Tuesday, September 2, 2008

FEMACT YATOA MAONI KUHUSU HOTUBA YA RAIS BUNGENI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Sisi wanamtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali yapatayo 50 yanayotetea usawa wa jinsia, haki za binadamu na ukombozi wa wanawake kimapinduzi (FemAct) tunatambua umuhimu wa hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuhutubia bunge mnamo tarehe 21 Agosti 2008 na kutoleaa kauli masuala kadhaa mazito yanayohusu mustakabali wa taifa letu ambayo kwa muda sasa yamekuwa yakijadiliwa na wananchi. Moja ya masuala hayo ni lile la wizi wa zaidi ya shilingi bilioni 133 kutoka Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Rais alisema tayari shilingi bilioni 53 kati ya shilingi bilioni 133 zilizoibwa zimesharejeshwa na kwamba alikuwa amewapa muda hadi Oktoba 31 mwaka huu (2008) wale wote ambao hawajarejesha fedha walizoiba wawe wamezirejesha vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Kadhalika Rais aliliambia bunge kuwa watu waliobainika kuiba fedha hizo kutoka akaunti ya EPA Benki Kuu wamefilisiwa na pia kunyang’anywa pasi zao za kusafiria.

Sisi FemAct tunaamini kuwa mafisadi wa EPA ni watu hatari walioifilisi nchi yetu. Kwa hiyo tunamshauri Rais abadilishe uamuzi wake wa kuwasamehe mafisadi hao badala yake aachie sheria ichukue mkondo wake. Tunaona kuwa kitendo cha mafisadi hao kusamehewa kabla ya sheria kuchukua mkondo wake kutafifisha vita dhidi ya ufisadi ikiwa ni pamoja na wizi wa mali ya umma na hivyo kuchafua heshima ya serikali na taifa kwa ujumla. Hakika mahali popote duniani ambapo vita dhidi ya rushwa na wizi wa mali ya umma vimefanikiwa ni pale tu ambapo kumekuwa na uwazi dhidi ya uovu huo.

Aidha Rais anapaswa pia autangazie umma majina ya maafisa wa BOT waliohusika na EPA ambao watakuwa wamechukuliwa hatua na uongozi wa benki hiyo. Kutowataja watu hao na kuchukuliwa hatua za kisheria kutawafanya maafisa wengine wa serikali wenye tabia ya kushiriki kukwapua mali za umma kuendeleza wizi wa mali ya umma kwa kasi. Sisi FEMACT tunaamini kabisa kuwa kashfa hii ya EPA ni fursa nzuri kwa Rais kuudhihirishia umma kwamba yuko tayari kupambana na mafisadi wanaoiba mali ya umma.

Tunahofu kwamba kama mafisadi wa EPA hawatashtakiwa huenda ikawa ni mwanzo wa nchi yetu kujenga matabaka ya wazi ya watu walio juu ya sheria na wengine walio chini ya sheria. Wakati wa uhai wake Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kuonya kwamba kuwaonea huruma watu dhalimu hujenga taifa lenye tabaka jambo ambalo ni hatari kwa amani ya taifa. Katika kuhimiza kuwa wadhalimu wasipewe nafasi katika taifa letu Mwalimu alisema “Wadhalimu muda wote lazima waandamwe hata kama wangekuwa wakubwa kama Mlima Kilimanjaro”.

FemAct tunaona ni muhimu pia kutafakari ni nini hasa athari za wizi wa fedha hizo nyingi bilioni 133 kwa maisha ya Mtanzania wa kawaida hawa wanawake na makundi mengine katika jamii? Kwa mfano kila siku wanawake zaidi ya 24 wanakufa hapa nchini wakati wa kujifungua kutokana na kukosa fedha za kununulia vifaa muhimu vya kumsaidia visivyozidi shilingi elfu kumi tu na ambavyo vingepaswa kutolewa bure na serikali kama huduma ya afya ya msingi. Fedha hizo zilizoibwa kwenye EPA zingetosha kuepusha vifo vya uzazi kwa wanawake zaidi ya milioni 13 na laki tatu na hivyo kuimarisha nguvu kazi muhimu ya maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla. Aidha tunapaswa tujiulize je fedha hizo zilizoibiwa zisingeweza kutosheleza kutoa mafunzo kwenye sekta ya afya na hivyo kupata maelefu ya madaktari na wauguzi ambao wangeokoa maisha ya wananchi wengi wanaokufa hasa vijijini kwa kukosa huduma za tiba? Je zisingetosheleza kujenga mabweni mengi kwa shule za sekondari za serikali na kuepusha adha wanazopata watoto wa kike kutokana na kukosekana kwa mabweni? Je zisingetosha kujenga maabara, maktaba na kununulia vitabu kwa ajili ya shule zote za sekondari zinazohitaji huduma hizo?

Rais aliseme fedha zinazorejeshwa na wezi hao zitatumika katika kuongeza ruzuku ya mbolea na dawa za mifugo na nyingine zitawekwa katika Benki ya Rasilimali (TIB) ili wakulima wakopeshwe mikopo yenye masharti nafuu na ya muda mrefu. Sisi FEMACT, hatupingi fedha hizo kuelekezwa kwa wakulima na wafugaji, kwa sababu tunatambua kuwa Watanzania wengi hasa wanawake na makundi mengine ya jamii yaliyopo pembezoni kiuchumi wako kwenye sekta ya kilimo na ufugaji. Lakini suala la msingi ni kuhakikisha usimamizi mzuri wa mgawanyo wa hiyo rasilimali na uwajibikaji. Tunaamini kuwa bunge ndicho chombo pekee kwa niaba ya Watanzania chenye mamlaka ya kuidhinisha matumizi ya fedha za umma na kufuatilia matumizi yake. Tunaona hatari ya fedha hizo kutowafikia walengwa kama hazitagawiwa na chombo chenye mamlaka ya kusimamia rasilimali za taifa. Aidha tunaona hatari ya kuweka fedha hizo TIB kwa sababu kama mafisadi waliweza kupenyeza na kuiba kwenye akaunti ya EPA iliyokuwa kwenye chombo nyeti kama Benki Kuu, watashindwaje kuingia Benki ya Rasilimali na kuiba tena fedha nyingine ili kukidhi matakwa yao?

Usu Mallya, TGNP
Mratibu
Mtandao wa wanaharakati wa Masuala ya Jinsia, Haki za Binadamu na Ukombozi wa wanawake (FemAct)
27th August, 2008

2 comments:

Anonymous said...

kwanza ninampongeza raisi kwa hotuba yake nzuri,na kupitia hotuba hii tumeona mapungufu mengi kupitia hotuba yake kama ifuatavyo;
1.Ameshindw kupata ujasiri wa kuwataja hao wahujumu uchumi na mafisadi wa nchi yetu.
2.kuendelea kuwapa muda wa kurudisha pesa badala ya kuwapeleka mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
3.kudai pesa zile si serikali wala si za wananchi.
4.kuingilia kazi ya bunge kwa kupanga matumizi ya pesa hizo.

r.maduka@yahoo.com

Anonymous said...

Ni mawazo mazuri kutoka ktk haya mashirika mmeonyesha njia inanifanya niamini kua wanaharakati tukiungana tunaweza kufanya mambo makubwa hata kuushinda ufisaddi.Tuko pamoja na ikibidi tutaandamana ili kulinda rasilimali zetu.
KUWASAMEHE/KUWAPA MUDA MAFISADI NI SAWA NA KUKUBALI UAFIDHINA WAO. HAIKUBALIKI HATA KIDOGO!!!!!
tunatakiwa tuonyeshe mfano kwa kuchukia ufisadi ili isitokee tena siku nyingine, WAFUNGWE MAISHA.