Friday, March 27, 2009

Raza: Nchi imeoza

-Asema tatizo ni uongozi wa juu wa CCM
-Ashauri viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi wakae pembeni

ALIYEKUWA Mshauri wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mohamed Raza, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), ‘kimeoza’ katika safu ya uongozi wa juu.

Hata hivyo, Raza anasema pia kwamba CCM bado ni imara katika ngazi ya matawi na ameshauri kufanywa kwa mabadiliko ya uongozi, na kusisitiza viporo vya kashfa za ufisadi vikamilishwe kabla ya Uchaguzi Mkuu, mwakani, ili chama hicho kipate wepesi wa kujinadi kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, kada huyo machachari kutoka Zanzibar amesema ni busara zaidi vigogo wanaotuhumiwa kwa ufisadi na ambao wanachunguzwa, lakini bado wakiendelea kushika madaraka ya juu katika CCM, waachie ngazi ili kukipa nguvu na heshima chama hicho mbele ya wapiga kura nchini.

Raza (pichani), aliyekuwa akimshauri aliyekuwa Rais wa SMZ, Dk. Salmin Amour Juma katika masuala ya michezo, alitoa msimamo na ushauri wake huo katika mahojiano maalumu na Raia Mwema, wiki iliyopita, jijini Dar es Salaam, huku akiweka bayana kuwa tegemeo pekee la wananchi kwa sasa katika kulinda maslahi yao ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Huko CCM juu watu wakae kitako, umaarufu wa mtu unatokana na chama na si mtu. Huko ndiko kumeharibika. Nafasi ipo watu wazoefu pia wapo, sasa warekebishe huko juu,” alisema Raza bila kutaja ni nafasi gani za juu zilizopwaya katika kukiongoza chama hicho kikongwe nchini.

Hata hivyo, alidokeza kwa namna nyingine akisema ; “Mimi nafikiri mfano huu wa Dowans, Bunge limetoa ushauri wake suala hili liachwe, ofisa waandamizi wametoka wanataka kununua Dowans, lakini tayari Richmond imetokana na Dowans.

“Hadi Spika wa Bunge, ambaye ni mwana-CCM anatoka kusisitiza ushauri anasema hapana sasa wote hawa wanaovutana ni CCM hakuna Chadema wala CUF. Kwa hiyo tatizo lipo katika uongozi wa juu wa CCM.

“Kuna mbunge anamwambia mbunge mwenzake wa CCM…bwana hapo ulipofika tulizana kuna mambo nikizungumza patakuwa hatari nchi inaweza kuingia katika zahma. Sasa hii ni one system, hakuna Chadema, CUF wala TLP. Kwa hiyo katika hali hiyo tatizo lipo na kama tatizo lipo tusilifungie macho tu.

“…kama Tanzania kungelikuwa na upinzani bora, imara na wa kweli CCM isingelibakia…believe me, kama tungelikuwa na upinzani uliokuwa wa ujasiri loo! Kwa hivyo tushukuru kwamba CCM, chama changu, hatuna upinzani, lakini CCM tunajivunia tunakubalika kwenye grass root wanatukubali na wanaendelea kutukubali,” anasema katika mahojiano hayo yatakayochapishwa katika toleo la wiki ijayo.

Kwa upande mwingine aliwageukia waandishi wa habari nchini akisema; “Nataka kuwasihi waandishi wa habari, bora wale mhogo na viazi, lakini waweke mbele nchi yao. Bora wale mhogo lakini wajiamulie mambo yao kwa maslahi ya Taifa. Nasi Watanzania bora tule mhogo na viazi, lakini tujiamulie mambo yetu wenyewe.”

Lakini pia anawazungumzia viongozi waandamizi serikalini na wananchi akisema; “Mtu anakuja anakwambia mimi natoa milioni 600 au 700 katika uchaguzi…huyu ana lake…atakuumiza. Nilisema mimi katika uchaguzi mwaka 2005, nendeni mkasome magazeti, nilisema bwana hizi pesa zinazotoka hawa wanatakiwa kuja kuzilipa na watakapoanza kuzilipa watakuwa wana-command sasa leo ndiyo haya.”

Anashauri wana-CCM wenzake na hasa viongozi kwamba ni vema ufumbuzi wa viporo vya ufisadi ukapatikana kabla ya Uchaguzi Mkuu mwakani.

“Kwa sababu tunataka kurudi kwa wananchi najua kuna mambo ya Mahakama huwezi kuingilia, lakini katika yale mambo ambayo unaweza kuyafanya mapema, tuyakamilishe kabla ya kuingia katika uchaguzi,” anasema.

Katika mahojiano hayo, Raza anaonekana kuwashangaa viongozi wa Serikali wanaolalamikia watendaji wanaovujisha siri za Serikali.

Katika kuwashangaa anasema; “Leo mimi nashangaa viongozi na watendaji wengine wanalalamika siri zinavuja. Hivi unachota bilioni 100, mimi pango na ada ya mtoto sina, sehemu nyingine za nchi hakuna huduma ya maji, shule nyingine hazina madawati. Watoto wanakaa chini, mbavu zinawauma; wewe unachota mabilioni halafu unalalama siri zinavuja?!”

“Mtu sasa utakuta kazikusanya kwa ubinafsi wake mabilioni kwa mabilioni ya shilingi; huku wananchi wakiwa na umasikini, wanahitaji huduma za msingi za maji, umeme na barabara. Halafu tunasema Tanzania ni nchi masikini, ndiyo…sawa nchi masikini lakini sisi wenyewe tunajisimamia vipi?”, anahoji.

Katika kuthibitisha imani aliyokuwa nayo kwa Bunge, Raza anasema; “Kama si Bunge, nchi ingekuwa pabaya sana…nafikiri watendaji kama wanataka kuvaa kanzu nzuri basi hiyo fulana yao ya ndani waioshe isitoe harufu, lakini usivae kanzu una fulana inatoa harufu ndani au unavaa koti shati yako inatoa harufu ndani. Kwa hiyo kama unataka kuvaa kanzu basi fulana yako isafishe na kama ni suti pia shati yako isafishwe.”

Source: www.raiamwema.co.tz

1 comment:

Anonymous said...

Kweli nchi yetu inahitaji marekebisho makubwa ili kuisaidia kuwa sawa kutokana na halisi ya ufisadi wa makusudi unaoendelea hapa sasa, lakini wananachi wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika hili kwani viongozi wetu wameshaonekana sio watu wa kutegemewa sana katika hili. Kila la kheri kwa wale wote wanaopingana na unyonyaji wa raia kwa hali yoyote...