Friday, March 27, 2009

Shehena kubwa ya almasi yazuiwa



-Ni ya mgodi wa Williamson, Shinyanga
-Kisa ni hali tete ya kuuzwa kwa mgodi

SHEHENA ya almasi inayotajwa kuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 4.5 (zaidi ya Sh bilioni 4.5) iliyopo katika Mgodi wa Almasi wa Wiliamson, uliopo eneo la Maganzo, mkoani Shinyanga, imezuiwa kuuzwa.

Hatua ya kuzuiwa kwa shehena hiyo kuuzwa inatokana na hali tete iliyopo baada ya kuuzwa kwa mgodi huo uliokuwa chini ya kampuni ya kimataifa ya Willcroft, iliyokuwa na ubia na Serikali, kupitia kampuni yake ya De Beers.

Kamishna wa Madini nchini, Dk. Peter Kafumu, amethibitisha kuhusu kuzuiwa kwa kwa shehena hiyo ya almasi na kusema kwamba uamuzi huo umetokana na mchakato wa kuhamisha umiliki wa mgodi huo baada ya shughuli za kampuni ya Wilcroft kupitia De Beers kuuzwa kwa kampuni ya Petra Diamonds.

Alisema kutokana na hatua hiyo, Serikali imezuia kwa muda uuzwaji wa almasi katika mgodi huo ili kupisha mchakato mpya wa maelewano baada ya shughuli za mgodi huo kuuzwa.

Dk. Kafumu pia alikiri kuzuiwa kwa karati 45,000 za almasi zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 4.5. Thamani hiyo imetokana na bei ya soko kuwa dola za Marekani milioni 100 kwa kila karati moja.

“Kinachofanyika sasa ni kuendelea kwa mchakato wa maelewano baada ya mabadiliko ya mbia kati ya Serikali na mwekezaji. Kama unavyojua serikali ina hisa asilimia 25 na mbia asilimia 75,” anasema Dk. Kafumu.

Katika uendeshaji wa mgodi huo, Serikali ilikuwa na hisa asilimia 25 wakati kampuni hiyo kwa kutumia kampuni ya De Beers, ikiwa na hisa asilimia 75.

Kwa sasa shughuli za mgodi huo zimeuzwa kwa kampuni ya Petra Diamonds kutoka Willcroft, kwa dola za Marekani milioni 10, katika uuzaji ambao unatajwa kutoipatia nchi mapato yaliyostahili, yakiwamo ya ushuru (Stamp Duty).

“Kimsingi migodi yote iliyofanya mabadiliko (kuuziana), Serikali imekuwa haipati fedha yoyote, kumbuka mgodi wa North Mara wa kampuni ya Placer Dome ya Canada kutoka kwa kampuni ya Afrika Mashariki ya Australia, na baadaye mgodi huo kuwa mikononi mwa Barrick ya Canada,” kinaeleza chanzo chetu cha habari.

Inaelezwa kuwa katika mgodi wa Williamson, licha ya Serikali kuwa na hisa asilimia 25, tangu mwaka 1994, imekuwa haina mwakilishi wake kwa upande wa uendeshaji hadi Mei, mwaka jana, na badala yake uwakilishi wa Serikali ulikuwa katika ngazi ya bodi ya wakurugenzi tu.

Habari zaidi zinaeleza kuwa katika kipindi hicho mgodi huo kupitia De Beers, umekuwa ukikopa fedha zilizofikia Dola za Marekani milioni 100 (zaidi ya sh bilioni 100), na kubwa zaidi imekuwa ikikopa fedha hizo kutoka kampuni ya Willcroft, ambayo ndiyo mama wa De Beers.

Mkopo umekuwa ukichukuliwa kwa awamu kwa madai kuwa mgodi umekuwa ukijiendesha kwa hasara, jambo ambalo ni vigumu kwa Serikali kuthibitisha kutokana na kutokuwa na mwakilishi wake katika uendeshaji.

“Kwa miaka kadhaa, De Beers wamekuwa wakidai kujiendesha kwa hasara, lakini wamekuwa wakiendelea kukopa. Mkopo sasa umefikia Dola za Marekani milioni 100. Inashangaza kuendelea kukopa huku ukilalamika kupata hasara.

“Mbali na De Beers kukopa kutoka katika kampuni yake mama ya Willcroft, pia iliweka masharti kwamba ni lazima almasi yote iuzwe katika kampuni yake nyingine ya DTC, hali ambayo watalaamu wanamini ni kuweka ukiritimba usio wa lazima.

“Kwa hiyo, De Beers ilikuwa ikieleza kuwa inapata hasara lakini ilikuwa ikikopa kutoka katika kampuni yake mama ya Willcroft lakini pia ilikuwa ikilazimisha almasi ziuzwe katika kampuni yake nyingine ya DTC. Wakati wote huu tangu mwaka 1994 hadi mwaka jana, Serikali haikuwa na mwakilishi katika shughuli za uendeshaji,” kinadokeza chanzo chetu cha habari.

1 comment:

Anonymous said...

madini yetu yamekuwa yakiibiwa kwa muda mrefu -utafikiri wenyewe hatupo? serikali nayo -sijui kwa maslahi ya nani? imekuwa ikumbatia sheria, mikataba na taratibu mbovu katika sekta ya madini na wananchi- kwa sababu ya kuaminishwa kuwa ni wanyonge!- wameshindwa kufanya hatua za wazi katika jambo hili, labda siku za usoni raia weengi watakapoamka wanaweza kuchukua hatua juu ya hili..