Wednesday, January 6, 2010

Seif, Karume waitibua CCM

-Yadaiwa wamekwenda kinyume cha maagizo ya NEC Butiama
-CUF: Ni uoga wa vigogo CCM

MARIDHIANO ya Rais Amani Karume na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad yamewachanganya wana Chama Cha Mapinduzi (CCM), na hasa wa Zanzibar, wanaoona kuwa ni mbinu ama ya kuendeleza utawala wa Karume au kumlinda kama ikilazimu Seif ndiye akawa mkuu wa nchi, Raia Mwema imeambiwa.

Tayari vigogo kadhaa wa CCM Zanzibar wameanza kuamini kuwa maridhiano hayo yanaweza kuhitimishwa kwa Rais Karume, kuwania tena urais wa Zanzibar, baada ya Katiba ya Visiwa hivyo kufanyiwa mabadiliko mahsusi.

Aidha, vigogo hao ambao wengine wangetamani kumrithi Karume, wanayatazama maridhiano hayo kwa hadhari kubwa, wakiamini kuwa yanakwenda kinyume cha maelekezo ya mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) iliyokutana kijijini Butiama, mwishoni mwa mwaka jana.

Katika kikao hicho cha NEC iliazimiwa kuwa Serikali ya mseto iundwe baada ya kufanyika kwa kura ya maoni Zanzibar (referendum), ambayo yatakuwa chanzo cha mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar.

Hata hivyo, baada ya kikao hicho CUF walipinga wakisema hapakuwa na haja ya kura za maoni na kwamba mabadiliko ya Katiba yamekuwa yakifanyika kila inapobidi kwa kuzingatia hali halisi na mahitaji ya nchi kwa wakati husika.

Kutokana na msuguano huo, CUF walikataa kuendelea na mazungumzo ya muafaka wakitaka utekelezaji lakini CCM, akiwamo Rais Jakaya Kikwete walitoa wito wakitaka warejee kwenye meza ya mazungumzo.

Lakini upepo umegeuka wiki kadhaa zilizopita, baada ya Rais Karume na Seif kukutana katika kikao kisicho rasmi lakini kilichoonekana kuwa na nguvu kuliko hata vikao vilivyokuwa na nguvu za kisheria.

Katika kikao hicho kulifikiwa maridhiano ambayo matokeo yake ni pamoja na CUF kutambua urais wa Karume, na yeye kuwateua baadhi ya viongozi wa CUF kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, akiwamo Juma Duni Haji.

Wakati hayo yote yakitokea mtafaruku umeibuka CCM Zanzibar, Karume na Seif wakitajwa kuwa na ajenda zenye malengo ya kuwanufaisha kama timu mpya ya watu wawili, iliyolenga kubeba siasa za Visiwa hivyo.

Wao wenyewe wamekuwa wakinukuliwa kusema kwamba kwa hali ya siasa zilivyo tete Zanzibar wanaona kwamba bila hatua kama hii uchaguzi wa mwakani unaweza kuzua machafuko makubwa ambayo yataweza kusababisha hata damu kumwagika.

Kwa hali hiyo wamedai kwamba wao kama viongozi hawawezi kuruhusu hayo yatokee na hivyo wameingia katika maridhiano kuepuka wao kama watu binafsi kushitakiwa baadaye katika Mahakama ya Kimataifa ya The Hague, Uholanzi kwa kusababisha maafa.

Kwa nyakati tofauti, vigogo ndani ya CCM wameieleza Raia Mwema kuwa kuna uwezekano wa kutaka kuunda serikali ya mseto Zanzibar, ndoto ambayo haiwezi kutimia hadi Katiba ibadilishwe na mabadiliko hayo yatahitaji muda jambo ambalo litalazimu Rais Karume kubaki madarakani mwakani, hadi uchaguzi ufanyike, hoja ambayo inaelezwa pia kubeba ajenda ya viongozi hao wa vyama pinzani.

Hoja nyingine inayochomoza ni kwamba mkewe Rais Karume, Shadya ana Upemba kiasi kwa kuwa mama yake ana asili ya Pemba, ikibidi Seif kuibuka kuwa kiongozi mkuu wa Zanzibar, familia ya Karume, ambaye inadaiwa sasa ana mali nyingi zinazomfanya abandikwe jina la Hapa Pangu itazidi kuwa katika neema endapo itafanikisha ushindi wa Maalimu Seif Shariff Hamad, kuwa Rais ajaye wa Zanzibar, ikidaiwa na vigogo hao kuwa hayo ni sehemu ya makubaliano yao ya siri.

Kama si Maalim Seif, vigogo hao wameieleza Raia Mwema kuwa mabadiliko ya Katiba mahsusi kuruhusu serikali ya mseto, yanaweza kumbakisha kwa muda Karume na baada ya baadhi ya vipengele kumruhusu agombee kwa mujibu wa Katiba hiyo mpya au yenye mabadiliko, na ikiwa hivyo naye pia atalinda maslahi ya Maalim Seif, kwa hoja ya mwingiliano wa asili ya familia (kutoka Pemba).

Lakini duru huru za habari zimedokeza kuwa msingi wa Rais Karume na Seif kuridhiana katika wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu, ni kuhofia machafuko na vifo na hivyo kuepusha mashitaka ya mauaji, kama ilivyo kwa Omar Bashiri wa Sudan, anayewindwa kufikishwa mahakamani The Hague kwa makosa anayodaiwa kuruhusu ukiukwaji wa haki za binadamu Darfur.

Kutokana na hofu hiyo ya baadhi ya vigogo wa CCM Zanzibar, Raia Mwema iliwasiliana na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, kujua maazimio ya NEC iliyokutana Butiama kuhusu kura ya maoni yamefutika vipi na jambo gani hasa linaloendelea kwa kuzingatia mwongozo wa CCM kama chama kwenda kwa Rais Karume.

Lakini Makamba alisema yupo likizo na akapendekeza Raia Mwema imtafute Naibu Katibu Mkuu George Mkuchika ambaye hata hivyo alikataa kuweka bayana hali halisi ya mambo.

Soma zaidi

No comments: