Thursday, February 26, 2009

Mrejesho wa Semina za GDSS- Maandalizi ya Kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.

Siku ya Kimataifa ya Wanawake (International Woman's Day -IWD) inaadhimishwa tarehe 8 Machi ya kila mwaka Ulimenguni pote. Ni sikukuu ya kidunia ya kusherekea mafanikio na harakati za wanawake katika nyanja za Uchumi, Siasa, na Kijamii. Siku hii ilianza kama tukio la kisiasa, na chimbuko lake ni kutoka katika tamaduni za nchi zilizokuwa jamuhuri ya Kisovieti ya Russia. Taratibu siku hii ilipoteza asili yake ya kisiasa na badala yake kuwa siku ambayo wanaume wanaonyesha/kueleza upendo wao kwa wanawake. Hata hivyo, dhana za kisiasa na haki za binadamu kama zilivyobuniwa na shirika la Umoja wa Mataifa-UN na kupenyezwa katika siku hii, zinaendelea kuwa imara, na kusadia harakati za kisiasa na kijamii za wanawake kuangaliwa katika hali inayotia matumaini zaidi.
Nchini Tanzania, wanaharakati wa haki za binadamu na Wanawake -TGNP na FemAct- wameendelea kuungana na wanaharakati wengine duniani kote katika maandalizi ya kuiadhimisha tena siku hii. Mara nyingi siku hii huadhimishwa kwa kuandaliwa mijadala ya wazi, semina, vipindi vya television na redio, na shughuli zingine ambazo zitaonyesha/kueleza harakati za kumkomboa mwanamke kimapinduzi zinazoendelea katika nchi yetu. Katika semina za kila jumatano za GDSS, wiki hii-tarehe 25/02/2009- wanaharakati waliweza kukutana na kujadiliana juu kuadhimisha siku hii muhimu. Wanaharakati waliweza kukubaliana juu ya kauli mbiu ya mwaka huu na waliona ni vyema ilenge/kuisisitiza serikali irudishe rasilimali kwa wananchi zaidi. Hivyo walikubaliana kauli mbiu ya mwaka huu iwe;
Kuwahudumia Wagonjwa wa UKIMWI Majumbani ni jukumu letu wote, Wanawake, Wanaume, na Serikali”
Wanaharakati walikubaliana na kauli mbiu hii na kuioanisha na mgogoro wa kiuchumi unaoendela duniani ambao unaongeza machungu na mateso kwa wanawake zaidi; kwa sababu mgogoro huu utasababisha upunguzwaji wa wafanyakazi katika sekta mbalimbali kwa mfano walimu, wafanyakazi wa afya na viwandani, na uchangiaji wa huduma za afya utazidisha machungu zaidi kwa wanawake. Utunzaji wa wagonjwa wa walioathrirka na VVU majumbani unaamanisha kuongezeka kwa mzigo wa kazi kwa akina mama majumbani, na shida zaidi ni kwa watu wanyonge-wasio na uwezo wa kifedha. Hivyo wanaharakati wanapendekeza haja ya kuilazimisha serikali iongeze rasilimali zaidi kwa watu wa aina hii ambao wana haki ya kudai rasilimali zaidi kutoka serikalini kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hawa.

Pamoja na mambo mengine wanaharakati wanadai kuwepo na mfumo mbadala ambao utatoa fursa kwa wanawake, wazee, na watoto kupata huduma za afya kwa gharama za serikali tofauti na sasa ambapo sera zinasema hivyo lakini utekelezaji wake umekuwa wakusuasua sana. Wagonjwa wengi hawana hata fedha ya nauli ya kwenda klinic kuchukua dawa, achilia mbali fedha ya kununua vyakula vyenye virubisho! Wanaharakati wanadai siku hii ya wanawake duniani mwaka huu iadhimishwe ili kutoa fursa kwa jamii yetu kuwa na upendo na akina mama kitu ambacho kitasaidia kuwalinda na kuwaenzi akina mama kama wazazi na watu muhimu katika maisha ya kila siku.

Wanaharakati wametoa wito kwa wanajamii kuiadhimisha siku hii kwa kuwatetea wanawake ili wapunguziwe mzigo wa kazi uliotokana na mfumo wa jamii yetu.

Ukiwa kama mwananchi wa kawaida unashiriki vipi katika kuiadhimisha siku hii muhimu? Na kuhakiksha juhudi zako zinaleta mabadiliko katika maisha ya wanawake wengi hasa wale wanyonge?

Jiandae katika ushiriki wa Siku hii Muhimu tarehe 8 Machi, 2009!

1 comment:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

safi sana kwa historia ya siku hii maana wabongo huwa tunadandia na kusheherekia tusiyoyajua, asante kwa kunitoa gizani jama.

sasa tukimpunguzia mzigo huyu mwanamke, itakuwaje? si tukibanwa na majukumu ndipo maisha yetu yanakuwa ya raha kwamba tuko bize tunajishughulisha?

wnawake siku zote ni wakombozi wa jamii, na wako mbele kuikomboa na wataendelea hivyo. tusiilaumu sana serikali kabla ya kjikagua sisi wenyewe.

I LOVE WOMEN