MKAKATI wa kuwajibishana katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za baadhi ya vigogo kuunda mitandao ya kisiasa, kuhusika na vitendo vya ufisadi na wengine kutoa matamko makali nje ya vikao vya chama hicho, imekamilika na wakati wowote utekelezaji utafanyika Raia Mwema limeelezwa.
Mambo mawili makubwa yanatarajiwa kujitokeza ndani ya chama hicho. Mosi, vigogo watuhumiwa wa ufisadi kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria. Pili, wenye kutoa kauli kali nje ya vikao vya chama hicho, wakiwamo baadhi ya wabunge watapewa onyo na kutakiwa kuwa makini.
Tayari mkakati huo umeanza kupata upinzani miongoni mwa watu ndani ya CCM na hata baadhi ya wajumbe wa Sekretariati ya chama hicho, ambayo Mwenyekiti wake ni Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.
Mbali na katibu Mkuu wa CCM, sekretarieti hiyo inaundwa na manaibu katibu wakuu wa CCM, ambao ni Saleh Ramadhan Feruzi (Zanzibar) na George Mkuchika (Bara), katibu wa NEC Taifa wa Organaizesheni, Kidawa Yusuf Himid, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Uchumi na Fedha, Amos Makala.
Majukumu ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ni pamoja na kusimamia shughuli zote za utendaji za CCM kitaifa na kuandaa shughuli za vikao vya chama hicho ngazi ya Taifa.
Kwa mujibu wa habari zilizotufikia, katika kikao cha sektretariati hiyo kilichoketi Dar es Salaam hivi karibuni, sehemu kubwa ya wajumbe wake wanaunga mkono chama kuwawajibisha watuhumiwa wenye kashfa za ufisadi wakiwamo wanachama wake ambao wanaelekea kuwa mzigo baada ya kuchukuliwa hatua na vyombo vingine.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa katika kikao hicho ambacho pia kimepanga Kamati Kuu ya CCM, kukutana Januari 23, mwaka huu na NEC kukutana kwa siku mbili, Januari 25 na 26, mjini Dodoma, ni mjumbe mmoja tu aliyeonekana kuwakingia kifua watuhumiwa wa ufisadi ambao kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa kufaidika nao, lakini upingaji wake haukuweza kubadili misimamo ya wajumbe wenzake walio wengi.
Lakini wakati hali ikiwa hivyo, inaelezwa kuwa vigogo wa juu serikalini wamekuwa wakiunga mkono uamuzi huo unaotarajiwa kufanywa na chama hicho na baadhi wakiwa tayari kukumbatia lawama za kiuongozi ikiwa ni hatua ya kumtenganisha Rais Kikwete na chuki zinazoweza kuibuka kutokana na kile kinachoweza kuitwa “uamuzi mgumu”.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa hali ya kujadiliwa kwa watuhumiwa wa ufisadi wakitajwa kuwa na mikakati yao binafsi ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikikisumbua chama hicho imewakera na kuwachosha viongozi wengi waadilifu serikalini na baadhi wakihoji; “wao (kwa majina) ni kina nani kwenye hii nchi hadi wawanyime watu usingizi?”
Vyanzo vyetu vya habari vilivyo karibu na viongozi waandamizi nchini vimedokeza kuwa hatua hiyo inachukuliwa ili kukisafisha CCM mbele ya majukwaa ya kampeni baadaye mwaka huu.
Mwelekeo huo wa kufikia “maamuzi magumu” unatajwa kuhusishwa na kile kinachotarajiwa kujitokeza katika ripoti ya Kamati ya Rais mstaafu, Ali HAssan Mwinyi, itakayowasilishwa kwenye kikao kijacho cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.
Kamati ya Mwinyi inayowashirikisha Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Abdulrahman Kinana, iliundwa na NEC katika kikao chake kilichopita mjini Dodoma ili kutoa mapendekezo ya kumaliza kile kilichotajwa kuwa uhasama miongoni mwa wabunge wa chama hicho pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar waliowahi kupishana kauli na viongozi wa juu wa Serikali ya Muungano.
Tayari imekwisha kuripotiwa kuwapo kwa hali ya mgongano wa kimtazamo miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo katika uandaaji taarifa na kwamba kutokana na mgongano huo, wajumbe wa kamati wanaandaa ripoti tofauti watakazowasilisha kwenye Sekretarieti ya CCM.
Hali halisi ya mwelekeo wa CCM katika Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu, inatajwa kuwa tete zaidi endapo chama hicho hakitafanya uamuzi wowote uliopachikwa jina la “uamuzi mgumu” wa kujitenga na watuhumiwa wa vitendo vya ufisadi, ambao tayari wamewajibika serikalini.
Baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM wanahusishwa na matukio makubwa ya ufisadi, yakiwamo wizi wa mabilioni ya fedha kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na baadhi yao tayari wakiwa wamefikishwa mahakamani na kesi zikiendelea, akiwamo Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM, mkoani Kigoma, Rajabu Maranda.
Mbali na vigogo hao chama hicho kinadaiwa pia ya kuwa kimekuwa kikichangiwa fedha za uchaguzi na baadhi ya wafanyabiashara wanaohusishwa na vitendo vya ufisadi nchini, ambao pia baadhi wamefikishwa mahakamani.
Tayari pia hali ya kuwapo mpasuko imebainika si tu miongoni mwa wabunge pekee bali hata miongoni mwa viongozi serikalini na hasa mawaziri.
Mwishoni mwa mwaka jana, Kamati ya Mwinyi iliwahi kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa imeanza kuparaganyika, ikielezwa kuwa sehemu ya mapendekezo katika taarifa yake ya pamoja kwa ajili ya kuwasilishwa NEC-CCM imevuja.
Katika habari hizo ilielezwa kuwa baadhi ya viongozi CCM wamedokezwa kuhusu mapendekezo ya kamati hiyo, yaliyodaiwa kuwa ni pamoja na kuwang’oa madarakani baadhi ya watuhumiwa.
Kutokana na mapendekezo hayo ya kung’oana, baadhi ya vigogo wanatajwa kuwa na mwelekeo wa kupingana na kamati kwa madai kuwa hiyo ni hatua kali, bila kujali kuwa wanaotakiwa kuachia madaraka ili wabaki wanachama wa kawaida walikwishafanya hivyo kwa kuacha nyadhifa zao serikalini.
No comments:
Post a Comment