CHAMA cha Wananchi (CUF) kimedai kuwapo viongozi waandamizi wa siasa, wanaopingana na maridhiano na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wenye malengo ya kutaka kuvuruga uchaguzi.
Hayo yamesemwa na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho, ambaye pia ni Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, katika mikutano ya kampeni kisiwani hapa mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Inasikitisha, kwamba tunakazania kudumisha amani, umoja na maridhiano, lakini kuna baadhi ya viongozi wanaofanya njama za chinichini kujaribu kuvuruga lengo hili na kuturudisha kwenye mgogoro.
Wanajaribu kujipenyeza katika mchakato wa uchaguzi na wapiga kura,” alisema Maalim Seif katika mikutano ya kampeni Pemba.
Alikwepa kuwataja majina au vyama vyao, lakini akawataka Wazanzibari kuwapuuza akisema wamekuwa wakikutana usiku kupanga mipango yao hiyo michafu, na kuhimiza amani na utulivu vilindwe.
Katika mikutano ya kampeni aliyoifanya katika uwanja wa Gombani, jimbo la Chake Chake na Pujini jimboni Chonga, Ijumaa na Jumamosi, Maalim Seif aliahidi kulinda maridhiano ya kisiasa akisema ni amali muhimu kwa maendeleo.
Aliwaomba wapiga kura kumpa nafasi ya kuwa rais wa Zanzibar, ili aiendeleze Zanzibar ikiwa ni pamoja na suala linalosubiriwa la uchimbaji wa mafuta na gesi asilia visiwani hapa.
Alifanya ziara fupi katika kijiji cha Tundaua ambako utafiti wa rasilimali hiyo ulifanyika mwaka 1961. Aliahidi kuendeleza kilimo na uvuvi ili kutengeneza ajira na kukomesha uzembe visiwani.
“Tunataka kuzalisha chakula cha kutosha; hii inawezekana kwa kuwa na mipango inayotekelezeka na kuwa na uongozi wenye ari.
Mimi ndiye ninayestahili kuongoza Zanzibar kupita katika kipindi hiki cha changamoto za kijamii, kiuchumi na kisiasa,” alisema.
Mgombea uwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, alisisitiza kwamba chama chake kitashirikiana na Serikali ya Muungano kutatua matatizo yaliyopo ya Muungano.
“Hakuna anayefikiria kuvunja Muungano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara. Hakuna shaka kwamba Muungano ni muhimu kwa maendeleo yetu,” Jussa alisema hayo katika mkutano wa hadhara Kikwajuni.
Aliwataka wanachama wa CCM kuchagua wagombea wa CUF na Seif kwa ajili ya maendeleo yao.
Naye Oscar Mbuza anaripoti kwamba Mkuu wa Mkoa katika Serikali ya Kwanza ya Rais Abeid Amaan Karume, Abdulazak Simai ‘Mzee Kwacha’, amechafua hali ya hewa kisiasa visiwani hapa.
Mzee Kwacha alifanya hivyo juzi baada ya kumtaka mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, kuwa makini na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa atakayoiunda.
Mzee Kwacha aliyepewa nafasi ya kumkaribisha Dk. Shein kwa niaba ya wazee wa mji wa Paje, mkoa wa Kusini Unguja, kabla ya mgombea huyo kuhutubia mkutano wa hadhara, aliwaacha midomo wazi maelfu ya watu waliohudhuria mkutano huo baada ya kumshambulia kwa maneno makali, Maalim Seif.
Huku watu wengi wakishikwa na butwaa kutokana na aina hiyo ya siasa kutoonekana kwenye kampeni za uchaguzi wa Zanzibar mwaka huu, Mzee Kwacha alimtaka Dk. Shein kuwa makini na Maalim Seif, akidai ataiuza Zanzibar akiingia madarakani.
Maneno ya mzee huyo, yalimfanya Dk. Shein aliyekuwa anamsikiliza kwa makini kuweka mikono kichwani akiwa kama vile haamini kusikia mzee huyo akitoa maneno hayo makali hadharani.
“Huyu tulikuwa naye ndani ya CCM na aliwahi kushika nyadhifa za juu sana, kwanza tulimpa uwaziri wa utalii, halafu tukamfanya kuwa Waziri Kiongozi, lakini hakutosheka ….
“Seif alitusaliti, tunakuomba uwe naye makini, sisi wananchi wa Zanzibar tutasimama kidete kuhakikisha hapati nafasi hata kidogo ya kuiyumbisha Serikali yako,” alisema Mzee Kwacha.
“Napenda kuwaambia hawa vijana wasiojua historia ya nchi yetu, Mzee Karume (Abeid), na viongozi wengine nikiwamo mimi tulipigania kuikomboa nchi hii, hatuwezi kukubali kuona watu wanataka kuirudisha Zanzibar kwenye Ukoloni tena.
“Angalia hapa Paje, leo hii maisha mazuri nyumba zinapendeza na barabara zinaboreshwa,” alisema.
Kauli ya mzee huyo iliwafanya maelfu ya wana CCM katika mkutano huo kulipuka kwa shangwe, lakini viongozi wakionekana kutopendezwa na kauli hiyo, katika kile
kilichotafsiriwa kuwa ni kutokana na maridhiano ya kisiasa baina ya CCM na CUF, ambayo yanaifanya Zanzibar kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, baada ya uchaguzi mkuu ujao.
Kutokana na maridhiano hayo, siasa za Zanzibar zimebadilika sana ikilinganishwa na miaka ya nyuma na maneno ya kashfa hayapewi nafasi katika mikutano ya kampeni ya CCM na CUF, badala yake vijembe vya kawaida vya siasa ndivyo vinavyotamba hivi sasa.
No comments:
Post a Comment