Friday, March 27, 2009

Mkanganyiko Kura za Albino Mwanza

ZOEZI la kupiga kura za maoni kuwabaini watu wanaojihusisha na mauaji ya walemavu wa ngozi (albino) na vikongwe lililofanyika Machi 10 mwaka huu, kwa mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, huenda lisisaidie katika kudhibiti mauaji hayo.

Hali hiyo inatokana na mwitiko mdogo wa wananchi hasa maeneo ya mijini ambako kuna vituo ambavyo havikupata kabisa wapiga kura. Zoezi hilo ambalo lilianza saa mbili asubuhi mpaka saa 12 jioni lilipangwa kufanyika siku moja lakini kama wananchi wangejitokeza kwa wingi, lingeendelea siku inayofuata.

Hata hivyo, vituo vingi vilikamilisha zoezi hilo na kufungwa hata kabla ya muda huo kufika. Kudorora kwa zoezi hilo hususan maeneo ya mijini, kulifanya uzinduzi wake uliokuwa ufanywe na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk. James Msekela uchelewe kutokana na watu wachache kujitokeza katika kituo cha Shule ya Msingi Mwenge.

Dk. Msekela anakiri kwamba watu katika maeneo ya mijini walijotokeza wachache lakini vijijini, hasa kwenye maeneo ambayo kuna mauaji ya maalbino na vikongwe, watu wengi walijitokeza.

“Ni kweli turnout hasa maeneo ya mijini haikuwa nzuri labda ni kwa vile hata mauaji ya vikongwe na maalbino pia ni kidogo. Sana sana watakuwa wanapigia kura majambazi na madawa ya kulevya. Lakini kule vijijini watu walikuwa wengi. Kuna mahali waliishiwa mpaka karatasi za kura ikabidi tuwaongeze”,” alisema Dk. Msekela.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa anasema kuwa tathmini ya zoezi hilo bado inaendelea kufanyika kwa kila wilaya na kwamba baada ya tathmini hiyo kukamilika ndipo itajulikana kama zoezi limefanikiwa au la.

“Tulipeana siku saba za tathmini ambazo ziliisha Jumanne iliyopita lakini zoezi hilo ni kubwa kidogo hivyo huenda wakaendelea. Unajua upigaji kura ulikuwa wa hiari hivyo kila mtu alikuwa na uhuru wa kwenda kupiga au kutokwenda”, aliongeza.

Mkoa wa Mwanza ambao unaongoza kwa mauaji ya vikongwe na albino, ulitarajia kuwa asilimia 40 ya wakazi wake watapiga kura hiyo.

Wananchi walitakiwa kupiga kura za siri katika maeneo manne ambayo ni mauaji ya albino, vikongwe, madawa ya kulevya pamoja ujambazi. Kutojitokeza huko kwa wananchi kunatokana na uhamaishaji mdogo uliofanyika na uoga wa baadhi ya watu.

Kabla ya kufanyika kwa zoezi hilo hapakuwapo na kampeni ya kutosha kuhamasisha wananchi pamoja na kuwaelimisha juu ya zoezi hilo .

Ofisa mmoja wa Serikali ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa wananchi wengi walikuwa hajui kuhusu zoezi hilo na hata wale wachache waliojua, walifahamu kupitia vyombo vya habari.

“Hapakuwa na maandalizi ya kutosha ukilinganisha na unyeti wa zoezi lenyewe. Ukitaka mwananchi akupe taarifa nyeti kama hizi lazima umwandae kwa kumwelimisha na kumhamasisha vya kutosha, jambo ambalo halikufanyika zaidi ya kuwatumia viongozi wa serikali za mitaa,” alisema ofisa huyo.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanaona kuwa zoezi hilo huenda lisisaidie sana katika kudhibiti mauaji ya albino na vikongwe ambayo yameshamiri katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Hata kama ukitaja fulani anahusika ni vigumu kumchukulia hatua za kisheria. Pia zinaweza kuwa zimepigwa kura za chuki au labda watu kadhaa wanamhisi fulani kuwa ni jambazi lakini wanampigia kura kuwa ni muaji wa maalbino au vikongwe,” anasema John Shija.

Anaongeza kuwa Serikali lazima iwe makini, vinginevyo itakuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu iwapo watamchukulia mtu hatua za kisheria kwa kupigiwa kura hizo za maoni.

