ZOEZI la upigaji kura ili ‘kuwachagua’ wanaoshukiwa kuhusika na vitendo vya mauaji ya albino lilizinduliwa kwa ving’ora kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, wiki iliyopita. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ndiye alikuwa mgeni wa heshima aliyeliza king’ora katika uzinduzi huo.
Kwa kawaida katika shughuli zinazohusu upigaji kura, tulitegemea kumuona mgeni wa heshima akitumbukiza kura yake kwenye sanduku la kupigia kura kama ishara ya ufunguzi wa zoezi hilo, lakini badala yake tukaonyeshwa akibonyeza kitufe cha king’ora.
Naamini ingeleta uzito zaidi iwapo mgeni wetu wa heshima angeonyeshwa akitumbukiza kura yake kwenye sanduku hata kama kura yenyewe ingekuwa haijaandikwa kitu kuashiria kuwa hamfahamu yoyote anayeshukiwa kuhusika na biashara hiyo haramu!
Nimejiuliza pia juu ya uamuzi wa kufanyia uzinduzi wa zoezi la kupiga kura jijini Dar es Salaam badala ya mji wowote wa Kanda ya Ziwa ambako mauaji ya maalbino yamekithiri kwa kiwango cha kutisha. Ni uamuzi ambao pengine ungeongeza hamasa ya wananchi wa maeneo hayo yaliyokithiri kwa vitendo hivyo kushiriki kikamilifu zoezi hilo.
Hilo pembeni, tumeambiwa kwamba kura hiyo ambayo ina vipengele vinne itasaidia kubainisha wale wote wanaohusika na uovu wa kuua albino kwa ajili ya viungo vyao. Vipengele vingine vya kura hiyo ni pamoja na kuwataja wanaoua vikongwe, majambazi na pia wauzaji madawa ya kulevya.
Pengine hapa tunapaswa kujiuliza kama kweli tupo serious na tatizo hili. Kwa nini kura ya maoni ya kuwatambua wanaohusika na mauaji ya ndugu zetu maalibino na wazee wetu ichanganywe na kura ya kuwatambua majambazi na wauza dawa za kulevya ambao majina yao tayari yapo mpaka ofisi ya juu kabisa ya nchi na hayajafanyiwa kazi?
Tunatoa picha gani hapa kwa ndugu zetu maalbino? Kwamba mwisho wa siku orodha ya watakaotajwa kuhusika na kuwaua haitashughulikiwa kama ambavyo hazijashughulikiwa orodha za majambazi na wauza madawa ya kulevya ambazo zimefungiwa kwenye makabati na watuhumiwa kupewa muda wa kujirekebisha?
Kwa hakika, kipengele cha kuwataja wauza madawa ya kulevya kitaongeza tu idadi ya watuhumiwa ambao tayari wako kwenye orodha mbali mbali ambazo viongozi wetu wamekaririwa mara kadhaa wakisema kuwa wanazo.
Sio vibaya iwapo wakati watu wanapiga kura kuongeza idadi hiyo, viongozi wetu nao wakaanza kuipunguza kwa kushughulikia yale majina yaliyomo tayari kwenye orodha ambazo wao wenyewe wamekiri mara kadhaa kuwa wanazo!
Hilo ni moja, lakini pia nimejiuliza sana iwapo kuna Juhudi zozote zimefanyika ili kuhakikisha kuwa wananchi wetu wamepata elimu ya kutosha kuhusiana na zoezi hili kabla halijazinduliwa rasmi.
Tukumbuke kwamba wengi wa wananchi wetu tunaotegemea wapige kura kuwataja wanaohusika na mauaji ya albino, ndio hao hao ambao hupata tabu hata wakati wa kupiga kura muhimu zaidi ya kuchagua viongozi wao.
Je, wananchi wetu hawa wamepata elimu na muda wa kutosha wa kujiandaa na zoezi hili ambalo kwa hakika, kwa namna moja ama nyingine, limekuja kwa namna ya ‘ghafla bin vuu’?
Sio nia yangu kubeza juhudi zinazofanywa ili kuhakikisha kuwa ndugu zetu maalibino wanaishi kwa amani kwenye nchi yao wenyewe kama ilivyo kwa raia wengine, lakini ni lazima niseme wazi kuwa nina wasiwasi sana kama zoezi hili litaleta matokeo yanayotarajiwa.
Kuna maswali kadhaa ya kawaida kabisa ambayo yanataka majibu. Je, kwa kututaka wananchi tupige kura ya maoni ‘kuchagua’ wale tunaodhani kuwa wanahusika na ushenzi huu, ndio kusema kuwa vyombo vyetu vya usalama vimeshindwa kuwaona na kwa maana hiyo kutaka msaada kutoka kwa wananchi?
