Kuelekea Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Kutathimini Hali ya Afya.
Mkutano Mkuu wa kila mwaka wa kutathimini sekta ya afya ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 8/10/08 utawashirikisha wadau mbalimbali wa maswala ya Afya ambao ni pamoja na; wizara ya Afya, Tamisemi, Mashirkia yasio ya Kiserikali, na Nchi wahisani na natarajiwa kujadili mambo yafuatayo: Mkakati wa serikali wa miaka sita ijayo katika sekta ya afya; Kutathimini mipango iliyopita; kuangalia ufanisi wa kiutendaji na utoaji wa Huduma; na kuangalia Changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa sera ya afya.
Katika Mkutano huo wanaharakati watawakilishwa na Kikundi cha Utetezi wa Haki sawa kwa Wote Katika Afya (A Group for Health Equity) Kikundi Kinachoundwa na taasisi zinazopigania haki za binadamu. Jumatano ya tarehe 24/09/2008 katika Semina za Jinsia na Maendeleo, Wanaharakati walijadili mapendekezo ambayo wanataka yawasilishwe katika mkutano huo. Pamoja na mambo mengine walipendekeza mambo yafuatayo yakajadiliwe na kupatiwa ufumbuzi; Sera ya Taifa ya Afya ya Mama na Watoto chini ya Miaka Sita Inatekelezwa kama inavyosema; Serikali inatekeleza Makubaliano ya Abuja(Abuja Declaration) yaliyofikiwa na viongozi wa nchi huru za Afrika mwaka 2000 juu ya sera ya afya; Mkakati maalumu wa Kupunguza vifo vya akina mama uliozimiwa na serikali na wadau wengine tarehe 22/04/2008 unatekelezwa kama makubaliano hayo yalivyoafikiwa; na serikali ichukue hatua dhidi ya wale wanaochukua rushwa katika sekta ya afya.
Pia wanaharakaati walipendekeza serikali iangalie upya rasilimali inayotengwa katika afya ya mama na watoto chini ya miaka sita, kwani mpaka sasa vifo vya akina mama wanaojifungua vinaendelea kutokea kwa kasi kubwa na kuhakikisha rasilimali kama wahudumu, vifaa vya uzazi, vifaa vya mawasiliano, miundo mbinu kama maji, umeme, na barabara vinaboreshwa kutokana na kuchangia sana vifo vya wajazito. Wanaharakati wametakiwa kufuatilia kiasi cha fedha na matumizi yake katika maeneo yao wanayotokea kuanzia ngazi ya kata mpaka wilayani, hii itasaidia katika kufuatilia na kutathimini utekelezaji wa sera ya afya kama ilivyopangwa.
Wanaharakati walipendekeza serikali itenge kiasi cha bilioni 10 kwa ajili afya ya akina wajazito kiasi hiko ni sawa na asilimia 1.7 ya fedha ya bajeti ya wizara ya afya, tofauti na sasa ambapo imetenga kiasi cha bilioni 3.6 amabacho ni sawa na asilimia 0.05 ya fedha yote ya bajeti ya wizara ya afya kwa mwaka 2008.
Pendekezo lingine la wanaharakati ni kuishawishi serikali inasimamia utekelezaji wa sera ya Afya ya uzazi kama ilivyo, kwa sasa wanawake wengi wanakufa wakati wa kujifungua kutokana na kukosa fedha za kununulia vifaa vya kujifungulia (Delivery Kit). Vifaa hivyo kwa mujibu wa sera ya serikali ni bure kabisa.
Ndugu mwanaharakati unachangia nini katika kuboresha sekta hii ya afya? Je unadhani serikali imefanya vya kutosha katika kuboresha sekta hii ya afya? Je, nini kifanyike katika kuboresha sekta hii ya afya- hasahasa katika eneo hili la afya ya uzazi?
1 comment:
Serikali yetu imeshindwa kabisa kuchukua hatua juu ya hali ya uzembeaji wa huduma za afya hasa afya ya uzazi. Nadhani endapo kungekuwepo na juhudi za dhati hali hii ingezwa kuboreshwa na kurekebishika kabisa. Wito wangu kwa wanaharakati ni kwamba waendelee kupiga kelele juu ya jambo hili na wajitahidi kukusanya nguvu kubwa ya wananchi ili waweze kushiriki katika vita hii muhimu ya kuwasaidia akina mama wanaojifungua na watoto wadogo chini ya miaka mitano.
Post a Comment