Friday, March 27, 2009

‘Wazee wa Mbeya wana darubini za kutambua watu wanaotia mimba wanafunzi’

Darubini ni kifaa kinachotumika kutazamia vitu vilivyo mbali. Lakini kutokana na mabadiliko ya teknolojia, kifaa hicho kimekuwa kikitumika kwa shughuli mbalimbali, zikiwemo shughuli za kisayansi, kivita na hata kutazama vitu vilivyopo angani, kama vile mwezi, jua na nyota. Darubini ya kwanza inayojulikana, ilitengenezwa mwaka 1608 na Mholanzi Hans Lipperhey, aliyekuwa fundi miwani.

Mfano wake ulichukuliwa na kuboreshwa na raia wa Italia, Galileo Galilei, aliyeanza kuitumia mwaka 1610 kwa kuangalia nyota. Darubini ziliendelea kuboreshwa katika karne zilizofuata. Mtambo mpya ulipatikana katika Karne ya 20, kwa kutumia mnunurisho wa sumaku umeme kutoka nyota, iliyoendelezwa kuwa darubini redio.

Lakini, nchi za Magharibi zikiwa zimepiga hatua kubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, nchini Tanzania, hususani wilaya ya Mbeya, baadhi ya wazee wa mila kupitia kamati zao za ufundi, wanazo darubini zinazowawezesha kutambua watu wanaowapa mimba wanafunzi, wezi na wapiga nondo.

Hivi karibuni wazee wa mila wa kabila la Wasafwa, wakiwemo Machifu na Mamwene, waliitisha mkutano uliomshirikisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, uliokuwa una lengo la kujadili masuala mbalimbali, ikiwamo kudhibiti mimba za wanafunzi, mauaji ya albino na wapiga nondo, ulinzi kwa viongozi wa ngazi ya wilaya hadi Taifa na kuomba Serikali iwatambue.

Mwenyekiti wa Mila wa Wilaya ya Mbeya (Mwene Mkuu), Shao Soja Masoko, anasema wazee wa mila wanakerwa na vitendo vya wanaume kuwapa mimba wanafunzi na kisha kukana mimba hizo. Anasema hali hiyo imesababisha wasichana wengi wakatishe masomo, hivyo kuwa chanzo cha watoto hao kushindwa kupata elimu.

Anasema wazee wa mila, wana uwezo wa kukabiliana na tatizo la wanafunzi kupata mimba, kwa kuwapa adhabu wanaume wanaowapa mimba wanafunzi. Adhabu hiyo itakuwa ni fundisho kwa wanaume wote; na watakaogopa kuwagusa wanafunzi, kwa kuwa madhara ya kufanya hivyo, yatakuwa yanaeleweka.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tunachoomba serikali ya mkoa itupatie kibali cha kuwadhibiti watu wanaowapa mimba wanafunzi na kukana kuwa na uhusiano na wasichana hao, kwa kuwapa adhabu ya kuwahamishia mimba hizo katika matumbo yao na wasichana kuendelea na masomo kama kawaida,” anasema. Anasema mimba kwa wanafunzi imekuwa ni kero kubwa katika jamii.

Anasema kwamba badala ya serikali kuendelea na mikakati ya kuboresha sekta ya elimu nchini, sasa inalazimika kukabiliana na mimba kwa wanafunzi na utoro, mambo yanayopaswa kudhibitiwa na wananchi wenyewe katika maeneo wanayoishi. Anaomba serikali iwape kibali cha kudhibiti mimba, kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

"Machifu na Mamwene tuna darubini zetu, tuna uwezo wa kuona mbali. Ukitupa kibali tunaweza kuwadhibiti wanaowapa mimba wanafunzi, kwa kuzihamishia mimba hizo kwao na mwanafunzi kuendelea na masomo salama salimini, huku akiwa si mjamzito tena," anasema na kuongeza kuwa hilo litakuwa fundisho kwa wengine.

Chifu Roketi Mwashinga anasema wazee wa mila, wana uwezo wa kusaidia shughuli mbalimbali katika jamii, ikiwamo kudhibiti watu waovu. Hata hivyo, anasema kuwa serikali imewasahau na kuwatenga, hali inayosababisha washindwe kutoa ushirikiano, hata pale wanaposhuhudia maovu yanatendeka mbele yao.

Anasema miaka ya nyuma walikuwa wakishirikishwa, lakini hivi sasa hawashirikishwi katika mambo mbalimbali, hali inayofanya wasiheshimike katika jamii na hivyo kutopewa nafasi. "Tukishirikishwa, tunaweza kusaidiana na viongozi wa serikali, lakini kama tutaendelea kubaguliwa, basi hatutakuwa na la kufanya," anasema. Wanaiomba serikali iwatambue na kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali.

Anasema kutofuatiliwa kwa wahamiaji wageni katika mitaa na kudharauliwa kwa wazee wa mila, ndio chanzo cha kuongezeka kwa vitendo viovu katika jamii, ikiwamo mauaji ya albino na raia wema kushambuliwa kwa kupigwa nondo na kunyang'anywa mali walizonazo. Anasema kukithiri kwa vitendo viovu katika jamii, kunachangiwa na Serikali kutowathamini wazee wa mila na kuwashirikisha katika kudhibiti vitendo hivyo.

