Tuesday, January 26, 2010

Mchakato kugawa majimbo waanza

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza uchunguzi wa majimbo ya uchaguzi wa Bunge na kuyagawa kama itahitajika, imeelezwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Omary Makungu, alisema katika kubaini vigezo vitakavyotumika katika kuchunguza mipaka na kugawa majimbo, Tume imezingatia vigezo vilivyotajwa katika Katiba sambamba na utafiti iliyoufanya katika nchi zingine za Afrika, ikiwamo idadi ya watu.

Uchunguzi umeonesha kuwa maeneo mengi yatagawanywa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu wanaozidi wastani wa 206,130 vijijini na watu 237,937 mijini.

Jaji Makungu alivitaja vigezo hivyo kuwa ni mawasiliano, jiografia, idadi ya watu, uwezo wa ukumbi wa Bunge, hali ya uchumi na ukubwa wa eneo husika; pia mipaka ya kiutawala, mazingira ya Muungano na mgawanyiko wa wastani wa idadi ya watu.

“Kwa kutumia vigezo vilivyopo, baada ya Tume kukokotoa, imebainika kuwa mgawanyo wa wastani wa idadi ya watu katika majimbo ya uchaguzi yaliyo katika maeneo ya vijijini ni watu 206,130 na mijini wastani wake ni 237,937, majimbo yatakayokidhi kigezo hiki, ndiyo yatakayoendelea kufikiriwa na vigezo vingine vilivyowekwa,” alisema Makungu.

Alivitaja vigezo vingine vitakavyotumika kugawa majimbo hayo ni pamoja na uzingatiaji wa jimbo moja kutokuwa ndani ya wilaya au halmashauri mbili, kata moja kutokuwa ndani ya majimbo mawili ya uchaguzi, uwezo wa ukumbi wa Bunge na idadi ya viti maalumu vya wanawake.

Alisema Katiba ya Nchi ya Mwaka 1977 imetenga kiasi kisichopungua asilimia 30 kwa ajili ya wabunge wanawake wa viti maalumu, ili kuleta usawa wa kijinsia, hivyo Tume haina budi kuzingatia idadi hiyo ya wabunge.

“Licha ya kuwapo matakwa ya asilimia 50 kwa 50 ya idadi sawa kwa wabunge wanawake na wanaume, mpaka sasa hatujapata uthibitisho wake, hivyo tutazingatia idadi hiyo kama ilivyoainishwa na Katiba,” aliongeza Makungu.

Akizungumzia gharama za uchaguzi huo utakaofanyika baadaye mwaka huu, Mkurugenzi wa NEC, Rajab Kiravu, alisema mchakato wa uchaguzi umegawanyika katika awamu tatu tofauti; ya kwanza na ya pili ilihusisha uboreshwaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura huku awamu ya tatu ikiwa ni uchaguzi wenyewe.

Alisema katika Daftari, zaidi ya Sh milioni 27 zilitumika huku awamu ya pili ikitumia Sh milioni 47 kwa ununuzi wa vifaa vipya zikiwamo kamera huku Uchaguzi Mkuu kwa ujumla ukitengewa kiasi kisichopungua Sh bilioni 64, tofauti na Sh bilioni 63 zilizotumika katika uchaguzi uliopita.

Kuhusu karatasi za kupigia kura, Kiravu alisema kwa kawaida Tume ina utaratibu wa kutangaza zabuni ya kuchapa karatasi hizo na anayeshinda ndiye hupewa. Alikanusha uvumi kuhusu mchakato wa kuchapa karatasi hizo katika moja ya kampuni za uchapaji nchini.

No comments: