Tuesday, March 24, 2009

Mafisadi kuamua nani awe rais 2010?



-Mbunge wa CCM asema nchi iko rehani
MBUNGE wa Kishapu, Fred Mpendazoe, amesema kutokana na matajiri mafisadi kuachwa wakitamba watakavyo, zipo dalili za wazi sasa kwamba wamejipanga kuamua nani awe rais wa nchi, mbunge, waziri na hata diwani; wakipora jukumu hilo kutoka kwa wananchi.

Akionyesha kukerwa na mwenendo wa mambo na hasa kuimarika kwa matabaka miongoni mwa wananchi, mbunge huyo amesema mafisadi hao wameweka mizizi yao ndani ya serikali, na nchi inaelekea kuwekwa rehani kwao.

“Kinachofanyika sasa kinazidi kutoa harufu ya ufisadi kwenye serikali. Upo msemo wa kisambaa unaosema kama unataka kuepuka nzi tupa kibudu cha mzoga. Kama Serikali inataka kuepuka harufu ya ufisadi, ishughulikie vyanzo vya ufisadi na iviondoe la sivyo itaendelea kuandamwa na kashfa,” anasema Mpendazoe katika mahojiano na gazeti hili ambayo yamechapishwa kwa kina.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, tatizo kubwa linaloitafuna serikali ya sasa ni uteuzi kufanyika katika misingi ya urafiki; hali inayowakwaza wenye mamlaka ya kuteua na hatimaye kushindwa kuwawajibisha wateule pale wanaposhindwa kutimiza wajibu wao.

“Upo msemo kwamba A friend in power is a friend lost; yaani rafiki yako akipata madaraka na dhamana kubwa ya kuongoza anakoma kuwa rafiki,” anasema na kufafanua kuwa;

“Anakoma kuwa rafiki yako ili aweze kutekeleza majukumu yake bila kuwa na upendeleo wowote. Nchi nyingi zinazoendelea zina tatizo hili. Mtu anapopata madaraka utakuta anaweka rafiki zake kwenye sehemu nyeti akidhani watamsaidia kumbe huwa ni kinyume chake.”

Akizungumzia kuhusu nchi kuwekwa rehani, mbunge huyo alisema ni jambo hatari sana, “maana yake serikali itaongozwa na matajiri na hivyo haitawajibika tena kwa wananchi na demokrasia itakoma na udikteta utaanza.

“Serikali haitakuwa ya watu na kwa maana hiyo haitachaguliwa na watu na haitawajibika kwa wananchi. Matajiri wataamua nani awe rais, nani wawe wabunge kwenye majimbo,” anasema na kuongeza kuwa;

“Wananchi hawatachagua madiwani wanaowataka. Baadaye matajiri wataamua nani awe waziri, jaji na wakuu wa vyombo vya dola ili kuhakikisha maslahi yao yanalindwa sehemu zote kwa mwavuli wa maslahi ya Taifa.

Na zipo dalili za kuelekea huko. Serikali inapochelewa kuchukua hatua haraka juu ya ufisadi unaotendeka si dalili nzuri.”

Katika kushauri nini kifanyike, mbunge huyo alisema; “Mfumo wa utawala tulionao unaotokana na Katiba hautoi fursa kwa watendaji kuwajibishana bali unatoa nafasi kubwa ya kulindana.

Ni mfumo wa viongozi kulindana badala ya kuwajibishana inapobidi.”

Akiweka wazi msimamo wake kuhusu sakata la ununuzi wa mitambo ya kufua umeme ya Dowans, na hususan kauli ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, mbunge huyo alimshauri waziri huyo kuwasilisha hoja yenye malalamiko yake kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ili yajadiliwe.

Katika hatua nyingine, alitonya kuwa kuna uwezakano wa kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu suala la Dowans, na alipoulizwa lini hatua hiyo inaweza kufanyika alijibu kwamba ni katika mkutano ujao wa Bunge.

Raia Mwema,18 Machi,2009.

No comments: