BURIANI KAKA KITWANA KASANZU
TANZIA
Mtandao wa Wanaharakati wa Haki za Binadamu na Masuala ya Jinsia (FemAct), tumestushwa sana na msiba wa ghafla wa mwanaharakati mkongwe na shupavu kaka
Kasanzu Kitwana(Pichani),kiongozi wa the African Youth Alliance, kilichotokea ghafla nyumbani kwake siku ya Ijumaa tarehe 5 Agosti 2008, majira ya saa mbili na nusu usiku.
Marehemu pamoja na kuwa mmoja wa Wanachama shupavu wa Mtandao wa Jinsia Ngazi ya Kati Kinondoni (KIGN) na Kiongozi wa The African Youth Alliance, pia alitoa mchango mkubwa sana katika harakati za ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi Vijana na Watoto Tanzania. Kwa kweli huu ni msiba mkubwa sana kwetu kwa sababu tumempoteza mpiganaji shupavu na hodari.
Wakati wa uhai wake marehemu alifanya kazi kwa karibu sana na FemAct katika harakati za kudai haki za Wanawake, Vijana na Watoto na kuhakikisha kwamba usawa na haki zao zinazingatiwa pamoja na sera na mipango madhubuti inapangwa na kuwalinda.
Pia FemAct inakumbuka mchango na ushiriki wake mkubwa katika matukio mbalimbali ikiwemo Matamasha ya FemAct ya Jinsia yanayofanyika kila baada ya miaka miwili (GF) Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) zinazofanyika kila Jumatano TGNP Mabibo. Na Jumatano ya mwisho kushiriki semina hizi, marehemu Kasanzu alikua ni miongoni mwa washiriki katika uzinduzi wa machapisho ya Hali Halisi ya Kijinsia Tanzania pamoja na tathmini ya Miaka Kumi Baada ya Beijing uliofanyika siku ya tarehe 27 Agosti 2008 katika viwanja vya TGNP.
Tunapenda kuungana na Wanaharakati wote katika kuwapa pole wale wote walioguswa na msiba huu hususan kwa watoto na familia yake, Wanaharakati na Taifa kwa ujumla. Hakika marehemu ameacha pengo kubwa katika mapambano ya harakati nchini, pengo ambalo tunaamini litakuwa ni chachu ya kuendeleza Mapambano ya kudai haki za binadamu na Ukombozi wa wanawake wote. Tunapenda kutumia fursa hii pia kutoa mwito kwa Wanaharakati wote tuendeleze utamaduni wa kuwaenzi wanaharakati wenzetu wanapofikwa na mauti kama ishara ya kutambua mchango wao katika mapambano ya harakati nchini
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya kaka Kitwana Kasanzu mahali pema peponi.
Imetolewa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa niaba ya FemAct.
Imesainiwa na Sekretariat ya FemAct,
Usu Mallya, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)
Mratibu
Mtandao wa Wanaharakati wa Haki za Binadamu na Masuala ya Jinsia (FemAct),
Tarehe 9, Septemba 2008
2 comments:
Napenda kuwapa pole wanaharakati wote katika kipindi hiki cha msiba huu mkubwa. Wote tunafahamu kwamba tunapata bahati yakuishi kipindi kifupi sana hivyo hatuna budi kutumia wakati wetu vizuri kwa ajili ya maendeleo ya jamii yetu.
Nawapa pole familia ya wafia na wanaharakati wote.
Mdau.
Napenda kuwapa pole wanaharakati wote katika kipindi hiki cha msiba huu mkubwa. Wote tunafahamu kwamba tunapata bahati yakuishi kipindi kifupi sana hivyo hatuna budi kutumia wakati wetu vizuri kwa ajili ya maendeleo ya jamii yetu.
Nawapa pole familia ya wafia na wanaharakati wote.
Mdau.
Post a Comment