Rais na Waziri Mkuu walihutubia taifa tarehe 21 na 29 wakiwa na lengo la kuelezea umma juu ya msimamo wa serikali juu ya maswala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Wana-GDSS walijadili juu ya hotuba hizo mbili Jumatano ya tarehe 3/09/08, mada ambayo iliongozwa na Geofrey Chambua, huu ni mrejesho mfupi juu ya mjadala huo.
Kwa ufupi, washiriki walikubaliana kuwa hotuba zote mbili hazikukizi matarajio ya wananchi juu ya hatua za serikali za kupambana na ufisadi. Ingawa hatua za mwanzo zilizochukuliwa za kumfukuza gavana wa benki kuu, kurudisha baadhi ya fedha zilizochotwa, kufunga akaunti ya EPA na kuunda tume, bado zinaonekana hazitoshi dhidi ya watuhumiwa wa skendo hizo za ufisadi.
Hotuba zote mbili hazikuonyesha matumaini ya kuwashughulikia watuhumiwa, wananchi walitegemea majina ya watuhumiwa kutajwa pamoja na makampuni yaliyohusika katika skendo hilo tofauti na mbinu za kuchelewesha kuwaadhibu zilizojitokeza katika hotuba hizo.
Baadhi ya washiriki wa GDSS waliona hotuba zinatoa changamoto nyingi za kufuatilia, hivyo imeweza kuwaamsha na imewasaidia kufikiria zaidi juu ya hatua za kuchukua hapo baadae. Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na; kufuatilia sheria ya uchaguzi itakayotolewa Januari 2009, kuhakikisha kwamba usawa wa aslimia 50 kwa 50 unafikiwa bungeni, sheria ya maadili ya uongozi inazingatiwa, na fedha za EPA zinazorudishwa zinatumika katika shughuli za kilimo kama zilivyopangwa.
Pia wana-GDSS waliona ni muhimu kwa jamii kuelewa hali iliyopo ili iweze kupitia, kuchanganua, na kutathimini vitu kwa undani na huku ikiendelea kuisimamia na kuishawishi serikali ili iwajibike katika maswala ya jamii yetu.
Je wanaharakati wanawezaje kutumia nafasi yao katika kufikisha taarifa hizi kwa jamii hasa ile inayoishi katka maeneo ya vijijini?
No comments:
Post a Comment