Friday, October 29, 2010

Mbivu na mbichi kuwa Jumapili

SIKU chache kabla ya kupiga kura Jumapili ijayo, wagombea watatu wa urais wanaochuana, Jakaya Kikwete wa CCM, Dk. Willibrod Slaa wa CHADEMA na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, wamekuwa na vigezo vinavyotofautiana mbele ya macho ya wapiga kura wengi, Raia Mwema imebaini.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kete kubwa ya Dk. Willibrod Slaa inayovutia wengi ni uadilifu, umakini na uwajibikaji kama alivyojipambanua akiwa mbunge kwa miaka 15, wakati Jakaya Kikwete wa CCM kampeni zake tofauti na mwaka 2005 zimetegemea zaidi mtandao wa chama hicho na kivuli chake cha urais. Hali hiyo ni tofauti na mwaka 2005 alipokuwa na mvuto zaidi kuliko chama hicho.

Wachambuzi wa mambo wanasema umaarufu wa Kikwete umeshuka kinyume cha 2005 kutokana na wananchi kujua upande wake wa pili kiutendaji kama Rais wa Tanzaia. Lakini wakati hali ikitajwa kuwa hivyo kwa Dk. Slaa na Kikwete, kwa upande wa Profesa Ibrahim Lipumba anavutia zaidi wapiga kura wanaomuunga mkono kutokana na kigezo cha usomi wa taaluma inayoaminika kuhitajika zaidi kwenye nchi inayodaiwa ni masikini kama Tanzania. Mtazamo wa wapiga kura wengi ni kama ifuatavyo.

Dk. Willibrod Slaa

Kabla ya kampeni kuhitimishwa Jumamosi, Dk. Willibrod Peter Slaa amezidi kujipambanua kama kiongozi mwenye nia ya dhati kusimamia maadili, uadilifu, umakini na uwajibikaji. Inaelezwa kuwa amekiinua mno chama chake ikilinganishwa na wagombea urais wengine kutoka kambi ya upinzani.

Kwa mfano, mwaka 1995, chama kilichokuwa na mvuto zaidi kilikuwa NCCR-Mageuzi na ndicho kilichotia changamoto zaidi CCM lakini kilianza kupoteza mvuto kwa kadiri miaka ilivyosogea kikitoa nafasi kwa Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kilitwaa nafasi ya chama kikuu cha upinzani hasa katika chaguzi za mwaka 2000 na 2005.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, CHADEMA kinaonekana kung’ara zaidi kisiasa kuliko hata CCM. Vyama vingine hasa CCM vimekuwa vikizidi kupoteza mvuto wakati CHADEMA ikijiongezea umaarufu. Wengi wanaamini mchango wa Dk. Slaa ni mkubwa katika kukinyanyua chama hicho.

Ni mtu mwenye kupenda kujisomea zaidi na hasa kusoma taarifa mbalimbali zinazohusu nchi na mataifa mengine. Itakumbukwa Dk. Slaa ndiye aliyebaini kuwa Rais Kikwete ambaye anagombea urais kwa tiketi ya CCM alitia saini Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa mbwembwe bila kujua kuwa alichosaini sicho kilichopitishwa bungeni. Ni kiongozi anayependa kutafiti kabla ya kutoa kauli zake.

Dk Slaa alizaliwa Oktoba 29, mwaka 1948 wilayani Karatu. Alipata elimu ya msingi katika shule za Karatu na Kwermusi (Mbulu) kati ya mwaka 1958 na 1965.

Alisoma elimu ya sekondari katika Shule za Dung’unyi Seminari na Itega Seminari kati ya mwaka 1966 na 1971.

Ni kiongozi mwenye stashahada tatu pamoja na shahada ya Uzamivu (PhD). Anayo Shahada ya Uzamivu (PhD ) katika Sheria ya kanisa kutoka Chuo Kikuu cha St. Urban, Rome. Pia anastashahada ya Theolojia kutoka Kipalapala Seminari, Stashahada ya falsafa kutoka Kibosho Seminari, Stashahada ya Afya ya Macho kutoka Kituo cha Kimataifa cha Macho.

Amewahi kuwa padri wa Kanisa Katoliki kuanzia mwaka 1977 hadi 1991, akishika nafasi za kiutawala katika kanisa pia. Amepata kuandika vitabu vitatu ambavyo ni Utimilifu wa Msichana (1977), Utimilifu wa Mvulana (1977) na Expediency and exigency Liturgical Legislation (1981). Ni mzungumzaji wa Lugha nane kwa ufasaha; ambazo ni Kiswahili, Kiingereza, Kilatini, Kiitaliano, Kijerumani, Kihispania, Kireno na Kifaransa.

Jakaya Kikwete

Tofauti na wagombea wenzake, Kikwete anaweza kupimwa katika miaka mitano ya urais. Mwaka 2005, aliongoza kampeni za CCM na kushinda kwa asilimia 80.28, wabunge 206 kati ya 232, sawa na asilimia 88.79 na udiwani walishinda kwa asilimia 91.46.

Ingawa washiriki wa kampeni za Kikwete wanaamini amefanya mambo makubwa na hasa ujenzi wa miundombinu na elimu, mbele ya macho ya wananchi nje ya CCM, anaonekana ni mtu mwenye uvumilivu wa kukosolewa. Hat ahivyo, kwa sehemu nyingine uvumilivu huo unatajwa kuvuka mipaka kiasi cha kuruhusu malumbano miongoni mwa viongozi wa CCM na hata serikalini.

Kikwete pia anatajwa kupoteza dira katika vita dhidi ya ufisadi ikifafanuliwa kuwa kama angekuwa na nia ya dhati ya kupambana na ufisadi hasingeweza kuruhusu watu wanaozongwa na mazingira ya ufisadi kuteuliwa na chama chake kuwania uongozi na baadaye kuwanadi jukwaani kuwa ni watu safi huku akitambua kuwa baadhi amewafikisha mahakamani.

Hapa wanarejea mfano wa Mwalimu Julius Nyerere ambaye hakusubiri uamuzi wa Mahakama kujitenga na mafisadi. Katika vita hiyo Mwalimu alijipambanua na msemo maarufu wa “kustaafishwa kwa manufaa ya umma.” Ushahidi wa mazingira ulitosha kumpumzisha kiongozi na kama ushahidi zaidi ulijitosheleza mhusika alifikishwa kortini.

Jakaya Kikwete alizaliwa Oktoba 7, mwaka 1950 katika Kijiji cha Msoga, Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani. Alipata elimu ya msingi (darasa la kwanza hadi la nne) mwaka 1958-1961 katika Shule ya Msingi Lugoba na Shule ya Kati ya Lugoba (darasa la tano hadi la nane) mwaka 1962-1965. Mwaka 1966-1969 alisoma Shule ya Sekondari ya Kibaha, kidato cha kwanza mpaka cha nne, na mwaka 1971-1972 alisoma kidato cha tano na cha sita Shule ya Sekondari ya Tanga.

Mwaka 1972-1975 alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alihitimu Shahada ya Kwanza ya Uchumi. Alipata mafunzo ya Uofisa wa Jeshi katika Chuo cha Uongozi wa Jeshi Monduli, mwaka 1976-1977 na kupata Kamisheni ya kuwa Luteni. Baadaye mwaka 1983 – 1984 alipata mafunzo ya Ukamanda wa Kombania katika chuo hicho hicho.

Prof. Ibrahim Lipumba

Huyu ni mgombea urais wa CUF, aliyezaliwa Juni 6, 1952. Mtanzania mtaalamu mbobeaji wa uchumi, mwanasiasa na mwenyekiti wa CUF. Amehitimu shahada yake ya uzamivu katika chuo kutoka Chuo Kikuu cha Stanford na baadaye kuwa Profesa wa Uchumi. Amewahi kushika nyadhifa mbalimbali zinazohusisha taaluma, kwa mfano amekuwa profesa katika Marekani na hapa nchini. Pia amewahi kuwa mtaalamu huru wa uchumi na kupata kuwa mshauri wa uchumi kwa Serikali ya Uganda mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Amekuwa kiongozi mzoefu katika uongozi wa chama katika nafasi ya siasa kuliko wenzake. Amekuwa mwenyekiti wa CUF tangu mwaka 1995 hadi sasa. Ni mzoefu pia katika kuwania urais wa Tanzania kuliko wenzake, akianza safari hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi uliosisiwa tena miaka ya 1990. Ameanza kuwania urais tangu mwaka 1995, akishika nafasi ya tatu akipata asilimia 6.43 ya kura. Mwaka 2000 alishika nafasi ya pili akitanguliwa na Benjamin Mkapa. Katika uchaguzi huo Lipumba alipata asilimia 16.26 ya kura, akijiongezea asilimia takriban 10 ya kura ikilinganishwa na mwaka 1995.

Katika Uchaguzi wa Desemba 14, mwaka 2005 alishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 11.68 ya kura, akitanguliwa na mmoja wa washindani wake wa sasa, Jakaya Kikwete. Mbali na kujishughulisha na siasa, Lipumba ameendelea kutumikia taaluma yake kama mchumi huru, akigawa sehemu ya muda kwenye siasa na taaluma.