Anasema kupitia darubini zao, wazee wa mila wanaweza kuwadhibiti wanaofanya vitendo hivyo, kwa kuwafanya wawe vichaa au wajipeleke wenyewe katika vituo vya polisi na kujieleza. Hata hivyo, anasema tabia ya baadhi ya polisi kushindwa kutunza siri, zinazotolewa na raia wema, imekuwa ni kikwazo kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo. Anaitaka Serikali kuwadhibiti askari wasio waaminifu ili maovu yadhibitiwe katika jamii.

"Kama serikali itakuwa tayari kushirikiana na sisi, tunakuomba wewe na sisi tuongozane katika operesheni ya kukamata wapiga nondo kutoka eneo moja hadi jingine. Kwa kutumia kamati zetu za ufundi, wote watapatikana na wengine watajipeleka wao wenyewe katika vituo vya polisi, wakiwa na viungo vya binadamu na kuanza kutoa maelezo wao wenyewe bila kuhojiwa," anasema.

Akizungumzia mauaji ya albino, anasema ili vitendo hivyo vidhibitiwe, ni lazima serikali ishirikiane na waganga wa kienyeji. "Ukitaka kumkamata mwizi ni lazima umtumie mwizi mwenzake," anasema. Anaongeza kuwa waganga wa jadi, ndio wanaoweza kusaidia kukomesha mauaji ya albino.

Mwashinga anaitaka serikali, kuangalia upya utaratibu wa usajili wa waganga wa kienyeji. Anasema utafiti wao wamebaini kuwa waganga wanaohusika na mauaji hayo, wengi wanatoka nje ya mkoa wa Mbeya, sanjari na wapiga nondo. Anawataka machifu na mamwene, kuwaonya watoto wao wasijihusishe na vitendo hivyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Waganga wa Jadi Mkoa wa Mbeya, Jeiko Ngurunguru, anasema waganga wanaotuma watu wakaue albino, si waganga wa jadi, bali ni wanamazingaombwe na matapeli wanaotoka nje ya Mkoa wa Mbeya. Anasema ikiwa serikali itahakikisha kuwa waganga wasio na vibali, hawaruhusiwi kufanya shughuli za tiba asili, mauaji hayo yatadhibitiwa.

Anasema uganga ni jambo la kurithi na waganga wa kweli, wanafahamika katika jamii na historia yao inafahamika, wanafanya kazi kwa uwazi na pale wanawatumia dawa za asili katika kutoa tiba na si vinginevyo. Hata hivyo, anasema hivi sasa yameibuka makundi ya wanamazingaombwe na wapiga ramli, ambao wanawadanganya wananchi na kufanya vitendo vingi viovu katika jamii.

“Hawa ni sawa na wanaokula nyama za watu, mganga wa kweli utatumaje mtu akaue binadamu mwenzake, hawa si waganga, hakuna mganga anayeweza kumwambia mtu akanajisi watoto, akaue vikongwe,” anasema. Anaongeza kuwa kuwafumbia macho wapiga ramli, ipo hatari kwa vitendo viovu kuendelea kuongezeka katika jamii. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Zelothe Stephen, anasema jeshi la polisi limekuwa likiboreshwa kiutendaji.

Anasema kwamba wananchi wanatakiwa kutoa taarifa za siri kwa viongozi wa jeshi hilo; na zitafanyiwa kazi kwa haraka; na mwananchi aliyetoa siri, hatatajwa popote pale. Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa Mbeya, John Mwakipesile, anawapongeza mamwene na machifu, kwa kuanzisha umoja wao, ambapo anasema serikali inawatambua na kwamba inaelewa mchango wao katika shughuli za maendeleo.

"Serikali haijasahau, inawatambua na inaelewa mchango wenu katika shughuli za maendeleo," anasema. Mwakipesile anasema Serikali itaendelea kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwakutanisha na viongozi wa kitaifa, wanaotembelea Mkoa wa Mbeya kwa ziara za kikazi. Baadhi ya wananchi wanasema teknolojia hiyo ya kuhamishia mimba, itakuwa ya kwanza na ya aina yake kutokea duniani.

Solomoni Mwansele anasema kuwa ikiwa jambo hilo ni la kweli; na ikatokea kweli mwanaume akahamishiwa mimba kwa njia za kimaajabu na wazee hao wa mila, Tanzania inaweza kuushangaza ulimwengu. Anasema ubunifu huo, unaweza kusaidia kukabiliana na mimba za wanafunzi. Brandy Nelson anasema kuwa Serikali haiamini katika masuala ya ushirikina na ni ndoto kwa serikali kutoa kibali kama hicho.

“Siamini kama kinachoongelewa kinawezekana, wapo watoto wa machifu na wazee wa mila wanapata mimba, lakini hatujawahi kushuhudia wakiwa wamewahamishia mimba wanaume waliowapa mimba watoto wao,” anasema. Anahoji kwa nini wazee hao wa mila, waibuke leo wakati tatizo la mimba limepigiwa kelele kwa muda mrefu?

Mnasemaje wanaharakati kuhusu hili?

No comments: