), wanakabiliwa na upinzani kutoka kwa wagombea wa CHADEMA. Joseph Selasini kuchuana na Mramba (Rombo), Naghenjwa Kaboyoka kuchuana na Kilango (Same) huku Mwanri akichuana na Mhandisi Humprey Tuni.
Kati ya majimbo hayo upepo wa kisiasa si mzuri kwa Mwanry ikidaiwa kuwa uongozi wa chama wa wilaya umeomba msaada wa uongozi wa CCM Taifa ili Jakaya Kikwete arudi kufanya kuokoa jahazi.
Katika majimbo hayo yenye ushindani wa kisiasa changamoto kubwa kwa CCM ni kufanya kampeni mbili; kwanza, kuvunja makundi yaliyozaliwa kwenye kura za Maoni. Pili, kunadi sera na kuomba kura kwa wananchi.
Lakini Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro Steven Kazi katika mahojiano ya simu na Raia mwema alidai CCM ina uhakika wa zaidi ya asilimia 90 kushinda majimbo yote hayo.
“Tuna nafasi kubwa ya kushinda katika majimbo karibu yote,vyama vya upinzani havina nguvu kama watu wanavyoelezea…..wananchi wa Kilimanjaro wanaikubali CCM na hawawezi kufanya makosa kuchagua upinzani,” alisema.
Kauli hiyo inapingwa na Katibu wa CHADEMA Basil Lema akisema chama chake kina uhakika wa kuongeza idadi ya majimbo kutoka moja la Moshi Mjini hadi majimbo matano au sita.
Katika Mkoa wa Arusha wenye majimbo saba ya Arusha Mjini, Arumeru Magharibi, Arumeru Mashariki, Monduli, Karatu, Longido na Ngorongoro hali si tofauti na Kilimanjaro.
Mkoani humo CCM ina matumaini ya kushinda majimbo ya matatu tu ambayo ni Ngorongoro, Monduli na Longido. Majimbo ya Arusha Mjini, Arumeru Magharibi, Arumeru Mashariki na
Karatu kushinda au kushindwa kutabainika baada ya kuhesabu kura.
Katika majimbo ya Ngorongoro mgombea wa CCM Sanig’o ole Telele anaweza kushinda kwa urahisi kutokana CHADEMA kuweka mgombea asiye na nguvu kisiasa Moringe ole Parkipuny, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa jimboni humo miaka ya 1990.
Jimbo la Monduli Edward Lowassa hana upinzani wa kutisha kutoka kwa Mchungaji Amani Silanga Mollel wa CHADEMA na Longido mgombea wa CCM, Michael Lekule Laizer hana upinzani wa kutisha kutoka kwa Paulina Laizer wa CHADEMA ambaye aliondoka CCM baada ya kushindwa kura za maoni za ubunge wa Viti maalumu.
Katika Arusha Mjini mgombea wa CCM Dk. Batilda Burian ambaye alishinda kwa kishindo katika kura za maoni anapambana na Godbless Lema wa CHADEMA na upepo wa kisiasa si mzuri kwake kutokana na madai kuwa baadhi ya viongozi wa CCM wilayani hawamuungi mkono.
Arumeru Magharibi mgombea wa CCM Gudluck Ole Madeye anachuana vikali na mgombea CHADEMA, Mathias ole Kisambo. Karatu, Dk.Wilbroad Lorri wa CCM anapambana na mgombea wa CHADEMA Mchungaji, Yohana Nat’se.
Mwenyekiti wa CHADEMA Karatu, Moshi Darabe alibainisha katika mahojiano na gazeti hili kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu chama chake kimepania kuweka rekodi kutokana na kupanua mtandao wake hasa baada ya kushinda viti vingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Tunatarajia kuvunja rekodi nyingine ya kushinda viti vya udiwani 10 kati ya kata 13 Jimbo la Karatu na napenda kuwatumia salamu CCM kuwa wasahau kupata chochote katika jimbo hili,” alijigamba Darabe.
Jimbo jingine ni Arumeru Mashariki ambako mgombea wa CCM ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi Jeremiah Sumari anapata upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa CHADEMA, Joshua Nasari (25).
Nasari, mhitimu wa Sosholojia na Utawala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ameibua changamoto isiyotarajiwa kutokana na kumudu kujenga hoja na kuwashawishi. Amekuwa akipata wafuasi wengi miongoni mwa vijana na wanawake jimboni humo.
Katika majimbo hayo manne sababu kubwa inayoelezwa kuwa vyama vya upinzani hasa CHADEMA kupata nguvu kunatokana na makundi ya kura za maoni hivyo. Baadhi ya wanachama wanataraji kuwapigia kura kampeni wagombea wa upinzani na wengine wakitoa michango ya fedha na vifaa vya kampeni.
Mkoa wa Manyara wenye majimbo sita ya uchaguzi CCM tayari imetwaa Jimbo la Simanjiro, mgombea Christopher ole Sendeka akipita bila kupingwa. Hata hivyo, CCM kinaweza kupoteza majimbo ya Mbulu na Babati Vijijini.
Katika Jimbo la Mbulu, Philip Marmo ambaye amekuwa mbunge jimboni humo kwa miaka 25 angependa, rekod yake hiyo ipo hatarini kuendelezwa kutokana na mgombea wa CHADEMA, Mwanasheria Boay Akonaay, kumdhibiti.
Jimboni humo hali si shwari kwa CCM kisiasa kutokana na wakazi wengi wakiwa kabila la Wairaq wanaotajwa kukusudia kufuata nyayo za jirani zao, Jimbo la Karatu. Upinzani dhidi ya Marmo ulijidhihirisha wakati wa ziara ya mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete ambaye alizomewa na baadhi ya waliohudhuria mkutano huo hali iliyosababisha polisi kupiga mabomu ya machozi kuwatanya wananchi hao.
Katika jimbo la Hanang Dk.Mary Nagu anapambana na Rose Kamili ambaye aliwahi kuwa Mke wa mgombea urais wa CHADEMA Dk.Wilbroad Slaa ingawa Nagu anapewa nafasi ya kushinda lakini chochote kinaweza kutokea na hali kama hiyo pia ipo Babati Mjini ambako Kiseryi Chambiri wa CCM anapambana na mgombea wa CHADEMA, Pauline Philipo Gekul.
Jimbo la Babati Vijijini mgombea wa CCM Jitu Soni ambaye ana asili ya Kiasia anapambana na Larent Tarra wa NCCR-Mageuzi na huenda pia CCM ikapoteza jimbo hilo kutokana na kukubalika kwa mgombea wa NCCR ambaye mwaka 2005 alishindwa kura chache sana na Damas Nakei wa CCM.
Kutoka mkoani Mara mwandishi wetu anaripoti; Majimbo ya Serengeti na Tarime ametawaliwa na siasa za ukabila na koo lakini Musoma Mjini, CCM kinakabiliwa na hali mbaya kutoka kwa wagombea wa CHADEMA.
Uchunguzi unabainisha kuwa Serengeti, mgombea wa CCM, Kebwe Stephen Kebwe anatafunwa na siasa za ukabila ambao msingi wake ni mpasuko ndani ya chama hicho wakati wa kura za maoni.
Wakati wa kura za maoni CCM kulikuwa na wagombea wanne wakitazamwa zaidi kwa makabila yao na wenzao kwenye chama hicho; Wakurya wawili ambao ni Dk. James Wanyancha aliyekuwa akitetea nafasi hiyo na Stephen Magoiga. Dk Kebwe ni kabila la Mungoreme na Daniel Muhochi ambaye ni Mwisenye.
Inadaiwa kuwa wakati wa kura hizo za maoni Dk. Kebwe alipata kura nyingi za Wangoreme ambao ni mojawapo ya makabila makubwa wilayani Serengeti huku wagombea wengine wakipata ‘namba za viatu’ katika eneo hilo.
Baada ya kura hizo za maoni inaelezwa wapinzani wa Dk Kebwe kupitia kwa wafuasi wake walieneza ‘sumu’ kuwa alishinda kutokana na ukabila kwa madai kuwa alipata kura nyingi kwa watu wa kabila lake huku wagombea wa makabila mengine wakiambulia kura chache.
Mmojawapo wa wagombea hao ambaye alikuwa na matumaini makubwa ya kushindwa inadaiwa kuwa alianza kutumia wazee wa Kimila kushawishi Wakurya na Waisenye wasimchague Dk. Kebwe kwa sababu Wangoreme hawakuwapigia kura wagombea wa makabila mengine ya Wakurya na Waisenye.
“Unajua baada ya kura za maoni mwenzetu (anamtaja) alianza kueneza sumu ya ukabila. Akawa anatumia wazee na vijana ambao ni wafuasi wake wa Kikurya na Waisenye kusema kuwa wasimpe kura Mungoreme kwasababu wakati wa kura za maoni hawakuwapa kura wagombea wa makabila mengine. Bahati mbaya baadhi ya viongozi wa chama wakati wa kura za maoni walieneza ukabila hivyo ikawa ni vigumu kurudi tena kubadili upepo,” anasema kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM wilayani Serengeti.
Anaongeza: “Hata (anamtaja tena) alipoitwa kuja kuvunja makundi ya kura za maoni kwa kumnadi Kebwe alikuwa anasimama jukwaani kumwombea kura mgombea wa urais na wagombea wengine wa CCM. Hakutaka kumtaja mgombea ubunge wetu. Pia kamati ya siasa (CCM-wilaya) ilibaini alikuwa akitusaliti zaidi badala ya kutusaidia.
“Kwa hiyo ikaamua (kamati) kuwa atolewe kwenye kampeni na hata asiwepo hapa jimboni make alikuwa anatuharibia. Vilevile kuna kiongozi mmoja (anamtaja) naye ilionekana ana kigugumizi katika kumnadi mgombea wetu vizuri kwani kwenye kura za maoni alikuwa hamuungi mkono hivyo naye tulisema akae pembeni kidogo.”
Alipoulizwa juu ya hali hiyo Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Chandi Marwa, alikiri kuwapo kwa siasa za ukabila lakini akasema ni siasa zinazozidi kudorora kwa kadiri siku zinavyokwenda kwa kuhusisha juhudi za viongozi wa chama hicho.
“Ni kweli mwanzoni hali ya ukabila ilikuwa ni mbaya sana upepo wa upinzani ulikuwa mkali sana. Lakini sasa tumejitahidi kurekebisha mambo na Kebwe anakubalika hata kwa Wakurya na Waisenye. Unajua kuangusha mtu (Wanyancha) ambaye alikuwa Naibu Waziri lazima kutatokea mtikisiko make ni mbunge wa miaka kumi na alikuwa na wafuasi wake. Lakini niseme tu sasa hivi upepo (wa kisiasa) ni mzuri tu na tutashinda bila wasiwasi,” anasema Chandi ambaye ni ndugu wa Dk. Wanyancha.
Katika hatua nyingine amemtuhumu mgombea wa CHADEMA, Marwa Ryoba ambaye ni Mkurya kuwa ndiye anatumia siasa za ukabila kama mtaji wake wa kupata kura. Hata hivyo mgombea huyo alikanusha madai hayo akisema kuwa hayo ni matatizo ya ndani ya CCM kwani hategemei kura pekee za Wakurya kupata ushindi.
“Mimi nina kura nyingi Majimoto, Kisaka, Ringw’ani, Nyambureti na huko kote ni kwa Wangoreme. Hayo ni maneno ya watu wa CCM. Wao ndiyo wamevugana huko halafu wanataka kunisingizia mimi. Nikiwa mbunge nakuwa wa watu wote wa Serengeti hivyo siwezi kubagua kwa kutumia ukabila,” anasema.
Kwa upande wake Dk. Kebwe anakiri kuwepo na kampeni za ukabila ambazo zimeenezwa zaidi na waliokuwa wapinzani wake wakati wa kura za maoni ndani ya CCM.
“Ni kweli hilo lipo lakini kwa sasa limepungua. Hivi sasa wamebaki watu wachache hasa vijana lakini kwa wazee tumejitahidi kuongea nao na wametuelewa. Naweza kusema kwa sasa hilo siyo tatizo kubwa sana na tuna uhakika wa kushinda”. Anasema.
Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa mkuu wa wilaya hiyo Edward ole Lenga amekuwa akifanya kazi ya ziada kukutana na wazee wa Kikurya na Waisenye ili kuondoa ‘fitina’ hiyo ya ukabila.
Kadhalika juzi Jumatatu Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kutoka mkoa wa Mara alilazimika kuwaita baadhi ya wazee kutoka sehemu mbalimbali za jimbo hilo ili kuweka mambo sawa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi Jumapili ijayo.
Wakati jimbo la Serengeti likiwa limetawaliwa na ukabila, katika jimbo la Tarime, nguvu ya koo ndiyo imetawala kutokana na wagombea wote wenye nguvu kutokea koo moja.
Wagombea hao, Charles Mwera (CUF) ambaye ni mbunge aliyemaliza muda wake, Nyambari Nyangwine (CCM) na Mwita Waitara (CHADEMA) wanatoka koo ya Wairege (Ingwe) ambayo ndiyo ina idadi kubwa ya watu kuliko koo nyingine. Koo ya Wairege ina kata 9 kati ya kata 30 za jimbo hilo lenye zaidi ya koo 11.
Mgombea mwingine mwenye nguvu ni Peter Wangwe (NCCR-Mageuzi) ambaye ni mdogo wake marehemu Chacha Wangwe aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya kupata ajali na kufariki mwaka juzi. Huyu anatoka koo ya Watimbaru (Inchage).
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kuwa historia ya uchaguzi katika jimbo hilo huegemea zaidi katika koo hivyo kutokana na wagombea watatu wenye nguvu kutoka koo moja ya Wairege kunafanya mshindi kutotabirika mpaka sasa.
Wakazi kadhaa waliozungumza na Raia Mwema katika jimbo hilo wanasema kuwa mshindi atategemea zaidi anavyokubalika katika koo zingine kwani katika koo ya Wairege wote watatu watagawana kura.
Aidha uamuzi wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Mwera kuhamia CUF kutoka CHADEMA baada ya kushindwa na Waitara kwenye kura za maoni na hatua ya mdogo wake marehemu Chacha Wangwe kugombea kwa tiketi ya NCCR Mageuzi kunaelezwa kuwa kutafanya wapinzani kugawana kura hivyo kuinufaisha CCM.
“Ninavyoona wapinzani wanaweza kugawana kura halafu ukashangaa CCM inashinda make mwaka huu wote wenye nguvu wanatoka koo moja halafu kuna huyu wa NCCR naye anakubali kwenye koo yao na zile zingine ambazo siyo Wairege. Kule kwa Wairege Mwera anakubalika na Nyangwine lakini pia huyu wa CHADEMA naye ana watu make ndiyo chama tawala hapa (Tarime)”. Anasema mzee Mwita Chacha mkazi wa Nyamongo.
Anaongeza: “Huyu wa CCM anaweza kupata tabu kwenye koo ya Wanyabasi, Watimbaru, Wakira, Wanyachari, Wanyari, Wasweta na Walunyaga make kwenye kura za maoni alimshinda (Christopher) Kangoye ambaye ni Mnyabasi na wao wanadai alimfanyia hujuma hivyo wanaweza kupigia upinzani. Habari za uhakika kutoka ndani ya CCM wilayani Tarime zinasema kuwa Kangoye ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza ameitwa mara kadhaa kwenda kusaidia kuondoa mpasuko huo wa koo.
Mwera ambaye alikuwa pia diwani kata ya Nyanungu na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo bado ana ushawishi mkubwa jimboni humo na inadaiwa kuwa kama ilivyokuwa kwa marehemu Chacha Wangwe tofauti zake kimtizamo na mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA Freeman Mbowe ndiyo zilisababisha asiteuliwe kugombea kwa tiketi ya chama hicho hata kama alikuwa mshindi wa pili. Mwera pia anagombea udiwani wa kata ya Itiryo baada ya kata ya Nyanungu kugawanywa.
Hali ya kukosekana kwa mgombea mwenye nguvu kuliko wengine katika jimbo hilo pengine inaweza kuonekana kutokana na kukosekana na ule msisimko wa kisiasa ambao unakuwepo nyakati za uchaguzi.
Mgombea wa CHADEMA, Waitara anakiri kuwa uchaguzi huo umetawaliwa na nguvu ya koo huku akimtuhumu mgombea wa NCCR- Mageuzi kwa kutumia njia hiyo ili kujipatia kura.
“Tuna uhakika wa kushinda ingawa kuna hili tatizo la koo. Na wanaoneza haya maneno ya koo ni NCCR Mageuzi. Anasema eti kwavile wagombea wengine wote ni Wairege, koo zingine zimchague yeye Mtimbaru” anasema. Hatahivyo Wangwe hakuweza kupatikana kujibu tuhuma hizo.
Pengine katika mkoa wa Mara zile zinazoitwa siasa za Tarime hivi sasa zimehamia katika jimbo la Musoma Mjini ambako kuna mchuano mkali kati ya mbunge aliyemaliza muda wake Vedastus Mathayo Manyinyi na mgombea wa CHADEMA Vincent Kiboko Nyerere. Vincent ni mtoto wa Josephat Kiboko Nyerere ambaye ni mdogo wake Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Mpasuko mkubwa wa kisiasa ndani ya CCM mkoa wa Mara ndio mtaji mkubwa wa mgombea huyo wa CHADEMA huku kukiwa na taarifa kuwa anaungwa mkono na viongozi wandamizi wa CCM mkoani humo.
Siasa za makundi mkoani humo zinaonekana kumwelemea Mathayo ambaye baadhi ya viongozi wa chama hicho wanamtuhumu kwa ‘kukivuruga’ chama kwa nguvu yake ya pesa.
Inaelezwa kuwa viongozi waandamizi wa CCM mkoani humo hawajawahi kuhudhuria kampeni za kumnadi mgombea huyo mpaka pale alipofika mgombea urais Jakaya Kikwete na mgombea mwenza Dk Mohamed Gharibu Bilal na kwamba na hata walipopata fursa ya kuzungumza walitumia falsafa ya chama hicho ya mafiga matatu kwa kukwepa kutaja jina la Mathayo.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara Makongoro Nyerere ambaye ni kaka yake mgombea wa CHADEMA ameonekana katika baadhi ya majimbo nje ya ya mkoa huo akiwanadi wagombea wa chama chake lakini amekuwa adimu kwenye mikutano ya kampeni ya Mathayo.
Ni katika jimbo hili ambako ulinzi wa jeshi la polisi umeimarishwa katika mikutano yote ya kampeni na hata katika mitaa ya katikati ya mji kama ilivyokuwa kwenye chaguzi za Tarime na hivi karibuni wafuasi wa vyama hivyo vya CHADEMA na CCM walijeruhiana katika vurugu.
Chanzo: www.raiamwema.co.tz
No comments:
Post a Comment