Profesa Lipumba anaonekana kung’ara zaidi kwenye kampeni kama msomi wa kiwango cha juu zaidi ikilinganishwa na wagombea wenzake wawili wakubwa, yaani Dk. Willibrod Slaa na Jakaya Kikwete. Kutokana na nchi kuwa na matatizo ya kiuchumi na hasa mfumuko wa bei ukiwaumiza wananchi masikini, taaluma ya Profesa Lipumba kama itatumika kigezo pekee cha kumpigia kura mgombea basi atashinda kwa kishindo.

Hata hivyo, Prof. Lipumba anaweza kuwekwa sehemu moja na Serikali ya CCM katika baadhi ya nyanja kutokana na kuwahi kufanya kazi za Serikali kama mshauri wa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi. Nyanja hizo ni pamoja na masuala ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma.

Kwa mfano, mwaka 1991 hadi 1993, Prof. Lipumba alikuwa Kamishna wa Tume ya Rais wa Kurekebisha Mashirika ya Umma. Mwaka 1992 hadi 1993, alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Bima la Taifa na mwaka huo huo, aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kuchunguza mgogoro wa menejimenti katika shirika hilo ambalo hadi sasa hali yake ni taaban.

Mwaka 1992, Prof. Lipumba pia aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya kuchunguza ufisadi katika Chama Cha Ushirika Shinyanga (SHIRECU) ambacho hakina unafuu hadi sasa na katika kampeni za mwaka huu, Kikwete ameahidi kulipa madeni ya fedha zilizoibwa bila kuahidi kuwachukulia hatua wahusika.

Kwa upande mwingine, Prof. Lipumba amewahi kuongoza, kuteuliwa au kusimamia shughuli mbalimbali za kimataifa kama mtaalamu gwiji wa uchumi. Amewahi pia kuwa mshauri wa uchumi wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni. Lakini wakati hali ikiwa hivyo kwa wagombea hao watatu wa urais, mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa inazidi kutoa picha tofauti kwa kadiri siku ya kupiga kura inavyokaribia.

Ukiacha mchuano huo wa wagombea urais, mbio za kuwania ubunge nazo ni kali kama ambavyo Paul Sarwatt anavyoripoti kutoka Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara kuwa vyama vinavyochuana vikali huko ni CCM, CHADEMA, NCCR-Mageuzi na TLP kwa mbali.

Kilimanjaro kwenye majimbo tisa CCM inachuana vikali na CHADEMA. Majimbo hayo ni Moshi Mjini, Moshi Vijijini, Vunjo, Rombo, Hai, Siha, Mwanga, Same Mashariki na Same Magharibi.

Kati ya majimbo hayo CCM inaweza kushinda kirahisi Moshi Vijijini, Mwanga na Same Magharibi, kwingine utabiri ni mgumu.

Moshi Vijijini Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyrill Chami anayepewa nafasi kubwa ya kushinda, anachuana na Anthony Komu wa CHADEMA. Mwanga; Waziri Profesa Jumanne Maghembe mambo yake si mabaya kama ilivyo kwa Naibu Waziri, Dk. David Mathayo anayegombea Same
Magharibi.

Majimbo ambayo ushindani ni mkali na lolote linaweza kutokea ni mchuano ambako mchuano ni kati ya CHADEMA, TLP na CCM. John Mrema (CHADEMA), Chrispin Meela (CCM) na Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, karibu wananguvu sawa, ingawa inaelezwa kuwa John Mrema ameanza kuwazidi maarifa wenzake.

John Mrema anapewa nafasi zaidi kutokana na mgombea wa CCM, Crispin Meela na wa TLP Agustine Mrema kulumbana mara kwa mara hasa baada ya Mrema wa TLP kuanza kumnadi mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete. Inaelezwa kuwa hali hiyo inampa nafasi nzuri John Mrema kujipambanua kwa wananchi kuwa ndiye bora.

Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo wa CHADEMA anaendelea kumburuza mpinzani wake, Justine Salakana wa CCM anayepewa nafasi finyu kushinda hasa kutokana na kukosa ushirikiano wa kutosha kutoka kwa washindani wake katika kura za maoni. Kwenye kura za maoni alishika nafasi ya tatu.

Kutoka Hai, uchunguzi unabainisha kuwa Freeman Mbowe, mwenyekiti wa CHADEMA hana upinzani mkali kutoka kwa Mbunge aliyemaliza muda wake, Fuya Kimbita wa CCM. Watani wa kisiasa jimboni humo wanasema Mbowe anasubiri kuapishwa tu.

Wagombea wa CCM kwenye Jimbo la Rombo, Basil Mramba na Aggrey Mwanri (Siha), Anne Kilango (Same Mashariki), wanakabiliwa na upinzani kutoka kwa wagombea wa CHADEMA. Joseph Selasini kuchuana na Mramba (Rombo), Naghenjwa Kaboyoka kuchuana na Kilango (Same) huku Mwanri akichuana na Mhandisi Humprey Tuni.

Kati ya majimbo hayo upepo wa kisiasa si mzuri kwa Mwanry ikidaiwa kuwa uongozi wa chama wa wilaya umeomba msaada wa uongozi wa CCM Taifa ili Jakaya Kikwete arudi kufanya kuokoa jahazi.

Katika majimbo hayo yenye ushindani wa kisiasa changamoto kubwa kwa CCM ni kufanya kampeni mbili; kwanza, kuvunja makundi yaliyozaliwa kwenye kura za Maoni. Pili, kunadi sera na kuomba kura kwa wananchi.

Lakini Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro Steven Kazi katika mahojiano ya simu na Raia mwema alidai CCM ina uhakika wa zaidi ya asilimia 90 kushinda majimbo yote hayo.

“Tuna nafasi kubwa ya kushinda katika majimbo karibu yote,vyama vya upinzani havina nguvu kama watu wanavyoelezea…..wananchi wa Kilimanjaro wanaikubali CCM na hawawezi kufanya makosa kuchagua upinzani,” alisema.

Kauli hiyo inapingwa na Katibu wa CHADEMA Basil Lema akisema chama chake kina uhakika wa kuongeza idadi ya majimbo kutoka moja la Moshi Mjini hadi majimbo matano au sita.

Katika Mkoa wa Arusha wenye majimbo saba ya Arusha Mjini, Arumeru Magharibi, Arumeru Mashariki, Monduli, Karatu, Longido na Ngorongoro hali si tofauti na Kilimanjaro.

Mkoani humo CCM ina matumaini ya kushinda majimbo ya matatu tu ambayo ni Ngorongoro, Monduli na Longido. Majimbo ya Arusha Mjini, Arumeru Magharibi, Arumeru Mashariki na
Karatu kushinda au kushindwa kutabainika baada ya kuhesabu kura.

Katika majimbo ya Ngorongoro mgombea wa CCM Sanig’o ole Telele anaweza kushinda kwa urahisi kutokana CHADEMA kuweka mgombea asiye na nguvu kisiasa Moringe ole Parkipuny, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa jimboni humo miaka ya 1990.

Jimbo la Monduli Edward Lowassa hana upinzani wa kutisha kutoka kwa Mchungaji Amani Silanga Mollel wa CHADEMA na Longido mgombea wa CCM, Michael Lekule Laizer hana upinzani wa kutisha kutoka kwa Paulina Laizer wa CHADEMA ambaye aliondoka CCM baada ya kushindwa kura za maoni za ubunge wa Viti maalumu.

Katika Arusha Mjini mgombea wa CCM Dk. Batilda Burian ambaye alishinda kwa kishindo katika kura za maoni anapambana na Godbless Lema wa CHADEMA na upepo wa kisiasa si mzuri kwake kutokana na madai kuwa baadhi ya viongozi wa CCM wilayani hawamuungi mkono.

Arumeru Magharibi mgombea wa CCM Gudluck Ole Madeye anachuana vikali na mgombea CHADEMA, Mathias ole Kisambo. Karatu, Dk.Wilbroad Lorri wa CCM anapambana na mgombea wa CHADEMA Mchungaji, Yohana Nat’se.

Mwenyekiti wa CHADEMA Karatu, Moshi Darabe alibainisha katika mahojiano na gazeti hili kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu chama chake kimepania kuweka rekodi kutokana na kupanua mtandao wake hasa baada ya kushinda viti vingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Tunatarajia kuvunja rekodi nyingine ya kushinda viti vya udiwani 10 kati ya kata 13 Jimbo la Karatu na napenda kuwatumia salamu CCM kuwa wasahau kupata chochote katika jimbo hili,” alijigamba Darabe.

Jimbo jingine ni Arumeru Mashariki ambako mgombea wa CCM ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi Jeremiah Sumari anapata upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa CHADEMA, Joshua Nasari (25).

Nasari, mhitimu wa Sosholojia na Utawala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ameibua changamoto isiyotarajiwa kutokana na kumudu kujenga hoja na kuwashawishi. Amekuwa akipata wafuasi wengi miongoni mwa vijana na wanawake jimboni humo.

