Adhabu ya kifo yaibua mjadala Bungeni miezi michache iliyopita na tumeshuhudia mjadala mkali kuhusu hukumu ya kifo. Baadhi ya wabunge walibishana na serikali kuhusu umuhimu wa kuendeela kuwepo kwa adhabu hiyo.
Wabunge wanataka ifutwe wakiwa na hoja mbili; kwanza wanasema adhabu hiyo haitekelezwi inavyotakiwa hapa nchini na pili wanasema ni adhabu ya kikatili.
Mhe.Kilontsi Mporogonyi yeye amesema kuwa hakuna mwanadamu ambaye anayo mamlaka ya kutoa uhai isipokuwa Mungu pekee, na mwelekeo unaonyesha kuwa nchi nyingi duniani zipo katika mchakato wa kufuta adhabu hii.
Hata hivto mjadala huo haukuendelea sana kwa sababu uliibuka katika kipindi cha maswali na majibu, ambapo mkuna kanuni ambayo inadhibiti idadi ya maswali yanayoulizwa. Kwa maana hiyo walichangia wabunge wawili tu.
Aliyeibua mjadala ni Mbunge wa Mchinga, Mhe.Mudhihiri Mudhihiri, aliyetaka kujua kwa nini adhabu hiyo isifutwe au kubadilishwa na kuwekewa kipimo cha kifungo.
Mudhihiri aliuliza swali hilo baada ya Naibu waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.Mathias Chikawe, kujibu swali la msingi lililouklizwa na Mhe.Mudhihiri kwa niaba ya Mhe.Richard Ndassa (Sumve-CCM) akitaka kujua idadi ya watu ambao walishanyongwa katika awamu zote za uongozi na awamu iliyoridhia utekelezwaji wa adhabu hiyo.
Ndassa aliitaka serikali kuleta muswada bungeni, ili kuifuta sheria inayotoa adhabu ya kifo kwa sababu uzoefu unaonyesha kuwa utekelezaji wa hukumu hiyo umekuwa mgumu na mzito hasa kwa mamlaka ya mwisho ya kusaini hati ya kumnyonga mwenye hatia.
Akiongezea katika hilo, Mudhihiri alisema tendo la kuua ni la kikatili na mara nyingi watu wanaohukumiwa kunyonga hadi kufa hawanyongwi hadi kufa kwa sababu hukumu hiyo inachelewa mno kutekelezwa.
Kutokana na hilo, Mhe.Mudhihiri alipendekeza kuwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa ingetengenezewa mbadala na kuwa na adhabu ya kifungo, ili mtu atakapohukumiwa kunyongwa afahamu kuwa asiponyongwa baada ya muda huo, anakuwa huru kwa sababu amekamilisha adhabu yake.
Hata hivyo, upande wa serikali ulionekana kutokubaliana na hoja zilizoibuliwa na wabunge hao, huku Mhe.Chikawe akisema kuwa pamoja na kuwa nchi nyingi zinataka kuifuta adhabu hiyo, lakini zipo pia nchi ambazo ziliifuta adhabu hiyo na sasa zinataka kuirejesha.
Akipinga dhana kuwa adhabu hiyo haitekelezwi, Mhe.Chikawe alisema kuwa jumla ya watu 82 wameshanyongwa katika awamu zote nne za utawala tangu nchi ijitawale.
Akifafanua, Mhe.Chikawe alisema kuwa kati ya watu hao, kumi (10) walinyongwa katika awamu ya kwanza ya utawala na 72 walinyongwa katika awamu ya pili. Hakuna mtu aliyenyongwa katika awamu ya tatu na nne.
Hata hivyo, ili kujiridhisha kama bado adhabu hiyo bado ni muafaka kwa wakati huu na iwapo inaendana na matakwa ya haki za Binadamu, Mhe.Chikawe alisema kuwa serikali imepanua wigo wa wananchi kutoa maoni.
Alisema kuwa serikali imeiagiza tume ya kurekebisha sheria kuanza mchakato na hatimaye kutafuta maoni ya wananchi ili kuona kama adhabu hii iendelee kuwepo katika vitabu vya sheria za nchi.
Je wewe unaonaje kuhusu kuwepo au kutokuwepo kwa adhabu hii?
1 comment:
Kuwa na adhabu ya kifo ni kufuru kwa Mwenyezi Mungu!
Mwenye uwezo wa kutoa uhai wa mtu ni muumba pekee, sisi binadamu hatuna mamlaka hayo, hayo ni maandiko matakatifu yasemavyo hivyo, kwa utukufu gani tulionao tuanze kuamulia watu kama waishi au wapoteze uhai!!!! Sikutegemea kama rais mstaafu Mwinyi aliruhusu watu kunyongwa!
Mimi nadhani tunakiuka maandiko ya Mungu na haki za binadamu.
Pablo,
Mabibo
Post a Comment