Semina hii ilifanyika jumatano ya tarehe 18/03/2009 katika viwanja vya ofisi za TGNP Mabibo na kuhudhuriwa na washiriki kutoka mikoa ya Morogoro, Pwani, na Dar es salaam pamoja na wanaharakati wengine walio katika sekta ya elimu nchini. Wawezashaji walikuwa ni Mama Shekilango na Rehema Mwaiteba(TENMET).
Mada ililenga kuangalia elimu kwa watoto wa kike katika mikoa mitatu ya kanda ya mashariki ambayo ni Dar es salaam, Morogoro, na Pwani. Watoa mada walitoa mrejesho wa utafiti uliofanywa na TENMET mwaka 2008 katika mikoa hiyo mitatu. Utafiti huo ulikuwa na Lengo la kujionea hali halisi ya elimu ya mtoto wa kike katika mikoa hiyo ili kuweza kubaini changamoto wanazokutana nazo watoto wa kike katika kupata elimu ya msingi, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kampeni inayoendelea ya kumpatia elimu mtoto wa kike.
Utafiti huo ulilenga kuangalia mambo makuu manne katika elimu ya wasichana ambayo ni; upatikanaji wa elimu(accesibility), kuendelea na masomo(continuation, kupanda darasa moja hadi lingine(transition), na kumaliza kwa elimu ya msingi(completion). Katika maeneo hayo manne yameonyesha bado kuna upungufu mkubwa, kwa mfano upatikanaji wa elimu bado ni wa tabu katika maeneo mengi yaliyofanyiwa utafiti-mf; shule nyingi za serikali hazina vyoo, vitabu ama walimu wa kutosha hivyo elimu inayopatikana haitoshelezi. Pia wasichana wengi wameshindwa kumaliza/kuendelea na shule kutokana na vikwazo kama utoro, mimba, kuzidiwa na kazi za nyumbani hasa za kutafuta kipato na kutunza wagonjwa, nk.
Michango kutoka kwa washiriki ni pamoja na;
• Bado kuna upungufu wa shule za awali-chekechekea serikali hajaweka shule hizi za awali ingawa sera inasema kwamba kila shule ya msingi ni lazima iwe na vyumba vya madarasa ya awali, lakini maeneo mengi bado yanaonyesha hayana madarasa hayo. Shule za awali za binafsi zipo lakini wananchi wengi wa hali ya chini wameshindwa kupeleka watoto wao katika shule hizo.
• Upatikanaji wa elimu bora unategeamea sana na mazingira ya shule, afya bora ya mwanafunzi, mwamko wa jamii husika juu ya elimu, utamaduni/mila potofu za jamii kuhusu kumsomesha mtoto wa kike, hali ya uwezo wa familia husika, na mahusiano ya walimu na wanafunzi, lakini kutokana na utafiti bado jamii yetu imeshindwa kutoa mazingira mazuri kama haya kwa ajili ya kuwapatia elimu watoto wa kike.
• Urasimu katika usajili wa shule za watu binafsi pia ulitajwa kama mojawapo ya chanzo cha upungufu wa shule za awali katika baadhi ya maeneo. Kwa mfano mshiriki mmoja kutoka Morogoro alisema, Morogoro kuna shule zaidi ya 40 za awali ambazo zinasubiri usajili, hali imesababisha upungufu wa shule hizi.
Nini Kifanyike
• Wanaharakati waishinikize serikali isifunge shule za bweni kwa kushindwa kuwalipa wazabuni wa chakula. Serikali inapaswa kutoa elimu kwa raia wake wote bila kubagua, ili waje kulitumikia taifa lao. Serikali inapaswa kuwalipa haraka wazabuni hao na kuendeleza shule hizo za bweni kama awali.
• Wanaharakati walipendekeza kianzishwe kitengo cha ushauri kwa watoto wa kike katika shule za watu binafsi na serikali ili kiwasaidie wasichana wanapopata matatizo wanapokuwa shuleni, na pia waweze kupata elimu ya kujisitiri wanapokuwepo mashuleni.
• Wanaharakati waishinikize serikali iongeze bajeti ya wizara ya elimu kutoka 18% ya mwaka jana, na kuangalia upya mgawanyo wa fedha hizo ili nyingi zitumike katika maendeleo ya elimu nchini.
• Jamii inapaswa ielimishwe umuhimu wa kumuelimisha mtoto wa kike na kumpa nafasi ya kujisomea pindi awapo nyumbani, pamoja na kumpunguzia kazi ambazo zinawezwa kufanywa hata na wavulana mf. kuteka maji, kufua, usafi wa mazingira nk.
• Wanaharakati watoe tamko la pamoja juu ya jambo hili, ikiwa na pamoja na kulipeleka jambo hili katika majukwaa mengine ya wanaharakati kama breakfast debate za policy forum nk.
• Nafasi za Halmashauri ziweke bayana katika kuimarisha elimu ya msingi nchini hasa elimu ya wasichana. Kwa sasa halmashauri ndizo zinazosimamia shule za msingi nchini lakini zimeshindwa kuleta maendeleo husika katika sekta hiyo.
Semina hiyo ilifungwa na kuacha majukumu ya ufuatiliaji kwa wanaharakati, ambapo maadhimio hayo yalitakiwa kutolewa mrejesho kwa wanaharakati katika siku za usoni.
Ukiwa kama mwanaharakati na mdau wa elimu kataka nchi yetu, unafanya nini ili kuhakikisha elimu ya msingi kwa watoto wa kike inaboreshwa?
No comments:
Post a Comment