Katika kuadhimisha siku hii muhimu ya harakati za kumkomboa mwanamke kimapinduzi, GDSS waliandaa big-bang ambayo ilijumuisha wanaharakati kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini, na kupambwa na vikundi vya sanaa na buradani, uimbaji wa nyimbo na ngonjera, maandamano madogo, na watoa ushuhuda. Mgeni rasmi katika sherehe hiyo alikuwa ni naibu waziri wa afya, Dr. Aisha Kigoda. Big bhang hiyo ilifanyika katika viwanja vya TGNP siku ya tarehe 4/03/2009 kuanzia saa sita mchana. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kuwahudumia wanaoishi na VVU ni jukumu letu sote sote Wanawake, Wanume na jamii kwa ujumla”
Mchangiaji wa kwanza katika tamasha hili dada Mary Rusimbi, alisema, uchaguaji wa kauli mbiu hiyo ya mwaka huu umetokana na juhudi za wanawake na wanaharakati kutaka mchango wa wanawake katika kazi za kijamii kupewa kipaumbele na kuthaminiwa, tofauti na sasa ambapo wanawake wanafanya kazi nyingi lakini hazithaminiwi. Kazi ambazo wanawake wamekuwa wakizifanya ni pamoja na kutafuta kuni na maji, kuhudumia wagonjwa na wazee, kulea watoto, kazi za kilimo, na kutunza familia kwa ujumla.
Kazi zote hizi zimeshindwa kutambulika katika mfumo wa hesabu za kiserikali na kusababisha wanawake kufanya kazi ambazo hazina malipo kwa muda mrefu. Kuanzishwa kwa mfumo wa kuwahudumia wagonjwa wa VVU majumbani kunamaanisha wanawake kuendelea kuongezewa mzigo wa kazi ambazo hazina malipo. Mfumo wa mila za jamaii yetu umekuwa ukichangia kuendeleza hali hii ya ukandamizaji wa wanawake. Pia dada Mary alieleza mchango wa mashirika ya kijamii-CSOs, ambapo aligusia juhudi zilizofanywa na kuendela kufanywa na mashirika haya katika kuifanya jamii itambue mchango huu wa wanawake. Mwaka 2005 CSOs ziliweza kuishawishi serikali kupitia National burue of statistic-NBS kufanya takwimu za matumizi ya muda kwa wanawake, wanaume, wazee, na watoto. Nia ya utafiti huu ilikuwa ni kutambua matumizi ya muda miongoni mwa wanajamii na kuifanya jamii itambue mchango wa wanawake katika kuleta maendeleo ya taifa, ambao wanachangia karibu asilimia 60 ya pato lote kupitia kazi ambazo hazina malipo.
Mchangiaji wa pili dada Neema Duma Kutoka Shirika la WOFATA-Women Fight Aids Tanzania-, yeye aligusia juu ya changamoto wanazokutana nazo katika kazi zao za utoaji wa huduma kwa wagonjwa waliopo majumbani. Ambaye pamoja na mambo mengine aligusia juu hali ya usiri kwa wagonjwa inayotokana na unyanyapaa katika jamii, na kushindwa kwa serikali za mitaa kutoa misaada/ushirikiano kwa wagonjwa ama mashirika yanayohudumia wagonjwa hao. Mchangiaji wa tatu, dada Salama kutoka Bagamoyo, yeye alitoa ushuhuda wa kuishi na VVU. Alijigundua kwamba anaishi na VVU mwaka 2000 na kuendelea kupambana navyo mpaka sasa. Alitoa wito kwa serikali na mashirika ya misaada kuongeza misaada ya chakula kwa wagonjwa, kwani wagonjwa wengi hawapati lishe bora kwa vile hawana fedha za kununulia chakula bora.
Kwa upande wake mgeni rasmi-Aisha kigoda- aliwapongeza wanawake kwa kuanza kuamka na kupigania haki zao, ambaye alisema ni tofauti na awali ambapo ilikuwa si rahisi kwa wanawake kusimama na kusema jambao lolote mbele ya hadhara, mfumo ambao ulilelewa na mila zetu. Pia alitaka wanaume nao waelimishwe ili waweze kutoa huduma kwa wagonjwa majumbani badala ya kuwaachia wanawake pekee yao. Waziri alikiri kuwepo na upungufu mkubwa wa wahudumu wa afya ambao unafikia asilimia 50, na kuahidi kuwa serikali inafanyia kazi kufidia upungufu huo. Alisema serikali imetoa mtaala ambao utasaidia kuwaongoza watoa huduma majumbani, kutolewa kwa mtaala huo ni juhudi za serikali katika kupunguza mzigo kwa watu wanatoa huduma kwa wagonjwa waliopo majumbani. Changamoto iliyopo mbele yetu alisema mgeni rasmi ni “jinsi ya kufikisha taarifa hizi kwa watu wengi zaidi na kuwafanya washiriki katika harakati hizi za kupunguza mzigo wa kazi kwa akina mama”
Baada ya mgeni rasmi kuongea, walifuata watoa ushuhuda kutoka sehemu mbalimbali nchini ambao walielezea uzoefu wao juu hali ya utoaji huduma kwa wagonjwa majumbani katika maeneo yao wakielezea changamoto wanazokumbana nazo na nini kifanyike ili kuboresha utoaji huduma katika maeneo hayo. Baada ya watoa ushuhuda ikafuatiwa na michango kutoka kwa washiriki wa tamasha hili, kabla ya muungozaji wa tamasha-dada Gema Akilimali- kuhitimisha kwa kuwashukuru wote walioshiriki.
Ukiwa kama raia/mdau unashiriki vipi katika harakati hizi? Nini mchango wako kuhakikisha mzigo wa kuwahudumia wagonjwa wa UKIMWI linakuwa ni jukumu la watu wote katika jamii?
No comments:
Post a Comment