Tuesday, March 24, 2009

Mkutano wa IMF-Afrika: Rais Kikwete utatanishi mtupu


KWANZA nawaomba radhi wapenzi wasomaji wa safu hii kwa kutokuandika kwa muda mrefu kwa sababu ya kutingwa na majukumu binafsi.

Wiki iliyopita, Rais Kikwete alikuwa mwenyeji wa mkutano wa IMF-Afrika, uliohudhuriwa na Rais wa Shirika la Fedha Duniani, Dominique Strauss-Kahn, mawaziri wa fedha wa nchi za Afrika, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia na sekta binafsi.

Mkutano huo, pamoja na mambo mengine, ulijadili mikakati ya kukinga uchumi wa nchi za Afrika dhidi ya mgogoro wa kifedha uliosababishwa na mtikisiko wa uchumi duniani.

Mshiriki Jeffrey Sachs alitoa kauli kwamba utawala wa Washington katika uchumi wa dunia (Washington consensus), umefika kikomo. Mwandishi wa CNN, Isha Sesay aliwataka washiriki walioamini kauli hiyo wanyooshe mikono. Rais Kikwete alinyoosha mkono kuashiria kwamba anakubaliana na kauli hiyo. Waziri wa fedha na uchumi, Mustafa Mkullo hakunyoosha mkono.

Ili kukabiliana na mtikisiko wa uchumi duniani, mkutano uliazimia kuwa sekta binafsi katika Afrika inahitaji fursa nzuri ya uwekezaji ili ichukuwe nafasi ya injini kubwa katika kukuza uchumi. Katika msukosuko wa namna hii wa kiuchumi duniani, Isha Sesay alitaka kujua Rais Kikwete anafanya nini ambacho ni tofauti ili kuvutia wawekezaji katika sekta binafsi?
Kwa ufupi, Rais Kikwete alijibu kuwa anaendeleza sera na mipango ileile iliyokuwapo.

Hakika mtikisiko wa uchumi duniani umewaacha viongozi wetu katika njia panda. Natatanishwa na imani ya Rais Kikwete kuwa Washington hawatatawala tena uchumi wa dunia, lakini wakati huo huo hana mipango na sera mpya zaidi ya kuendeleza zilezile zilizotungwa Washington!

Na kama sera zilizotungwa Washington ndizo zilizoutikisa uchumi wa dunia, kwa nini tuziendeleze? Je, sera zinazoutikisa uchumi imara wa Marekani, hazitauzika kabisa uchumi wetu mahututi?

Utatanishi wa namna hii umeibua maswali mengi kichwani mwangu. Je tumetoka wapi, tupo wapi sasa hivi na kwa nini? Je, Washington ni akina nani? Wametoka wapi na wapo wapi sasa hivi? Lengo langu ni kuchokoza mjadala ili tuweze kupata mwanga wa wapi tunakwenda. Katika waraka wa leo na wiki ijayo nitajadili kwa ufupi maswali yote haya.

Tangu mwaka 1967 mpaka 1992, mwongozo na dira ya Serikali ya Tanzania ilikuwa ni Azimio la Arusha. Liligawanyika katika sehemu tano, lakini zinazohusu mada hii ni tatu; Ujamaa, Kujitegemea na Maadili ya viongozi.

Chini ya Ujamaa, njia kuu za uchumi zilimilikiwa na umma. Nguzo kubwa ya uchumi ilikuwa ni wawekezaji ambao walikuwa ni umma. Makampuni na mabenki yalimilikiwa na umma chini ya uendeshaji na usimamizi wa serikali. Yalipopata faida, yalilipa kodi serikalini na salio lilikuwa la umma ambalo lilitumika, ama kukuza mtaji wa biashara katika kampuni na benki husika au katika huduma za jamii kama elimu na afya. Hasara iliyopatikana ilikuwa ni ya umma pia.

Hii ni tofauti na nchi za kibepari ambapo chanzo cha mapato serikalini ni kwa njia ya kutoza kodi tu, kwa sababu faida au hasara siyo ya umma, bali ni ya wanahisa au wamiliki binafsi wa makampuni na mabenki.

Siasa ya kujitegemea ilitahadharisha suala la mikopo, kwa hoja kwamba kuwabebesha watu masikini mikopo ambayo inawazidi kimo si kuwasaidia bali ni kuwaumiza. Kwamba “haiwezekani kutegemea nchi za nje na kampuni za nje kwa misaada, mikopo na rasilimali kwa maendeleo ya Watanzania bila kuhatarisha uhuru wa Tanzania. Haikuamini dhana ya wageni kumiliki uchumi wa Tanzania kwa ajili ya kupata faida kupeleka nchini kwao.

Maendeleo huletwa na watu hayaletwi na fedha. Fedha ni matokeo siyo msingi wa maendeleo na unyonge wa Mtanzania usingeweza kuondolewa na fedha kutoka nje bali kutoka kwa Watanzania wenyewe.

Masharti ya maendeleo yalikuwa juhudi na maarifa. Na ili kuendelea walihitajika watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora” (kitabu cha Azimio la Arusha).

Kimaadili, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa mashirika ya kiserikali, madiwani na watumishi wa serikali waliokuwa na vyeo vya kati na juu, hawakuruhusiwa kuwa na hisa katika kampuni yoyote. Hawakutakiwa kuwa na mishahara miwili au zaidi na hawakuruhusiwa kuwa wakurugenzi katika kampuni ya kikabaila au kibepari.

Ingawa ilikuwapo mipango na maazimio na mikakati ya muda mfupi kama vile; Azimio la Musoma lililohimiza umuhimu wa Watanzania wote kupata elimu, msisitizo ulilenga kukuza maarifa ya ufundi na sayansi na Azimio la Iringa la kilimo cha kufa na kupona.

Ardhi ya Tanzania ni kubwa yenye udongo wenye rutuba, hivyo kilimo kilikuwa uti wa mgongo. Mikakati ya muda mrefu iliwekwa katika ujenzi wa viwanda vya mazao ya biashara na zana za kilimo.

Mifano michache ni viwanda vya majani ya chai, kahawa, nguo, pareto, mkonge, bia, sigara, sukari na zana za kilimo. Viwanda vingine vilihusu bidhaa muhimu kama sabuni, saruji na kiwanda cha kusindika nyama cha Kawe.

Ilianzishwa benki ya taifa ya biashara (NBC) iliyokuwa na matawi mpaka vijijini. Nyingine ni Benki ya Nyumba (THB) na Posta (TPB). Pia, yalianzishwa mashirika mbalimbali ya umma kama Shirika la Ndege (ATC) na Shirika Bima la Taifa (NIC).

Misingi hii ya uchumi iliiwezesha serikali kugharamia elimu kuanzia chekechea, kisomo cha watu wazima, msingi, sekondari mpaka chuo kikuu. Wanafunzi wote walipatiwa huduma za afya, chakula, nauli, na fedha ya kujikimu. Shule zote za serikali zilikuwa na vifaa vya mahabara na nyenzo muhimu za kufundishia.

Walimu, wauguzi na madaktari walilipwa mishahara yao. Serikali iliweza kununua madawa kwa ajili ya dispensari mashuleni, vijijini na mahospitalini.

Misingi ya uchumi wa Tanzania ilianza kujaribiwa na dhoruba kutoka ndani na nje ya nchi. Mfano, Mwaka 1973 kulikuwa na ongezeko kubwa la bei ya mafuta ya petroli duniani. Gharama za uzalishaji zilipanda na thamani ya shilingi iliathiriwa.

Kuanzia 1973 mpaka mwishoni mwa 1974 ulitokea ukame uliosababisha upungufu wa chakula. Na mwaka 1977 jumuiya ya Afrika Mashariki ilivunjika na hivyo Serikali kulazimika kugharamia huduma zilizotolewa na jumuiya hiyo.

Aidha kuanzia 1978 mpaka 1979 Tanzania ilipigana vita dhidi ya majeshi ya Iddi Amin wa Uganda. Vita hiyo, kwa kiasi kikubwa, iligharamiwa na Tanzania.

Matukio haya katika ujumla wake yaliutikisa uchumi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa. Bidhaa muhimu kama sukari, unga wa ngano, mahindi, na vifaa vya ujenzi kama mabati na simenti, viliadimika. Ili kulinda wananchi wasio na uwezo, Serikali iliingilia mgao wa chakula na mafuta ya petroli kwa kutoa vibali.

Baadhi ya watendaji serikalini na wafanyabiashara wachache walitumia mpango wa vibali kulangua bidhaa na kuziuza kwa magendo. Serikali ilitangaza vita dhidi wahujumu uchumi iliyoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine (Mungu airehemu roho yake).

Kumwagia tindikali kwenye kidonda, hata uzalishaji katika viwanda ulianza kudhoofika, na ufanisi katika uendeshaji wa mashirika na mabenki ulianza kulegalega.

Viwanda, mabenki na mashirika mengi ya umma yalianza kuwa msalaba kwa serikali kwa sababu yalikuwa yanaendeshwa kwa hasara wakati yakipokea ruzuku kutoka serikalini. Hali hii ilisababishwa na mambo mengi, lakini baadhi ni uzembe, wizi na ubadhilifu wa mali ya umma. Mashirika kuendeshwa kisiasa badala ya kibiashara, kwa sababu wakurugenzi wengi walikuwa ni wanasiasa bila kuwa na ujuzi wa kuendesha shirika.

Halikadhalika utamaduni wa kuwazawadia na kuwalea vihiyo, wabadhirifu, na wazembe uliharakisha msambaratiko wa mashirika mengi. Mfano, mkurugenzi aliyevurunda shirika moja alihamishiwa shirika jingine bila kuadhibiwa.

Kuanzia katikati ya kipindi cha awamu ya pili mwaka 1985, serikali ilikuwa na uhaba mkubwa wa fedha za kujiendesha, kulipa madeni yaliyojenga baadhi ya viwanda na kutoa huduma muhimu kwa jamii.

Katika kipindi hicho, hali ya kisiasa duniani ilikuwa imebadilika. Vita baridi kati ya Urusi na Marekani, ambayo ilizitesa na kuzinufaisha baadhi ya nchi ilikwisha kumalizika. Katika vita hiyo, mabepari walitoka vifua mbele.

Kwa bahati mbaya, ni wakati huo huo, ambapo serikali ya Tanzania na nchi nyingine ambazo uchumi wake ulikuwa taabani, zilikimbilia Washington kuomba fedha kama zawadi au mikopo.

Je, huko Washington kuna akina nani? Hasa zinazoumiza kichwa ni asasi kubwa mbili za fedha. Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia (WB). Hizi asasi zilianzishwa 1944 mjini Bretton Woods, New Hampshire (Marekani) na ndiyo maana zinaitwa Bretton Woods System.

Mataifa 44 waanzilishi waliunda taasisi hizo ili waweze kupata mikopo ya muda mfupi baada ya kuathiriwa vibaya na vita kuu ya pili ya dunia.

Dhumuni la mikopo lilikuwa kuyajenga upya mataifa yao yaliyokuwa yamebomolewa na vita. Wakati huo hayakuwapo makundi ya nchi za dunia ya kwanza na nchi za dunia ya tatu au nchi masikini kama ilivyo sasa. Zilikuwapo dola kubwa ambazo zilitawala maeneo makubwa duniani.

Kwa hiyo, hizi taasisi ambazo ni kubwa kwa sasa hazikuundwa na jumuia ya kimataifa. Ziliundwa kwa maslahi ya wale waliozianzisha.

Mathalani, muundo wa Shirika la Fedha Duniani bado unayapa nguvu mataifa makubwa yenye nguvu za kiuchumi. Kura ya kila taifa inategemea na ukubwa wa uchumi wake. Marekani bado inaongoza kwa kuwa na zaidi ya asilimia 17 ya kura zote, ikifuatiwa na Japan na Ujerumani.

Kikatiba, ili kuathiri maamuzi ya IMF, kubadili muundo au sera zake, kunahitaji asilimia 80 ya kura zote. Hata hivyo, Marekani na nchi za ulaya peke yake zina zaidi ya asilimia 80 ya kura zote.

Idadi ya wanachama wa IMF imeongezeka kutoka 44 tangu ianzishwe mpaka 185 sasa hivi. Uchumi wa Afrika ni takriban asilimia mbili ya uchumi wa dunia. Kwa hiyo, pamoja na ongezeko hilo la wanachama, na kutokana na kanuni za IMF, hata mataifa yote masikini duniani yakiungananisha kura zao, hayawezi kubadilisha sera au masharti ya hili shirika. Kubadili kitu chochote ndani ya IMF lazima kwanza upate baraka za mataifa makubwa.

Je, uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania ulipotikiswa, Washington walitoa ushauri gani kwa serikali kuhusu kilimo, mashirika ya umma, mfumo wa biashara, utoaji wa huduma muhimu kwa jamii kama elimu na afya? Je ushauri huo ulikuja na dira?

Na je, uti wa mgongo wa uchumi wa nchi za Magharibi ulipotikiswa, walikimbilia IFM kwa ushauri? Je, wanatekeleza waliyoishauri serikali ya Tanzania au wameiacha kwenye mataa kwa kutenda waliyotukataza?


Mfano, mabenki, viwanda vya magari, shirika kubwa la bima la Marekani yaliposhindwa kujiendesha, serikali ilifanya nini?

Je, Rais Barrack Obama ana mipango gani kuhusu elimu, afya na sheria mpya ya maadili kwa viongozi na watumishi wa serikali?

Kwa hiyo katika mkutano huo wa IMF-Afrika uliofanyika Dar es Salaam, watawala wetu Tanzania hawakuwa na jipya. Lakini yote tisa, kumi ni kitendo cha mpigania haki za kisiasa, Bob Geldof kutoa karipio na kumkatisha Rais Kikwete wakati anazungumza. Je, Kwa nini Bob Geldof hakukanywa? Ni kwa sababu ya ugeni, rangi, au utajiri wake?

Mbona baadhi ya wazee waliostaafu wanapotoa ushauri kama huo huo tena kwa lugha ya kistaarabu, wanaambiwa kwamba wanatolea ushauri vijiweni? Je ni kwa sababu ya rangi, uenyeji, au umasikini wao? Matendo haya yanalinda heshima na utu wetu?

No comments: