Friday, January 15, 2010

Pinda ataja mali zake, ana sh milioni 25 benki

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, jana alitaja mali anazomiliki ambazo miongoni mwake ni nyumba mbili pamoja na akaunti katika benki zenye fedha zisizozidi Sh milioni 25.

“Kama shilingi milioni ishirini na tano ni utajiri, basi nami nimo.” amesema Waziri Mkuu ofisini kwake, Magogoni, Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari vya ndani ya nchi.

Pinda amesema, anamiliki nyumba moja mjini Dodoma na nyingine kwao Mpanda mkoani Rukwa eneo la Makanyagio, na ana kibanda shambani kwake Pugu nje kidogo ya Dar es Salaam.

“Mimi kila mwaka nataja mali zangu kwa Tume, sijaulizwa, sijagombana na Tume. Ukiniuliza ni masikini kiasi gani, nitakwambia nina property (nyumba) Dodoma, nimejenga kwa utaratibu wa serikali wa kuomba mkopo, ninayo nyingine kwetu Mpanda pale Makanyagio,” alisema Pinda.

“Dar es Salaam sina nyumba, pale Pugu nina nyumba kidogo, inahitaji kazi ya ziada…kijijini nilikuwa nafikia kwa babu, babu ana kanyumba kake ka ovyo ovyo…kile ambacho mlikiona, ana vyumba viwili nilikuwa nalala pale, lakini baada ya Uwaziri Mkuu, jamaa wakaniambia aah…haiwezekani pale, nilijua nitaweza kulala pale na hawa jamaa (wasaidizi wake) watalala mjini humo, nikaambiwa hapafai.”

Pinda ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda Mashariki alisema hana gari lolote zaidi ya gari alilopewa kwa kuwa Mbunge, na kwamba katika akaunti zake zote, ana fedha kiasi cha Sh milioni 22 hadi 25.

“Akaunti zangu zote jumla yake haizidi shilingi milioni ishirini na tano…basi kama shilingi milioni ishirini na tano ni utajiri, basi nami nimo,” alisema Pinda na kusababisha wahariri hao waangue kicheko.

Lakini kubwa Pinda alisema kwamba kwa jinsi serikali inavyowajali watu wanaoshika wadhifa kama wake, haoni ni kwa nini awe na tamaa ya fedha na mali, kwa sababu serikali inamjali kwa kumtunza kwa kila kitu.

“Kwa utaratibu wa serikali, unapewa nyumba, magari, unalishwa na serikali…kwa mshahara wake unaweka akiba ya

kutosha, unataka utajiri wa nini? Maisha yako ni mazuri, unataka nini zaidi ya hapo? Ukitoka nje ya utumishi wa serikali, akiba yako inakusaidia kusomesha watoto wako,” alifafanua Waziri Mkuu.

Alisema hana sababu ya kuwa na tamaa na jukumu lake kubwa aliloomba kwa Mwenyezi Mungu ni kumpa uwezo wa kuwatumikia Watanzania vizuri zaidi.

“Sina hisa popote, labda huko mbele ya safari nitafikiria. Yaani ukiwa Waziri Mkuu ndio mwanya wa kujinufaisha, kwa nini? Labda mimi watu wanaweza kusema Waziri Mkuu wa sasa ni mjinga,” aliongeza Pinda.

Akizungumzia utendaji wa serikali yake, kiongozi huyo mkuu wa shughuli za serikali, alisema anaridhika na utendaji huo kwa yale yote yanayokubaliwa katika Baraza la Mawaziri yanatekelezwa ipasavyo.

“Naridhika kwamba yale yote tunayokubaliana katika Baraza la Mawaziri yanatekelezwa ipasavyo, kwa pamoja. Tunakwenda vizuri, si mbaya. Lakini kama watu wanasema kuhusu utendaji wetu, ni mzuri, watuhukumu vizuri,” alisema.

Pinda amesema, Rais aliyemteua ndiye atakayeamua kama amteue tena baada ya Uchaguzi Mkuu.

No comments: