MKE wa mchimbaji maarufu wa madini ya tanzanite katika machimbo ya Mererani wilayani Simanjiro, Jacqueline Minja (28), ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake.
Marehemu ambaye pia alikuwa na ujauzito wa miezi minane, ni mke wa Deo Minja ambaye ni mdogo wa mfanyabiashara maarufu mjini Arusha, Anselmi Minja, anayemiliki maduka makubwa katika miji ya Arusha na Nairobi.
Tukio hilo ambalo limewashtua wakazi wengi wa hapa na ambalo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Basilio Matei, lilitokea juzi saa 3.30 usiku nje ya lango la kuingilia nyumbani kwa mchimbaji huyo eneo la Lemara mjini hapa.
Kamanda Matei alisema jana kuwa Jacqueline alipigwa risasi kichwani na mmoja wa watu wawili waliokuwa na pikipiki akiwa ndani ya gari lake aina ya Toyota Nadia wakati akisubiri mtumishi amfungulie lango la nyumba yake.
“Wakati anasubiri kufunguliwa geti, ghafla walitokea watu wawili wakiwa na pikipiki aina ya Toyo rangi nyekundu na mmoja alishuka na kumfuata na kumwuliza aliko mumewe, kabla ya kuchomoa bastola na kumpiga risasi iliyompata kwenye paji la uso,” alisema Kamanda Matei.
Alisema baada ya tukio hilo, mtu aliyempiga risasi alipanda pikipiki iliyokuwa akiendeshwa na mwenzake na kutoweka kwa kasi kutoka eneo hilo huku mtumishi aliyekuwa akifungua lango akipiga kelele za kuomba msaada.
“Watu walijitokeza kutoa msaada wa kumkimbiza mama huyo katika Hospitali ya KKKT Selian, lakini alifariki dunia kabla ya kufikishwa hospitalini,” alisema.
Kamanda alisema tukio hilo limeacha maswali mengi kwa polisi na wameshindwa kufahamu iwapo tukio hilo linahusiana na ujambazi au ni mauaji ya kukusudia kutokana na wahusika kutopora chochote.
“Kwa kweli tunajiuliza kama tukio hili linahusiana na ujambazi au ni mauaji ya kupangwa, kwani watuhumiwa hao hawakuchukua chochote … tumehoji ndugu na jamaa wa karibu wa wanafamilia hao, wanasema hawakuwahi kuwa na ugomvi wa aina yoyote na mtu yeyote,” alisema Matei.
“Kwa sasa tumeanzisha uchunguzi mkali wa tukio hilo na mwili wa marehemu uko katika mochari ya Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru ukisubiri taratibu za mazishi kutoka kwa ndugu zake,” alisema Kamanda.
Hata hivyo, moja wa ndugu za marehemu aliyeomba jina lake lihifadhiwe, aliiambia HabariLeo kuwa watu hao waliondoka na funguo za gari na simu ya mkononi ya marehemu.
“Baada ya tukio, tumekuta funguo za gari hazipo na pia simu yake ya mkononi haionekani na tunahisi kuwa majambazi hao waliondoka navyo,” alisema ndugu huyo.
Mji wa Arusha umekuwa na matukio makubwa ya uhalifu unaohusisha mauaji kwa muda mrefu sasa pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Jeshi la Polisi kupambana na matukio hayo, lakini bado kiwango kiko juu.
No comments:
Post a Comment