Monday, January 11, 2010

Wasichana 6,000 wanaacha shule kila mwaka

WASTANI wa wanafunzi wa kike 5,720 nchini wanaacha shule kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ujauzito.

Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinaonesha kuwa, tangu mwaka 2004 hadi 2008, wanafunzi wa kike 28,600 wameshindwa kuendelea na masomo huku sababu nyinginezo ikiwa ni utoro na vifo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Selestine Gesimba, amesema, kati ya idadi hiyo ya walioshindwa kuendelea na masomo, 17,000 ni wanafunzi wa shule za msingi na 11,600 ni wa sekondari.

Tatizo kubwa linalotajwa kuchangia wanafunzi hao wa kike kutomaliza masomo, linadaiwa kuwa ni utoro.

Kwa upande wa mimba, Gesimba, amesema, takwimu zinaonesha idadi ya wanafunzi walioacha shule kutokana na mimba haizidi wastani wa asilimia saba kwa mwaka.

Amesema, takwimu za mwaka 2007 zinaonesha Mkoa wa Mtwara unaongoza kwa kuwa na wanafunzi 435 walioacha shule kutokana na ujauzito.

Mikoa inayofuatia na idadi ya wanafunzi waliopata ujauzito katika mabano ni Mwanza (308), Tanga (290), Pwani (280), Rukwa (265), Ruvuma (204), Lindi (144), Shinyanga (137), Dodoma (111) na Mbeya wanafunzi 105.

Kwa mujibu wa toleo jipya la Sera ya Elimu na Mafunzo 2009, waliopata ujauzito katika ngazi ya elimu ya msingi mwaka 2007 ni asilimia 0.3 na upande wa sekondari ya kawaida ni asilimia 0.6.

Gesimba alisema miongoni mwa njia za kukabili mimba kwa wanafunzi ni pamoja na kujenga hosteli kwa watoto wa kike.

Kuhusu utoro, mtendaji huyo alitaja kuwa unachangiwa na ukosefu wa lishe shuleni hususan kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Ingawa Gesemba alisema wizara haijafanya utafiti unaojitegemea kubaini hali halisi ya wanafunzi kuozwa kabla ya kumaliza masomo, hilo pia ni tatizo ambalo limekuwa likiyakumba hususan maeneo ya vijijini.

“Bado hatujawa na utafiti wa kubaini kiwango cha ndoa za utotoni kinavyochangia tatizo.

Haya mambo mara nyingi yanafanyika kwa kificho, inategemea na uzalendo wa watu ambao huamua kufichua kwamba mtoto fulani kaachishwa shule kwa ajili ya kwenda kuolewa,” alisema Naibu Katibu Mkuu, Gesimba.

Tathmini ya miaka minane ya ripoti ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) ya mwaka 2000 hadi 2008, imeainisha kuwa mimba na ndoa za utotoni ni matatizo yanayoendelea kuchangia watoto wa kike kutomaliza masomo vijijini na mijini.

Kuendelea kuwepo wanafunzi wanaoacha masomo kutokana na sababu mbalimbali, kunaipa serikali changamoto kubwa ikizingatiwa wafadhili wa elimu wamekuwa wakifuatilia kwa karibu kwa kuhimiza usawa wa kijinsia katika elimu.

Serikali ya Uholanzi ni miongoni mwa nchi wafadhili ambazo Balozi wake, Ad Akoekkoek alikaririwa hivi karibuni na moja ya tovuti akihimiza umuhimu wa kuimarisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake katika elimu nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa MDGs. Hata hivyo, serikali imekuwa katika mikakati ya kuwezesha elimu kwa wasichana.

Tathmini ya ripoti ya MDGs inaonesha kwamba serikali imedhamiria kuhakikisha ifikapo mwaka 2015, hakuna mwanafunzi wa shule ya msingi anayekatiza masomo.

Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2009 pia inaainisha umuhimu wa kuwepo marekebisho ili kufikia usawa wa kijinsia katika ngazi zote za elimu na mafunzo ikizingatiwa kwamba ushiriki wa wasichana ngazi ya elimu ya sekondari kwenda ngazi ya juu ni mdogo ikilinganisha na wavulana.

Sera inaelekeza kuweka utaratibu wa kuwabaini na kuchukua hatua dhidi ya watu watakaosababisha wanafunzi wa kike kukatisha masomo yao kwa sababu yoyote ile; iwe utoro, kufanyishwa kazi ngumu na ujauzito.

No comments: