Friday, March 13, 2009

Mrejesho wa GDSS - Ukuaji wa Uchumi wa Tanzania Unamsaidiaje Mtu wa Chini?

Mrejesho wa Semina wa GDSS iliyofanyika jumatano ya tarehe 11/03/2009 katika ofisi za TGNP Mabibo. Mada ilikuwa ni Ukuaji wa Uchumi wa Tanzania Unamsaidiaje Mtu wa Chini? Mada hii ambayo ilikuwa na lengo la kuendeleza mjadala kuhusu zahama/mgogoro wa uchumi duniani na kufanya tathimini iwapo ukuaji wa Uchumi wa Tanzania unamnufaisha mwananchi wa hali ya chini, iliwakilishwa na Bubelwa Kaiza kutoka Concern for Development Initiatives in Africa (ForDIA).

MJADALA KWA UREFU.
Mtoa mada alitafsiri neno Uchumi ambapo alisema ni mahusiano yaliyopo kati ya mwananchi na shughuli za uzalishaji kwa kuangalia mambo yafuatayo.
i) Mapato/shughuli inayoleta ujira. Mfano: Kazi za kuajiriwa, Shughuli za kilimo na Biashara.
ii) Uwezo wa kununua. Mfano: Manunuzi ya bidhaa/ kupata huduma.
iii) Uwezo wa kuchagua bidhaa/ huduma husika.

Alisema, takwimu za IMF zinaonesha kukua kwa uchumi nchini kwa zaidi ya 7%, lakini ukuaji huu hauendani kabisa na kupungua kwa umasikini kwa watanzania,na hivyo kushindwa kutoa nafuu ya maisha kwa wananchi walio wengi na kupelekea kuongezeka kwa pengo la kipato kati ya “Walionacho” na “Wasionacho” pengo ambalo limetajwa kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Bubelwa katika uwasilishaji wake huo, alionesha wasiwasi mkubwa kwa jinsi ambavyo vigezo katika ukuaji wa uchumi nchini vinavyoangaliwa na taasisi hiyo kubwa ya fedha duniani. Ailisema “Wakati wanapoangalia mauzo ya jumla hapa nchini kama kigezo kimojawapo katika ukuaji wa uchumi, hali ni tofauti kabisa kwani hakuna uhalisia kabisa katika matumizi ya bidhaa husika kwa mtanzania wa hali ya chini”.

Huku akisikiliza michango ya mawazo kutoka kwa wana GDSSS ambao nao hawakukubaliana na vigezo vimumiwavyo namashirika husika katika kutoa tathmini ya ukuwaji wa uchumi nchini, mtoa mada aliendelea kubainisha vigezo vingine vinavyotumia katika kupima ukuaji wa uchumi na ufanisi wake kutia shaka hapa nchini kuwa ni pamoja na:-

i) Uwiano uliopo katika utoaji wa huduma, ambapo alisema kuwa ni mdogo kati ya watoa huduma na wapewaji na kutolea mfano wa uchache wa madaktari na wauguzi katka sekta ya afya, hivyo kutostahili katika tathmini hiyo hapa nchini na kuonyesha shaka kuwa yawezekana vinatumika kwa ajili ya kuonyesha utukufu wa sera kandamizi za IMF na washirika wake.
ii) Utoaji wa elimu kwa kuzingatia ubora, nacho kama kigezo kingine kilikuwa na dosari nyingi kama wana GDSS walivyo bainisha kutokana na kutokuwa na uhalisia na maisha ya wananchi wa kawaida. Ulitolewa mfano wa ujenzi wa shule nyingi za sekondari usioendana na idadi ya walimu waliopo, hivyo kupelekea kuanzishwa utaratibu wa mafunzo ya muda mfupi ambao kwa hakika hawana uwezo wala sifa za kufudisha watoto na kusababisha kiwango cha elimu kushuka siku hadi. siku.
iii) Pengo la kipato kwa wananchi ambalo imechangiwa na watu wachache kujilimbikizia mali isivyo halali, ukosefu wa ajira, kukosa udhati kwa serikali katika kutoa fursa ya biashara za kazi kwa wananchi wazawa na kudorora kwa sekta ya kilimo nchini.
iv) Uwajibikaji, Uwazi na fursa ya kuhoji utendaji wa serikali pia kimekuwa ni kitendawili maana sasa kila mtu anafanya atakalo. Mikataba mibovu kila kukicha tena katika sekta nyeti na viongozi kutokupenda kuwajibika hata pale yanapobainika matatizo waliyotusababishia mpaka litoke shinikizo kutoka kwa IMF na washirika wake.
v) Uwezo katika maamuzi/uthubutu wa taifa katika maamuzi ndicho kigezo ambacho wana GDSS walikipinga zaidi kwa utamua uwezo mdogo wa kimaamuzi uliopo na hivyo kutoa majumuisho ya jumla kuwa hawakubaliani na takwimu za IMF kuwa uchumi wa Tanzania umekuwa bali kwa kuzingatia igezo hivyo wanaamini uchumi umeshuka kwa kiwango kikubwa.

NINI KIFANYIKE
Baada ya mjadala mrefu kufanyika, wana GDSS kwa pamoja walitoa mapendekezo kadhaa kwa serikali na wananchi kwa ujumla ili kuhakikisha juhudi za makusudi zinafanyika na kunusuru mamilioni ya watanzania ambao wanaishi maisha ya duni kutokana na serikali kukumbatia sera za mabepari. Hivyo katika muktadha huo yafuatayo yaliazimiwa katika semina hiyo:-
i) Ufanyike mjadala wa kitaifa kujadili/kuhoji utekelezaji wa sera za IMF na WB nchini kwetu ili kubaini ukweli juu ya dhamira yao kwetu na kupanga mkakati madhubuti kwa kuishinikiza serikali yetu kubadili mtazamo wa utekelezaji wa mipango yake kwa kujali zaidi maslahi ya wananchi wake kuliko maslahi ya wachache.
ii) Tupinge kwa nguvu zote utekelezaji wa sera/mipango yote isiyo na tija kwetu hivi sasa kutoka kwa taasisi zote kubwa za fedha duniani kama IMF na Benki ya Dunia(WB) na nchi tajiri wakati tukishinikiza kuwepo kwa mjadala wa kitaifa kuhusu mustakabali wa taifa letu.
iii) Kuongeza ushawishi kwa umma/ wananchi wengi zaido ili kushirikisha maisha yao na uchaguzi wa viongozi wa serikali katika ngazi mbalimbali.
iv) Kufanya mabadiliko katika uongozi wa serikali kuu kila tunapoona malengo tuliotarajia hayakufikia matarajio/baada ya kushindwa kuleta maendeleo stahili na hali bora kwa wananchi walio wengi.
v) Kuanzisha mtaala wa elimu kuhusu uzalendo na kuwa na malengo ya kitaifa.
vi) Kuhimiza wasomi na wataalamu wengine nchini wajitoe muhanga katika kuleta maendeleo nchini badala ya kuwaachia wanasiasa peke yao.

HITIMISHO
Wakati wa kufanya hitimisho la semina, ilikubaliwa na washiriki wote kuwa pamoja na kuitaka serikali yetu itazame upya utekelezaji wa sera za mashirika makubwa ya fedha duniani na nchi wahisani lakini ni jukumu letu pia kuwa na macho ya umakini kwa viongozi tunaowachagua ili kuzuia/kuepuka mfumo wa uwakala/kibaraka ambao kwa kiasi kikubwa umeifanya serikali yetu kuwajibika zaidi kwa IMF, WB na mashirika mengine makubwa ya fedha ama nchi tajiri duniani kuliko wananchi wake jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limeathiri hata utendaji katika ngazi ya serikali za mitaa.

Ukiwa kama mwanaharakati unashiriki vipi kuhakikisha Ujumbe huu unawafikia walengwa?

Ripoti imetayarishwa na Ally Nindi.

2 comments:

Anonymous said...

Ally Nindi, nimefurahi sana kusoma report hii kutoka hapo nyumbani Tanzania. Kusema kweli IMF/WB policy ndio zimetufikisha hapa tulipo leo. Kuanzia SAPs za mwaka 1980s ambapo tulipewa ERP I kitu kilichochoea kuuwa viwanda vya ndani ya nchi, kuongezeka kwa maambukizi ya HIV/AIDS (sababu tulikatazwa kufund elimu).

Leo kabla sijakutana na blog hii nilikuwa nachambua MGD na MKUKUTA(NSGRP) ambapo kumejaa adithi ambazo hazionekani ni kwa njia gani zinaweza kufikiwa.

Kilimo bado ni 60% ya mapato ya serikali yatokanoyo na usafirishaji wa bidhaa nje. Lakini 36% ya wakulima hao bado wanaishi chini ya mstari wa umasikini wa Tanzania. NSRGP walisema watapunguza hiyo namba mpaka nusu yake kabla ya mwaka 2010, lakini mpaka sasa hakuna ane fungu mdomo kusema nini kimetokea.

Kelele za IMF na WB kuhusu uchumi kukua kwa 7% zinatokana na ukuaji wa sector ya madini ambapo serikali kuu ya Muungano haipati hata 10% ya revenue yake. Kukua kwa uchumi kwa 7% hakujaleta mabadiliko kwa zaidi ya 80% ya Watanzania sababu bado kwa 19 kupungua kwa umasikini kumeshukwa kwa karibu 4% ukilinganisha na kelele wanazopiga IMF, WB and TAKUKURU.

Mwisho..
Mkuu Ali naomba kama kuna link yoyote ya kujua website ya GDSS.
mtanganyika01@yahoo.com

Anonymous said...

ipo haja ya kuangalia upya hii dhana ya ukuaji wa kiuchumi kwani inavyoonekana longolongo zimekuwa nyiiingi kuliko vitendo, wananchi wapate fursa ya kuelimishwa na kueleza maoni yao juu ya swala hili, huo uchumi uliokuwa upo wapi?