Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imepeleka serikalini mchanganuo wa maombi ya fedha kwa ajili ya kustaafisha kwa maslahi ya umma wafanyakazi wapatao 70 wa kampuni hiyo, kutokana na kuelemewa kiutendaji kwa idadi kubwa ya wafanyakazi.
ATCL yenye wafanyakazi 300 ina jumla ya ndege tano na mbili kati ya hizo aina ya Bombadia Dash 8 zenye uwezo wa kubeba abiria 50 ndizo zinazofanya kazi kwa sasa, jambo lililoelezwa kutowiana na uwezo wa gharama za uendeshaji.
Mchanganuo huo utakapokubalika serikalini, utahusu wafanyakazi wenye umri mkubwa, wanaokaribia kustaafu, wasio na taaluma yoyote na wakatisha tiketi, watu wa mapokezi bila kugusa wataalamu, wakiwamo marubani na wahandisi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa ATCL, Balozi Mustafa Nyang’anyi alisema leo bila kutaja kiasi walichoomba serikalini, kuwa tayari wamewasilisha mchanganuo wa fedha zinazohitajika kwa kazi hiyo na kwamba wanasubiri na kuwa habari zilizoandikwa juzi na gazeti moja la kila siku (si HabariLeo) kuwa wanapeleka likizo na kustaafisha wafanyakazi takriban 150, si za kweli.
“Hakuna mazungumzo wala hatua yoyote iliyofikiwa ya kupeleka watu likizo bila malipo na hatua ya kustaafisha watu ni kwa maslahi ya umma na si ya sasa, maana inahitaji fedha nyingi, hatujui Serikali itatoa fedha lini, pengine mwaka ujao wa fedha,” alisema Balozi Nyang’anyi.
Kwa upande wake, kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (COTWU), tawi la ATCL, ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, alithibitisha kufanyika vikao vya mchakato wa kupunguza wafanyakazi kwa kuwastaafisha na kukazia kuwa mpango wa likizo bila malipo walishaukataa na endapo ukiibuliwa, watagoma upya.
Mwishoni mwa mwaka jana, ATCL ilipata msukosuko baada ya kunyang’anywa leseni ya kurusha ndege na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kutokana na kubainika dosari katika nyaraka muhimu na baada ya kufunguliwa, ilipewa na Serikali Sh bilioni 4.5 za uendeshaji, lakini ulizuka mzozo baada ya menejimenti kuwatangazia wafanyakazi kuwa watapewa likizo bila malipo, kutokana na uhaba wa fedha.
Baada ya suala hilo kufutiliwa mbali kwa vikao vya ndani vya kampuni, Bodi na wafanyakazi, hivi sasa Serikali ipo katika mazungumzo na kampuni ya China iitwayo China Sonangol International Limited (CSIL) kwa ajili ya kuingia nayo ubia baada ya kuvunja mkataba na Kampuni ya Afrika Kusini (SAA) miaka mitatu iliyopita kutokana na kubaini hali ya kampuni hiyo kuwa hatarini.
No comments:
Post a Comment