Monday, September 15, 2008

Tanzania iseme hapana kwa EPA hii

WIZARA ya Viwanda, Biashara na Masoko iliandaa warsha ya siku moja mjini Dar es Salaam, kujadili juhudi zinazofanywa na Umoja wa Ulaya (EU), wa kuwa na mpango mpya wa kibiashara wa Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchuni (EPA) kati yake na nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (ACP).

Warsha hiyo iliyoandaliwa maalum kujadili utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Misaada la Oxfam la Uingereza, ilikubaliana na matokeo utafiti huo, kwamba mpango huo mpya wa Ulaya ni kitanzi ambacho kitaua maendeleo ya nchi hizo kufanya ziendelee kuwa tegemezi la wakubwa hao wa kisiasa na kiuchumi.

Tunaunga mkono msimamo ulioonyeshwa na washiriki wote wa warsha hiyo, iliyowashirikisha wadau mbali mbali, wakiwamo wawakilishi wa vikundi vya kijamii na wafanyabiashara, kwamba mpango huo haufai.

Kama ilivyojitokeza katika warsha, kuingia kichwa kichwa kusaini mkataba wa mpango huo mpya wa ushirikiano itakuwa ni kosa la karne, ambalo halipaswi kufanywa na watu wa kizazi cha sasa, waliokwenda shule.

Akichangia katika warsha hiyo, Mzee Arnold Kileo alitahadharisha kwamba kusaini mpango huo itakuwa ni sawa na kuirudisha nchi yetu katika enzi za machifu, waliorubuniwa kwa shanga kuuza ardhi zao kwa kusaini mikataba wasiyoielewa.

Kwa kifupi ni kwamba, vipengele vilivyomo katika Mkataba wa EPA havina maslahi kwa nchi zetu zinazoendelea. Ulaya inataka kutumia msuli wake wa kiuchumi kuziburuza nchi hizo ziendelee kuteseka na umasikini na ukosefu mkubwa wa ajira.

Ushirikiano unaotaka kufanywa na Ulaya unaoweza kulinganishwa na wa Goliati na Daudi, katika uwanja usiokuwa tambarare, utaleta majuto makubwa kwani utavuruga mambo mengi kwa hali ilivyo sasa kiuchumi katika eneo letu.

Kwa mfano, mfumo wa utozaji kodi, kama unavyosomeka katika kifungu cha 15 cha mkataba huo, unazitibua nchi zilizomo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili tu ya kuunufaisha Umoja wa Ulaya.

Cha kufurahisha ni kwamba, kupitia warsha hiyo, wadai walihakikishiwa na wachangiaji wa upande wa serikali, kuwa Tanzania haiwezi kutia saini katika mkataba huo kama ulivyo hivi sasa.

Kama kweli kuna umuhimu wa kufanya biashara na Ulaya, basi iwe katika uwanja wa tambarare. Hivyo basi, tunaunga mkono wote wanaotaka serikali iendelee kushirikiana na wadau wote na kufikia uamuzi wa kusaini pale tu marekebisho yatakapofanywa, ambayo yataondoa kasoro zote zilizoonekana kwa wakati huu.

Bila ya hivyo, Tanzania iseme HAPANA kwa mpango huo, kwani utauza uhuru wetu na kutuzidishia umasikini na ukosefu wa ajira utakuwa mkubwa zaidi.

Raia Mwema
Sept 10, 2008.

2 comments:

Anonymous said...

kwa nionanvyo mimi EPA si kingine zaidi ya kuendeleza unyanyaji kwa nchi maskini na na kujaribu kurudisha tena zama za ukoloni, ikiwa sasa ni hali ya uwazi kabisa. NChi za afrika hazina budi ziungane ili ziweze kuchana na hali ya unyanyaji, na endapo hazitaungana basi zikubali kuendelea kunyonywa na mabeberu hawa..

Mdau

Anonymous said...

huu utaratibu wa EPA ni mtindo mwengine wa kutaka kuleta unyonyaji kwa Waafrika na hakuna jambo lolote zaidi, lakini kwa kuwa waafrika tumekataa kuungana basi tutanyonywa mpaka mwisho.
Nawasikitia watoto wa Afrika watakaokuja baada yetu..Mungu ibariki afrika