WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amependekeza kuwepo kwa ukomo wa nafasi ya ubunge kama ilivyo kwa nafasi ya urais na akapendekeza iwe ni miaka 15.
Aliwaambia wahariri wa vyombo vya habari katika mkutano wake jana Dar es Salaam, kwamba hiyo itasaidia kupatikana kwa damu mpya katika uongozi, lakini akabainisha kuwa suala hilo ni gumu kwa baadhi ya wanasiasa.
“Ukiniuliza mimi, nitakwambia inafaa kuweka kipindi maalumu cha ubunge…hii itasaidia kuondoa vimaneno maneno na kutafutana uchawi. Viwepo vipindi maalumu kama ilivyo kwa urais. Nadhani miaka kumi na tano inatosha (vipindi vitatu),” alisema Pinda ambaye ni Mbunge wa Mpanda Mashariki mkoani Rukwa.
Kwa kauli yake, Pinda mwenye umri wa miaka 61, akifanikiwa kuteuliwa na chama chake, CCM na kuchaguliwa tena kuongoza jimbo hilo, atakuwa anamaliza miaka yake mitano ya mwisho aliyojiwekea baada ya kuingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2000.
“Nadhani baada ya miaka kumi na tano, itakuwa imetosha, na hata watu hawatakuparamia, watasema Mzee Pinda tumwache, hawatakupa taabu,” aliongeza Pinda, lakini akawa mwepesi wa kuonesha jinsi pendekezo lake lilivyo gumu kwa kueleza kuwa baadhi yao (wabunge), wangependa waendelee kuwemo katika Bunge.
“Sisi wenyewe ndio lazima tuone haja hiyo, sasa ugumu ni kwamba wengine tunaona tabu kutoka humo, tunataka kuendelea na ubunge tunauhitaji sana…uheshimiwa pekee ni hadhi. Lakini kwa kweli hili lingetusaidia sana. Lakini linahitaji busara. Tulitazame kwa maslahi mapana,” alisema Pinda.
Alisema Mkoa wa Rukwa umeonesha mfano baada ya wabunge wake wawili, Paul Kimiti (Sumbawanga Mjini) na Dk. Chrisant Mzindakaya (Kwela), kutangaza kutosimama tena katika uchaguzi ujao kutetea majimbo yao.
“Rukwa tumetoa mfano, kwa kweli nawapongeza sana wale wazee…na baada ya kutangaza tu wamejitokeza watu wengine, tena wengine maprofesa. Napenda kutoa mwito kwa wazee wengine walione hili, miaka kumi na tano inatosha. Ni busara zaidi,” alisema.
Awali, Pinda aliwachekesha wahariri baada ya kuuliza swali kugusiana suala la uzee, kiasi cha Waziri Mkuu kuhoji kuwa “kwa hiyo, na mimi unaniweka katika kundi hilo (la wazee)? Utakuwa unanionea.”
Alisema kinachoelezwa hapo ni ule utumishi wa muda mrefu katika umma na umri mkubwa, na si kwamba mtu amekaa ubunge kwa miaka mingi.
“Hapa naona wanazungumzia kipindi kirefu cha utumishi wa umma na umri mkubwa. Yaani wanakuona na kuuliza, yaani bado umo, umo tena. Hiyo ndiyo changamoto,” alisema.
Waziri Mkuu alirudi kauli yake aliyoitoa katika salamu za serikali kwenye maziko ya Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa zamani, hayati Rashidi Kawawa, Januari 2, mwaka huu, alipomsifu kwa kustaafu kwa hiyari ubunge baada ya miaka 27 na pia nyadhifa nyingine kwenye Chama Cha Mapinduzi.
Hivi karibuni, baada ya Kimiti na Mzindakaya kutangaza kutogombea ubunge, kumekuwa na mjadala wa kutaka wazee waliokaa muda mrefu bungeni na walioitumikia nchi kwa muda mrefu kuachia ngazi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bunda mkoani Mara ambaye pia ni Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira, alisema hanyimwi usingizi na wanaojitokeza jimboni kwake kwa kuwa nafasi hiyo haina hati miliki.
Hata hivyo, alisema ni vyema wanaowania nafasi hizo wakajitangaza kwa kutumia masuala ya maendeleo badala ya kung’ang’ania kigezo cha uzee na ujana ambacho hakina umuhimu bungeni kwa kuwa chombo hicho kinatumiwa na wawakilishi wa wananchi bila kujali umri.
“Pale bungeni wapo wazee, vijana, walemavu na wazima, cha muhimu ni uwezo wao katika kuwakilisha wananchi wao na kujadili na kuweka mikakati ya kimaendeleo kwa faida ya Watanzania, hakuna sehemu iliyosema bungeni ni sehemu ya vijana,” alisema.
No comments:
Post a Comment