Tuesday, March 17, 2009

Katika haya yote, yu wapi Kikwete?

HIVI karibuni Rais Jakaya Kikwete aliwajia juu viongozi wa zamani wanaoikosoa serikali yake “vijiweni”.

Ingawa hakutaja majina ya viongozi hao, ni dhahiri alikuwa akiwazungumzia kina Joseph Warioba, Cleopa Msuya, Joseph Butiku, Hassy Kitine, Bakari Mwapachu na wengine kadhaa ambao katika siku za karibuni walitumia haki yao ya kikatiba kuzungumzia namna nchi inavyoendeshwa.

Kwa kuamua kutumia neno “vijiweni” (wanaikosoa serikali ‘vijiweni’), Rais Kikwete alilenga katika kuwafanya Watanzania wawapuuze viongozi hao wastaafu, kwa sababu, kwa mtazamo wake, hawana hoja.

Je, Watanzania tunapaswa kukubaliana na Rais Kikwete kwamba viongozi hao wastaafu ni wa kuwapuuza? Je ni kweli hawana hoja katika kila walichokizungumzia, na kwamba ushauri wao si chochote wala lolote?

Sitaki kuzungumzia alichozungumzia Jenerali Ulimwengu, wiki iliyopita, kwamba watawala wetu wakishakamata madaraka hujaribu pia kuhodhi fikra na kujiona ni wao tu ndiyo wanaojua kila kitu; lakini napenda nikite katika kile kilichozungumzwa (‘kijiweni’?) na mmoja wa viongozi hao wa zamani ambao Rais Kikwete anataka tuwapuuze.

Namzungumzia Bakari Mwapachu ambaye ameitumikia Serikali ya Tanzania kama waziri kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi. Katika mahojiano na gazeti hili, Mwapachu alilalamika, miongoni mwa mambo mengine, kwamba mambo hayaendi vizuri kwa sababu tunatumia muda mwingi mno wa utendaji kwa kupiga domo!

Kwa hakika, kauli hiyo si mpya; kwani ilishapata kutolewa huko nyuma na Jaji Warioba ambaye alilalamika kuwa nchi sasa inaendeshwa kwa malumbano. Kwamba badala ya viongozi serikalini na katika chama tawala kushughulikia masuala ya kimsingi ya maendeleo, wamejikita katika kulumbana wenyewe kwa wenyewe.

Je, si kweli kwamba walichokisema Warioba na Mwapachu ni sahihi; hata kama walikisemea ‘vijiweni’? Na kama si sahihi, utayaelezeaje haya tunayoyaona yakiendelea hivi sasa katika mihimili mitatu ya dola; yaani Serikali, Mahakama na Bunge?

Nazungumzia malumbano kati ya Bunge na Serikali, Mahakama na Bunge, na hata kamati moja ya bunge dhidi ya kamati nyingine ya bunge ndani ya mhimili huo. Kwa hakika, hata mhimili wa nne (press) nao haujasalimika katika malumbano haya.

Tumefika mahali pa kutisha ambapo kamati mbili za bunge moja, chini ya spika mmoja, zinalumbana zenyewe kwa zenyewe hadharani; kama tulivyoshuhudia hivi karibuni katika sakata hili la ununuzi wa mitambo ya kufua umeme ya Dowans.

Tumefika mahali pa kutisha ambapo mhimili wa Mahakama unalumbana hadharani na mhimili wa Bunge kuhusu ni nani hasa championi wa kusimamia haki; huku kila upande ukitumia katiba kuhalalisha nguvu iliyonayo dhidi ya mwenzake.

Tumefika mahali hatari ambapo utendaji wa serikali unagubikwa na usanii; kiasi kwamba kauli zake sasa haziaminiki tena moja kwa moja.

Leo, Waziri (Ngeleja) atasema kamwe Serikali haitanunua mitambo chakavu ya Dowans, lakini kesho waziri huyo huyo atasema mitambo hiyo lazima inunuliwe!

Tumefika mahali Rais (Kikwete) anasema hakuna mwanafunzi wa chuo kikuu atakayeshindwa kusoma kwa sababu ya ukosefu wa ada, lakini miezi kadhaa baadaye watoto wa wakulima masikini wanatimuliwa vyuoni kwa sababu baba zao hawana fedha za kuchangia gharama za kuwasomesha!

Tumefika mahali mbunge kijana aliyekuwa championi wa kutetea sheria na haki (Zitto) katika kutetea hoja yake ya kunuuliwa mitambo chakavu ya Dowans anasema sheria ya manunuzi iliyopitishwa na bunge si msahafu, na hivyo isiwe kikwazo cha ununuzi huo!

Wakati (Zitto) akiyasema hayo, mbunge mwenzake (Dk. Mwakyembe) naye anajitokeza hadharani na kumjibu kwamba ni heri nchi ikae gizani kuliko kununua mitambo hiyo chakavu ya Dowans ambayo mpaka leo umma haujatajiwa mmiliki wake halisi!

Na katikati ya malumbano haya ya wabunge (Zitto vs Mwakyembe na Shelukindo) Spika wao, Samuel Sitta naye anajitokeza hadharani na kuungana na Shelukindo na Mwakyembe kwa kusema kwamba kama Serikali itanunua mitambo hiyo chakavu ya Dowans, itakiona cha moto bungeni!

Kauli hiyo bila shaka ndiyo iliyomchochea mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba kuliambia gazeti la Mtanzania, toleo la Jumamosi iliyopita,kwamba Sitta na Mwakyembe ni maadui wa CCM! Je, wanakuwa maadui wa chama chao kwa sababu tu ya kuishauri serikali iachane na mpango wa kununua mitambo chakavu ya Dowans (binamu wa Richmond, kwa mujibu wa Spika Sitta!)?

Katikati ya malumbano hayo, Ikulu ya Rais Kikwete ikatoa taarifa kuhusu kikao ambacho Rais alikifanya na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini; taarifa ambayo dhahiri inaonyesha kuwa hata Ikulu nayo imeingia katika malumbano hayo ya Dowans.

Aya “D” ya taarifa hiyo ya Machi 3, 2009, inasomeka hivi kuhusu maelekezo yaliyotolewa na Rais Kikwete katika kikao hicho: “Ziongezwe juhudi katika uzalishaji wa umeme nchini kwa sababu programu ya taifa ya uzalishaji umeme bado iko nyuma na bado liko pengo kubwa katika mahitaji halisi ya umeme nchini na umeme unaozalishwa kwa sasa.”

Nayo aya “E” inasomeka hivi: “Dhana ya tenda na Sheria ya Manunuzi isiruhusiwe kuwa kikwazo katika miradi mikubwa mikubwa ya miundombinu ya nishati….”

Ukitafakari kwa makini aya “D” na aya “E” unaona wazi kwamba kauli ya Rais inafanana na iliyotolewa na Zitto Kabwe kwamba Sheria ya Manunuzi si msahafu. Kwa maneno mengine, kauli hiyo ya Rais inabariki kununuliwa kwa mitambo hiyo ya DOWANS; hata kama ni kuizunguka sheria ya nchi iliyopitishwa na Bunge.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu, Salva Rweyemamu alilumbana na gazeti la Mwananchi akidai kwamba taarifa yake haikugusia kabisa suala la Dowans. Ni kweli, lakini Mtanzania yeyote mwenye akili anajua kwamba aya “E” ya taarifa hiyo ilikuwa inalenga mitambo ya Dowans; vinginevyo ni manunuzi gani mengine yenye utata ambayo katika siku za karibuni yamehusishwa na Sheria ya Manunuzi kama si mitambo hiyo ya Dowans?

Au tuamini kwamba ilikuwa ni coincidence tu kwa Rais Kikwete kuitaja, hivi sasa, sheria hiyo ya manunuzi katikati ya mjadala huo wa Dowans? Kwa mtazamo wangu, ingekua vyema kama Rais Kikwete angelijitokeza wazi wazi na kueleza msimamo wa Serikali yake kuhusu manunuzi hayo ya mitambo chakavu ya Dowans, badala ya kuchomeka kijembe ambacho kinaendeleza tu malumbano. Ni nani asiyejua kuwa kauli ya Rais ni ya mwisho, na wala halazimiki kufuata ushauri wa Bunge?

Lakini funga-kazi katika sakata hili la mitambo ya Dowans ni kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk. Idriss Rashid aliyoitoa mwishoni mwa wiki. Yeye ameamua kuzira na kuitoa Tanesco katika mpango huo wa kununua mitambo hiyo. Amefanya hivyo si kwa hoja, bali kwa kuzira na kususa; huku akisema wananchi watajijua wenyewe nchi itakapogubikwa na giza!

Dk. Idriss aligoma kujibu maswali ya waandishi wa habari, na yalikuwa mengi ambayo mpaka leo hayana majibu – Ni nani mmiliki wa Dowans? Kwa nini Tanesco ing’ang’anie kununuliwa mitambo chakavu ya Dowans badala ya kuishauri serikali ianze mchakato wa haraka (fast track) wa kununua mipya?

Kutojibiwa kwa maswali hayo na mengine mengi kunajenga hisia kwamba kuna kitu ambacho Serikali inajaribu kuuficha umma, na hisia hizo ndizo zinazofanya malumbano haya yapambe moto; kama yalivyokuwa mengine huko nyuma.

Kwa ufupi, unaweza kuandika kitabu kizima kabisa cha jinsi Serikali ya Rais Kikwete ilivyotawaliwa na usanii na malumbano ya wenyewe kwa wenyewe tangu ilipoingia madarakani mwaka 2005.

Nimezungumzia mifano hiyo michache ya karibuni ya malumbano, na sikutaka kabisa kuzungumzia mingine iliyopata kuibuka huko nyuma kuanzia ya Buzwagi, Bulyanhulu, Meremeta, Balali na EPA, Kagoda na EPA, Richmond, Kiwira, Majengo Pacha ya BOT, TICT, OIC, Vyuo Vikuu n.k

Kwa hiyo, Mwapachu anaposema tunapiga domo na kulumbana badala ya kukaa chini na kupanga mikakati ya kuendeleza nchi yetu na kuwapunguzia wananchi wetu umasikini, anachosema ni kweli kabisa; hata kama anakisemea ‘kijiweni.’

Kama yasingekuwa yanaathiri uchapaji kazi wa Serikali, pengine malumbano haya yangekuwa yanafurahisha, na kwa wengine ingekuwa ni burudani ya aina yake inayoonyesha kukomaa kwa demokrasia yetu na jinsi tunavyoheshimu uhuru wa kujieleza na kukosoana!

Lakini ukweli ni kwamba yameathiri mno utendaji wa Serikali. Vitu vya msingi vimewekwa pembeni; wakati usanii, malumbano na scheming za ki-mitandao zikiendelea!

Na mfano mzuri ni ziara ya ghafla ya Rais Kikwete ya hivi karibuni katika bandari ya Dar es Salaam ambako alikuta maagizo yake aliyoyatoa miezi mitatu iliyopita hayajatekelezwa. Ni nani alipaswa kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo ya Rais?

Bila shaka ni Waziri wa Miundombinu. Alikuwa wapi muda wote huo hadi Rais mwenyewe kulazimika kwenda, ni swali ambalo nawaachia wenyewe mjibu; kwani sote tunaijua nguvu ya ki-mtandao ya TICT katika bandari hiyo.

Liko suala hili jingine (kwa mfano) la matrekta ambayo tuliambiwa yataagizwa kwa pesa za EPA zilizorejeshwa na mafisadi. Je yameshanunuliwa? Na kama jibu ni ndiyo, ni matrekta mangapi? Utaratibu wa kuyapata ni upi? Bei itakuwa ni nafuu au itakuwa ni bei ya soko?

Hakuna mwenye majibu ya maswali haya ambayo, bila shaka, wakulima wangependa kuyajua. Hakuna majibu kwa sababu watawala wanaopaswa kutoa majibu hayo wako kwenye malumbano na scheming za ki-mtandao!

Chukua mfano mwingine. Mwanzoni mwa mwaka huu Rais alitembelea mkoa wa Mbeya. Alipofika Mbarali alisikitika baada ya kuona mwekezaji, aliyeuziwa kwa bei chee mashamba ya mpunga yaliyokuwa ya umma, ameamua kuyageuza kuwa ya kilimo cha mibono (jatrofa) badala ya mpunga kama mkataba unavyosema.

Kwa kujua wazi kwamba hatua hiyo itaathiri kiasi cha mpunga unaozalishwa mkoani Mbeya (hutoa asilimia 60 ya mpunga wote unaozalishwa nchini), Rais aliagiza mwekezaji huyo aache mara moja kulima mibono na kama hataki kulima mpunga, basi, mashamba hayo yarejeshwe tena kwa umma. Muda mrefu umeshapita tangu atoe agizo hilo, je hilo limefanyika?

Nina hakika agizo lile liliishia pale pale Mbarali; kwani wanaopaswa kulitekeleza wako bize na malumbano ya ufisadi na scheming za ki-mtandao!

Majuzi hapa, Rais wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Strauss Khan alitahadharisha kwamba kipindi cha Nchi Zinazoendelea, zikiwemo za Afrika, kuanza kuathirika na anguko la uchumi wa dunia kimewadia, na hivyo zianze kuwa makini. Alisema kwamba kuna awamu tatu za kuathirika – ilianza Marekani, zikafuatia nchi nyingine tajiri zilizoendelea, na sasa ni kipindi cha Nchi Zinazoendelea zikiwemo za Afrika.

Je, watawala wetu Tanzania wameisikia tahadhari hiyo ya Strauss Khan? Sitashangaa kama hawakuisikia; kwani wako bize na malumbano ya ufisadi na scheming za ki-mtandao!

Lakini swali kuu la kujiuliza ni hili: Katikati ya malumbano haya, mwenye kigoda (Rais Kikwete) kasimamia wapi? Ni muhimu kujiuliza swali hili kwa sababu Rais ana nguvu na mamlaka makubwa yanayomwezesha kukomesha mara moja malumbano haya na kuirejesha nchi katika mwelekeo sahihi.

Je, amejaribu kufanya hivyo? Siamini kama amejaribu kufanya hivyo; kwani hata kukemea tu hatujamsikia akikemea malumbano haya na scheming hizi za ki-mtandao ambazo zinaathiri utendaji wa serikali yake.

Binafsi, kuna wakati napata hisia kama vile anayafurahia malumbano haya na scheming hizi za ki-mtandao zinazoendelea ndani ya serikali, asasi za umma na ndani ya Bunge.

Nimalizie tafakuri yangu kwa kusema kwamba, mpaka hapo atakapowakemea watendaji wake kuacha malumbano haya na scheming hizi, na kuwahimiza watendaji wake warejee katika uchapaji kazi, hana uhalali wa kuwajia juu kina Warioba, Butiku, Msuya, Mwapachu, Kitine nk wanaojaribu kukemea hali hii inayotukwaza; hata kama wanakemea kwenye ‘vijiwe’.

Tafakari.

Raia Mwema,Machi 11, 2009

No comments: