UTAFITI wa Kampuni ya Synovate uliodaiwa kuonesha mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa akiongoza, umetolewa rasmi jana ukiwa na tafsiri tofauti kuhusu sifa za uongozi kwa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, aliyeibuka mshindi katika kura hizo za maoni.
Sifa hizo za uongozi, ikiwemo ya kuaminika, ametajwa kuwa nayo na idadi ya Watanzania wanaompa sifa hiyo kuwa kubwa (84%) kuzidi matarajio ya tathimini ya awali ya ushindi wake kwa mujibu wa chama chake cha CCM ya asilimia 80 na sifa nyingine ya utendaji bora, akipewa na Watanzania wanaokaribia matarajio hayo (78%).
Hata hivyo, wakati Kikwete akipewa sifa hizo na idadi kubwa ya Watanzania waliohojiwa na kampuni hiyo kati ya Septemba 5 hadi 16, Watanzania hao walipoulizwa watamchagua nani katika uchaguzi wa Oktoba 31, awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, asilimia 61 tu ndio walisema watamchagua mgombea huyo wa CCM.
Lakini kati ya walioulizwa watampigia nani kura katika uchaguzi ujao, asilimia 13 ya waliohojiwa katika mikoa yote nchini, hawakupenda kutoa maoni yao kwa madai kuwa ni siri yao.
Meneja wa kampuni hiyo nchini, Aggrey Oriwo alipokuwa akitoa matokeo ya utafiti huo alisema endapo waliokataa kujibu swali hilo, wangepiga kura katika utafiti huo, asilimia 70 wangempigia Rais Kikwete, Dk Slaa asilimia 18 na Profesa Lipumba pamoja na vyama vingine vya siasa wangepata asilimia sita.
Oriwo mbali na kusisitiza kuwa kampuni yake haitambui matokeo yaliyotolewa na Chadema yakimpa ushindi Dk. Slaa, lakini pia alitetea utafiti wao kuwa unatoa matokeo yenye uhakika wa asilimia 95.
Utafiti mwingine wa Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pia ulitoa matokeo yanayoonesha sifa za ushindi wa mgombea huyo wa CCM.
Katika utafiti huo ambao umeshapingwa na CCM kuwa umewapunja ushindi wao na kupingwa pia na vyama mbalimbali vya upinzani kuwa umeipendelea CCM, ushindi wa Rais Kikwete ulionesha sura mbili tofauti.
Katika sura ya kwanza ya ushindi huo, Watanzania waliulizwa kama uchaguzi ungefanyika siku utafiti huo ulipofanyika, wangemchagua mgombea wa chama gani katika nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, asilimia 71 ya wahojiwa wakasema mgombea wa CCM.
Lakini wananchi hao katika utafiti huo wa Redet, walipotakiwa kutaja jina la mtu mmoja ambaye wangependa kumchagua ili awe Rais wa Tanzania, asilimia 68 walimtaja Rais Kikwete.
Matokeo hayo yalionesha tofauti ya ushindi wa Rais Kikwete kama mtu Watanzania wanayemtaka awe rais, na mgombea wa chama wanayemtaka kuwa rais.
Katika utafiti wa Synovate katika sifa ya ushindi wa kiongozi ya kuaminiwa na wananchi, Watanzania waliohojiwa na kampuni hiyo, waeleze ni kwa kiasi gani wana imani na taasisi au watu waliotajiwa, Rais Kikwete aliibuka na ushindi wa asilimia 84, huku Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Nchikavu na Majini (Sumatra) ikishika nafasi ya mwisho kwa kuaminiwa ya asilimia 44.
Nafasi ya pili ya mtu, au taasisi inayoaminiwa na Watanzania wengi imeshikwa na Baraza la Mawaziri (68%) na kufuatiwa na taasisi za fedha (52%), taasisi za huduma ya afya na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) zilizofungana kwa kupata asilimia 50.
Taasisi au mtu waliotajwa katika sifa ya kuaminiwa na Watanzania ni vyama vya upinzani (48), Shirikisho la Wafanyakazi (Tucta) na Mahakama zilizofungana kwa kupata asilimia 47, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) iliyoshika nafasi ya saba kwa asilimia 46 ya kuaminiwa huku Jeshi la Polisi likishika nafasi karibu ya mwisho kwa kupata asilimia 45.
Katika sifa ya utendaji bora, Watanzania hao 2,000 walipoulizwa, unatathimini vipi utendaji na viongozi na taasisi walizotajiwa, asilimia 78 walisema utendaji wa Rais Kikwete ni bora.
Makamu wa Rais na mgombea wa CCM wa urais Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein alipata asilimia 77 ya utendaji bora huku Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), likishika mkia kwa kuambulia asilimia 30.
Aliyeshika nafasi ya tatu katika utendaji bora wa mtu au taasisi ni Spika wa Bunge na mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Urambo Mashariki, Samuel Sitta na kufuatiwa na vyombo vya habari (72%), wanamuziki wa Tanzania (59%), Baraza la Mawaziri (58%).
Wengine katika ubora wa utendaji ni asasi zisizokuwa za kiserikali (57%), watumishi wa umma (41%), Tucta asilimia 40, taasisi za afya (39%), Sumatra iliyopata asilimia 37, Jeshi la Polisi likishika nafasi karibu na mwisho katika utendaji bora kwa kupata 33%.
Kuhusu mtu ambaye Watanzania watampigia kuwa rais Oktoba 31, Rais Kikwete aliongoza kwa kupata asilimia 61 na kufuatiwa kwa mbali na mgombea urais wa Chadema, Dk. Slaa (16%), mgombea urais wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba aliambulia asilimia 5 tu.
Alisema katika dodoso inayohoji juu ya utendaji wa serikali inayomaliza muda wake ya awamu ya nne, asilimia 50 ya waliohojiwa walionesha kuridhika na utendaji wa serikali hiyo huku asilimia 24 wakionesha kutoridhika na wengi wa wahojiwa walionesha kuridhika ni kutoka vijijini.
Oriwo alisema katika dodoso ya utendaji wa serikali katika kutoa huduma za jamii, asilimia 83 hawakuridhika na utolewaji wa ajira huku asilimia 72 wakionesha kutoridhika na bei ya vyakula ingawa waliohojiwa wengi walionesha kuridhika na utolewaji wa huduma ya elimu ya msingi na sekondari pamoja na hali ya usalama.
Alisema kwa upande wa waliohojiwa kuhusu ushiriki wao katika kupiga kura siku ya Oktoba 31, mwaka huu, asilimia 83 walisema watapiga kura, asilimia 16 walisema hawatopiga kura na kati yao asilimia 30 walitaja sababu za kutopiga kura kuwa hati zao hazijaboreshwa na asilimia 27 walisema ni kutokana na kuchoshwa na siasa.
Watanzania walipoulizwa iwapo wangepewa nafasi ya kuchagua baadhi ya vijana waliojitokeza na wenye vipaji vya uongozi katika nafasi ya urais, asilimia 38 walisema wangemchagua Zitto Kabwe, asilimia 15 walimtaja Dk Hussein Mwinyi na asilimia 12 Makongoro Nyerere.
Kwa upande wa umaarufu wa vyama vya siasa, utafiti huo ulionesha asilimia 64 ya wahojiwa waliitaja CCM, asilimia 22 Chadema, CUF asilimia saba na asilimia tano walitaja vyama vingine huku asilimia mbili wakisema hawajui.
Aidha kati ya watu hao waliohojiwa ni asilimia 38 ndio walikiri kushiriki katika mchakato wa kura za maoni za kuteua wagombea.
Alisema kuhusu utendaji wa wabunge katika Bunge lililovunjwa asilimia 20 walimtaja Zitto Kabwe kuwa alifanya vizuri, akifuatiwa na Dk Slaa kwa asilimia 11 na asilimia tatu walimtaja Harrison Mwakyembe, Anna Kilango na John Magufuli.
No comments:
Post a Comment