Mwanasheria mmoja wa Serikali ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kuwa ni vigumu kumfungulia mtu mashitaka kutokana na kupigiwa kura za maoni na wananchi.

“Kisheria ni vigumu kupata ushahidi wa kuithibitishia Mahakama (beyond reasonable doubt) kwa kutumia tu kura za maoni, tena za siri. Hivi hao mashahidi watatoka wapi wakati hizo kura ni za siri?, alihoji.

Kauli hiyo ya mwanasheria inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama cha Maalbino Mkoa wa Mwanza, Alfred Kapole, ambaye amewahi kukaririwa kuwa pamoja na kuunga mkono kura hiyo ya maoni hadhani kama itasaidia kuwakamata wahusika wa mauaji hayo na kuwachukulia hatua za kisheria.

Alihoji Kapole: “Iwapo watu wamekamatwa wakiwa na viungo vya albino (ushahidi wa kutosha) lakini hadi leo hatujawahi kusikia mtu kafungwa itakuaje kwa aliyepigiwa kura tu?”.

Baadhi ya wananchi pia wanaona kama kufanyika kwa zoezi hilo ni kielelezo cha vyombo vya usalama nchini kushindwa kufanya kazi yake.

Lakini ofisa mmoja wa polisi amesema kuwa taarifa hizo ni muhimu kiitelijensia na kwamba zitasaidia katika mapambano dhidi ya mauaji ya maalbino, vikongwe pamoja na uhalifu mwingine.

“Kwetu sisi (vyombo vya usalama) hizi taarifa za wananchi ni muhimu na zitatusaidia sana . Unajua bila taarifa ni vigumu kupambana na uhalifu wowote na wenye hizi taarifa ni wananchi wenyewe ndiyo maana tunahimiza ulinzi shirikishi au polisi jamii,” alisema.

Hata hivyo tayari Chama cha Maalbino nchini (TAS) kwa kushirikiana na Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu, na Shirika la Under-the Same Sun, wamefungua kesi dhidi ya Serikali wakidai imeshindwa kulinda maisha yao .

Katika shauri hilo la kikatiba, mashirika hayo, yanatumia ibara ya 12, 14, 18(2),na 29(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinazotamka haki ya kuishi, kutambuliwa, kuheshimiwa, kupata na kutoa habari pamoja na kulindwa kisheria.

Wakili wa LHRC Clarence Kipobota, anasema wanamlalamikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara Afya na Ustawi wa Jamii na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwa kukiuka haki za binadamu.

Kesi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inahusu kushindwa kutoa taarifa rasmi kwa walalamikaji na kwa umma, kuhusu mwenendo wa mauaji ya maalbino.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, inalalamikiwa kwa kushindwa kulinda heshima na maisha ya walemavu hao wa ngozi.

Wakili huyo anaongeza kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inalalamikiwa kwa kutopatikana kwa kinga ya ngozi za maalbino katika vituo vyake vya afya, ambayo ingewasaidia dhidi ya kansa ya ngozi.

Aidha, Kipobota anasema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inalalamikiwa kwa kushindwa kuweka mikakati madhubuti kwa ajili ya maalbino, kuwawezesha kupata elimu kwa urahisi.

Kutokana na malalamiko hayo, na kwa mujibu wa wakili Kipobota wanaiomba Mahakama itoe tamko kwa Serikali kukubali kushindwa kuwalinda na kuwaheshimu, kutoa taarifa kwa walalamikaji na kwa umma kuhusu mwenendo wa mauaji ya maalbino, na kuitaka kutoa tamko la kuwafidia walioathiriwa na mauaji hayo.

Mengine ni kutoa tamko la kupatikana kwa kinga ya ngozi za maalbino katika vituo vya afya, kukubali kutunga sheria zitakazowawezesha wao, na wengine wenye ulemavu kufurahia haki zao za kikatiba.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alizindua upigaji kura za siri, kuwabaini wanaojihusisha na mauaji ya hayo, ili wachukuliwe hatua za kisheria. Kura hizo zinapigwa kikanda.

1 comment:

Anonymous said...

mi sidahani kama njia hii ni nzuri kufichua wauaji wa albino, nahisi kama jamii inatakiwa kufanya zaidi ya kupiga kura katika kudhibiti mauaji ya albino nchini.