Je, zoezi hili likijumlishwa na ile kauli ya ‘jino kwa jino’ iliyopata kutolewa na Pinda ya kutaka wanaoua ndugu zetu maalibino nao wauawe, ichukuliwe kama ushahidi kwamba vyombo vyetu vya usalama vimeshindwa kazi na hivyo kuurudisha kwetu mzigo wa kuwatafuta wahalifu hawa wanaowaua maalbino?
Kama tunakubaliana kwamba kila mwananchi wetu ni mlinzi wa nchi yetu na anawajibika kutoa taarifa kuhusu uhalifu wowote, ni kitu gani kinachowafanya wananchi wetu wasifanye hivyo kwa hiyari yao wenyewe mpaka tuzindue zoezi la kupiga kura ya maoni kuwataja watuhumiwa ambao wanawafahamu siku nyingi? Tatizo ni nini?
Je, zoezi hili na kauli ya Pinda ni ushahidi kwamba viongozi wetu sasa hawajui cha kufanya kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili, na matokeo yake kuwa haya ya kuwa wafa maji wanaokumbatia hata nyasi katika juhudi zao za kujiokoa wasizame?
Kwa utaratibu huu wa kupiga kura za maoni ili kuwapata wanaohusika na mauaji ya albino, je huko mbele ya safari tutegemee rundo la mazoezi ya kupiga kura za maoni kubaini wezi wa mitihani ya taifa, makampuni ya mabasi yanayoongoza kwa kusababisha ajali, viongozi wenye shahada feki na kadhalika!?
Niko tayari kukosolewa, lakini nina uhakika kwamba hakuna sheria ya nchi inayosema kuwa kuna mhalifu anaweza kutiwa hatiani kutokana na ‘kuchaguliwa’ na kura za maoni za wananchi wenzake.
Hii ina maana kwamba baada ya kupiga kura majina yatakayopatikana yatarudishwa tena kwenye vyombo vyetu vya usalama ambavyo vitalazimika kufanya tena uchunguzi dhidi ya watuhumiwa hao ili kupata ushahidi unaotosha kuwasimamisha kizimbani!
Mwisho wa yote tunajikuta tumerudi tena kule kule. Ni vyombo vyetu hivi hivi vya usalama ambavyo hadi leo hii vimeshindwa kungurumisha angalau kesi moja tu ya wahalifu wanaoshukiwa kuhusika na mauaji ya albino, halafu leo tunatakiwa kupiga kura ili kuwaongezea mzigo mwingine wa majina ya mabazazi tunaowashuku!
Nakubaliana na kauli ya Mkurugenzi wa Shirikisho la Vyama vya Wenye Ulemavu Tanzania (SHIJAWATA), Christopher Andelekisye aliyotoa siku ya uzinduzi wa zoezi la kupiga kura za kuwatambua wanaohusika na mauaji ya maalibino.
Mkurugenzi huyu alionekana kutofautiana na Waziri Mkuu kwa kusema kuwa zoezi hilo halitakuwa na tija iwapo mwenendo wa kesi za wauaji wa maalbino hautabadilishwa.
Mkurugenzi huyo alishauri kuwepo kwa marekebisho ya sheria ya uchawi na ile ya adhabu (penal code). Sheria iliyopo na ambayo tumerithi kutoka kwa wakoloni inapinga kuwepo kwa uchawi.
Ni kweli kwamba mpaka sasa hakuna sheria tofauti kwa ajili ya kesi zinazohusu mauaji ya albino. Zinaendeshwa kama zinavyoendeshwa kesi za mauaji ya mtu mwingine yoyote.
Labda tungeazia hapo; kwamba Bunge na asasi za serikali zinazohusika zitunge na kupitisha sheria maalumu kwa ajili ya kushughulikia kesi zinazohusu mauaji ya albino, ikiwezekana hata kuanzisha vitengo maalumu kwenye mahakama na ofisi za waendesha mashitaka wa serikali kwa ajili ya hilo.
Lakini wakati tukisubiri hilo, tunaweza kuamua kuwa kesi yoyote inayohusu mauaji ya albino ni priority. Aidha, yanapotokea mauaji hayo, polisi wa eneo husika waruhusiwe kuweka pembeni uchunguzi wa mauaji mengine yoyote waliokuwa wakiendelea nayo ili kushughulikia yale ya albino.
Kwa hatua hizi, tunaweza tukafika mahali tukagundua ni nani anayesababisha kesi za mauji ya albino kusuasua na tukamchukulia hatua zinazostahili, mbali ya kwamba tutafika mahali tukajikuta hatulazimiki kupoteza muda kupiga kura ya ‘kuwachagua’ watuhumiwa wa mauaji ya ndugu zetu.
No comments:
Post a Comment