Wednesday, January 20, 2010

Kashfa gari la wagonjwa Ikulu yatupiwa zigo

OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha imesema mkanganyiko uliotokea Ikulu Dar es Salaam juzi, mbele ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu nani anastahili kupokea msaada wa gari la kubeba wagonjwa kati ya halmashauri ya wilaya ya Longido na Ngorongoro, ulitokana na Ikulu kwenyewe.

“Binafsi ninavyofahamu na maandishi (barua) niliyonayo ofisini kwangu, yanaonesha kwamba, gari hilo ni la Longido na si Ngorongoro, sasa sijui ilikuwaje lakini taarifa nilizonazo ni kwamba Mkurugenzi wa Ngorongoro alipata taarifa kutoka kwa Mkuu wake wa Wilaya, ambaye naye alipokea simu kutoka Ikulu kwamba wakachukue gari,” alisema Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha (RAC), Nuru Milao, alipozungumza na gazeti hili kwa simu jana.

Milao, ambaye mbali ya ufafanuzi huo alidai hana taarifa ya kilichotokea Ikulu kwa kuwa yuko nje ya ofisi, kwa shughuli za ukaguzi wa serikali za mitaa, alisema anachofahamu ni kwamba kama Rais amesema gari ni la Longido ni kweli, kwa kuwa hata taarifa za ofisi yake zinaonesha hivyo na si vinginevyo.

Katibu Tawala huyo wa mkoa alisema kama kuna mkanganyiko wowote basi umeanzia Ikulu kwenyewe kwa kuwa kabla hajawa nje ya ofisi kikazi, Mkurugenzi wa Ngorongoro, Kayange Jacob, alimweleza kuwa ameambiwa na Mkuu wa Wilaya (Ngorongoro) kuwa aende Ikulu, wilaya imeitwa kuchukua msaada wa gari la wagonjwa.

“Unajua unapopewa taarifa kama hiyo, tena kutoka Ikulu, huwezi kuhoji sana, lakini hata hivyo Mkuu wa Wilaya (Ngorongoro) naye alielewa kuwa si yeye, alipata wasiwasi, maana alikuwa na taarifa ya msaada kama huo kwa halmashauri ya Longido si yake, ila alivyodai, alikuwa ameona Mkurugenzi wake aende tu, huenda magari yamepatikana zaidi ya mahitaji aliyoahidi Rais Kikwete,” alisema na kuongeza:

“Hata mpaka jana, Mkuu wa Wilaya aliyekuwa akitafutwa kwenye simu na Ikulu baada ya mkurugenzi wake kuchelewa eneo la makabidhiano, ni wa Ngorongoro na si wa Longido, akielezwa katika simu na maofisa wa Ikulu ‘mbona mkurugenzi wako haonekani?’ Na nijuavyo mkurugenzi huyo ni mgeni Ikulu, bila shaka alichanganya aingie kwa mlango gani.”


Milao alisema kama Rais amekataa kumpa wa Ngorongoro, basi yuko sahihi, maana ni kweli alikiahidi kijiji cha Engarinaibo, Longido alipofanya ziara Arusha mwaka jana na taarifa (dokezo) za mkoa zimeshaandikwa kuwa ahadi ya Rais kwa kijiji hicho, imetimia.

Huku akionesha naye kuchanganyikiwa na hali hiyo, alisema watu wengi wamekuwa wakichanganya majina kati ya Longido na Loliondo, jambo linalochangia nyaraka na taarifa nyingi kuchanganywa na kwamba Longido ilipewa taarifa mapema na ofisi ya mkoa kuhusu msaada huo na kuahidi kuwa ingawa mawasiliano ni duni, atawasiliana na halmashauri hizo kupata taarifa zaidi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali aliliambia gazeti hili kuwa alipokea taarifa kwa simu kutoka Ikulu ikimtaka ampeleke Mkurugenzi wake akapokee msaada huo wa gari na kwa kuwa idara zake kadhaa zinauhitaji, hakusita kufanya hivyo.

“Nilipigiwa simu wala si barua, nikaelezwa nimpeleke mkurugenzi akapokee msaada wa gari kutoka kwa Rais, tunauhitaji hapa, hivyo sikuhoji, wala sikuuliza jina la aliyenipigia baada ya kuelezwa kuwa ni Ikulu na asubuhi nikapigiwa tena kama amefika, nikawajibu yupo nje ya lango la Ikulu,” alisema Wawali.

Juzi, Rais Kikwete aligoma kukabidhi gari la msaada la kubeba wagonjwa katika hafla iliyokuwa ifanyike kwenye viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam, baada ya utata kuibuka kuhusu halmashauri inayopaswa kukabidhiwa gari hilo baada ya Mkurugenzi wa Ngorongoro kufika kupokea msaada huo badala ya wa Longido.

Kwa mujibu wa kauli ya Rais Kikwete kwa maofisa wa Ikulu, wakati ulipozuka mkanganyiko huo, gari hilo moja kati ya mawili yaliyokuwa yakabidhiwe, badala yake likakabidhiwa moja, yalitolewa na kampuni ya CMC Automobiles Limited na ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa mwishoni mwa mwaka jana kwa wananchi wa kijiji cha Engarinaibo na kituo cha Afya cha Kamsamba, Mbozi, alipofanya zaira katika mikoa hiyo.

“Mimi mwenyewe nilifika katika kijiji hicho cha Engarinaiko, Longido, nikiwa katika ziara mkoani Arusha, hali niliyoikuta pale katika kituo cha afya cha kijiji, ilinifanya nikaahidi nikipata gari la wagonjwa, nitawapa na si hawa wa Loliondo, hii ni nini! Ni kashfa kubwa hii,” aliwaeleza maofisa wa Ikulu waliokuwa katika tukio hilo akiwamo Katibu wa Rais, Prosper Mbena.

Mwandishi wa Rais Msaidizi, Premi Kibanga, alifafanua mkanganyiko huo kwa waandishi wa habari walioalikwa Ikulu kuandika kuhusu makabidhiano hayo, akikiri kuwapo udhaifu katika mawasiliano na kusema Ikulu inaendelea na mawasiliano ili kumpata anayepaswa kupewa gari hilo na si watu wa Ngorongoro.

Hata hivyo siku hiyo jioni, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu ilisema Rais Kikwete alikabidhi gari moja kwa halmashauri ya Mbozi ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Levison Chilewa alipokea msaada huo kwa niaba ya wananchi wa Kamsamba na maeneo jirani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya CMC Automobiles Limited ya Dar es Salaam, iliyotoa msaada huo wa magari hayo aina ya Land Rover Defender 110 Hard Top yenye thamani ya dola 108,000 za Marekani, Abdul Haji, alimkabidhi Rais Kikwete magari hayo hivi karibuni ikiwa ni kumbukumbu ya mkewe, Claude Haji, aliyewahi kuishi nchini kwa zaidi ya miaka 30 na kusaidia wasiojiweza enzi za uhai wake.

No comments: