Tuesday, March 3, 2009

Dowans yatesa Bunge


-Kisa ni kununua au kutonunua mitambo yake
-Tanesco: Mgao miezi minne ijayo

KUNA mvutano wa kimyakimya baina ya Kamati mbili za Kudumu za Bunge kuhusiana na ununuzi wa mitambo ya kufua umeme ya Dowans kama ilivyopendekezwa na Shirika la Umeme (Tanesco) ambalo linadai kwamba kama hatua hazitachukuliwa mapema, nchi itaingia katika mgao wa umeme miezi minne kuanzia sasa, Raia Mwema imefahamishwa.

Sambamba na hatari hiyo ya mgao na Kamati za Bunge kujichanganya, kuna maoni miongoni mwa umma kwamba Bunge limekuwa likiingilia sana masuala ya utendaji wa Serikali kiasi kwamba sasa inaonekana kama Bunge “linapaa na kuvuka mpaka wake huku Serikali ikirudisha nyuma majeshi yake katika masuala ya utendaji”.

Kamati zinazolumbana ni za mashirika ya umma inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto na ya Nishati na Madini iliyo chini ya Mbunge wa Bumbuli, William Shellukindo.

Katika taarifa yake kuhusu hali ya umeme katika Gridi ya Taifa, TANESCO inapendekeza kuwa mtambo wa Dowans ununuliwe pamoja na vifaa vyote vya kuunganisha kwenye Gridi ya Taifa kwa Dola za Marekani milioni 60 (zaidi ya Sh bilioni 60).

Sababu za TANESCO kusisitiza ununuzi huo kunatajwa kuzingatia vigezo mbalimbali ambavyo ni pamoja na unafuu, ikielezwa kuwa kama utanunuliwa mtambo mpya gharama zake zitakuwa juu mno.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, Kama Serikali itanunua mtambo mpya gharama ya mtambo pamoja na watalaamu wake inatajwa kuweza kufikia Dola za Marekani milioni 87 hadi 90 (zaidi ya Sh bilioni 87). Pia inaelezwa kuwa kutokana na TANESCO kuidai Dowans wastani wa Dola za Marekani milioni nane (zaidi ya Sh bilioni 8), deni hilo litakatwa katika fedha itakazolipwa Dowans wakati wa mchakato wa ununuzi.

Lakini jambo jingine kubwa zaidi katika mchakato huo wa ununuzi wa mitambo ya Dowans ni kwamba TANESCO imeanza kuiona Sheria ya Manunuzi ya Umma ni kikwazo ikiweka bayana kuwa suala la kununua mitambo iliyotumika katika sheria hiyo iangaliwe upya kwa makini na kwa manufaa ya sekta ya umeme nchini.

Baadhi ya watalaamu wa TANESCO wanasema licha ya mitambo hiyo kuwahi kutumika ukaguzi uliofanywa na kampuni ya kigeni ya TransCanada Turbines Uk Ltd, unabainisha kuwa mashine (mitambo) zote nne za Dowans ziko kwenye hali nzuri.

“Kwa ujumla hali ya mashine hizo ni nzuri kwa uzalishaji zaidi, mpaka sasa (Mei/2008) mashine LM6000PD haijafanyiwa uchunguzi kwa vile imefungwa karibuni ikiwa imeanza uzalishaji rasmi Oktoba 2007 ikiwa mpya kabisa.

“Kampuni ya Dowans walitoa orodha ya vipuri mbalimbali na kuonekana kuwa baadhi ya mashine ziliko kwenye tela, zilikuwa na vipuri zaidi kuliko mashine za LM6000PD. Mshauri wa kitalaamu alivikagua vipuri hivyo na kuridhika navyo,” inaeleza sehemu ya maelezo ya TANESCO katika kutetea ununuzi wa mitambo ya Dowans.

Lakini wakati TANESCO ikiwa na msimamo huo, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini inaamini kuwa ni kinyume cha Sheria ya Ununuzi wa Umma kununua mitambo hiyo ambayo kwa mujibu wa kamati ni chakavu.

Msimamo wa Kamati hiyo ya Shellukindo unatofautiana na wa Kamati ya Zitto ambayo inaunga mkono ununuzi wa mitambo hiyo kiasi cha kufikia hatua ya Zitto mwenyewe wiki iliyopita kumwandikia barua Spika wa Bunge, Samuel Sitta, akimuomba kuzikutanisha kamati hizo.

Zitto anataka Kamati hizo zikutanishwe ili kuwasilikiza watalaamu husika na kisha kujadili suala hilo na hatimaye kufikia uamuzi. Katika kikao hicho Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja anapendekezwa kuwapo, pamoja na uongozi wa TANESCO na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA). Kikao hicho kimependekezwa kufanyika Fabruari 28, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Taarifa zinasema hoja ya Kamati ya Zitto ya kutaka kikao cha pande husika katika suala hilo inatokana na sababu nyingi ikiwamo kwamba inawezekana Kamati ya Shellukimdo haikupata wasaa muafaka wa kusikiliza hoja za Tanesco kuhusu haja ya ununuzi wa mitambo hiyo ya Dowans.

“Kuna uwezekano mkubwa wa kuingia katika mgao wa umeme wenye madhara makubwa kama Serikali na Bunge vikiendelea kushikilia msimamo wa kutonunua mitambo ya Dowans au mingine kutoka nje haraka,” anasema mmoja wa wanasiasa waliozungumzia suala hili katika mahojiano mbalimbali na Raia Mwema wiki hii akiongeza:

“Kamati (ya Zitto) inasema kama hatua za kununua mitambo hiyo hazitafanyika kuna uwezekano wa kampuni binafsi kujitokeza kuinunua na kisha kuwauzia Tanesco ambayo italazimika kuwa inalipa capacity charge ambayo ni ghali”.

1 comment:

Anonymous said...

tumesikia giza linakuja nchini acha tulisubiri nadhani itakuwa vizuri zaidi.