Katika majimbo hayo manne sababu kubwa inayoelezwa kuwa vyama vya upinzani hasa CHADEMA kupata nguvu kunatokana na makundi ya kura za maoni hivyo. Baadhi ya wanachama wanataraji kuwapigia kura kampeni wagombea wa upinzani na wengine wakitoa michango ya fedha na vifaa vya kampeni.

Mkoa wa Manyara wenye majimbo sita ya uchaguzi CCM tayari imetwaa Jimbo la Simanjiro, mgombea Christopher ole Sendeka akipita bila kupingwa. Hata hivyo, CCM kinaweza kupoteza majimbo ya Mbulu na Babati Vijijini.

Katika Jimbo la Mbulu, Philip Marmo ambaye amekuwa mbunge jimboni humo kwa miaka 25 angependa, rekod yake hiyo ipo hatarini kuendelezwa kutokana na mgombea wa CHADEMA, Mwanasheria Boay Akonaay, kumdhibiti.

Jimboni humo hali si shwari kwa CCM kisiasa kutokana na wakazi wengi wakiwa kabila la Wairaq wanaotajwa kukusudia kufuata nyayo za jirani zao, Jimbo la Karatu. Upinzani dhidi ya Marmo ulijidhihirisha wakati wa ziara ya mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete ambaye alizomewa na baadhi ya waliohudhuria mkutano huo hali iliyosababisha polisi kupiga mabomu ya machozi kuwatanya wananchi hao.

Katika jimbo la Hanang Dk.Mary Nagu anapambana na Rose Kamili ambaye aliwahi kuwa Mke wa mgombea urais wa CHADEMA Dk.Wilbroad Slaa ingawa Nagu anapewa nafasi ya kushinda lakini chochote kinaweza kutokea na hali kama hiyo pia ipo Babati Mjini ambako Kiseryi Chambiri wa CCM anapambana na mgombea wa CHADEMA, Pauline Philipo Gekul.

Jimbo la Babati Vijijini mgombea wa CCM Jitu Soni ambaye ana asili ya Kiasia anapambana na Larent Tarra wa NCCR-Mageuzi na huenda pia CCM ikapoteza jimbo hilo kutokana na kukubalika kwa mgombea wa NCCR ambaye mwaka 2005 alishindwa kura chache sana na Damas Nakei wa CCM.

Kutoka mkoani Mara mwandishi wetu anaripoti; Majimbo ya Serengeti na Tarime ametawaliwa na siasa za ukabila na koo lakini Musoma Mjini, CCM kinakabiliwa na hali mbaya kutoka kwa wagombea wa CHADEMA.

Uchunguzi unabainisha kuwa Serengeti, mgombea wa CCM, Kebwe Stephen Kebwe anatafunwa na siasa za ukabila ambao msingi wake ni mpasuko ndani ya chama hicho wakati wa kura za maoni.

Wakati wa kura za maoni CCM kulikuwa na wagombea wanne wakitazamwa zaidi kwa makabila yao na wenzao kwenye chama hicho; Wakurya wawili ambao ni Dk. James Wanyancha aliyekuwa akitetea nafasi hiyo na Stephen Magoiga. Dk Kebwe ni kabila la Mungoreme na Daniel Muhochi ambaye ni Mwisenye.

Inadaiwa kuwa wakati wa kura hizo za maoni Dk. Kebwe alipata kura nyingi za Wangoreme ambao ni mojawapo ya makabila makubwa wilayani Serengeti huku wagombea wengine wakipata ‘namba za viatu’ katika eneo hilo.

Baada ya kura hizo za maoni inaelezwa wapinzani wa Dk Kebwe kupitia kwa wafuasi wake walieneza ‘sumu’ kuwa alishinda kutokana na ukabila kwa madai kuwa alipata kura nyingi kwa watu wa kabila lake huku wagombea wa makabila mengine wakiambulia kura chache.

Mmojawapo wa wagombea hao ambaye alikuwa na matumaini makubwa ya kushindwa inadaiwa kuwa alianza kutumia wazee wa Kimila kushawishi Wakurya na Waisenye wasimchague Dk. Kebwe kwa sababu Wangoreme hawakuwapigia kura wagombea wa makabila mengine ya Wakurya na Waisenye.

“Unajua baada ya kura za maoni mwenzetu (anamtaja) alianza kueneza sumu ya ukabila. Akawa anatumia wazee na vijana ambao ni wafuasi wake wa Kikurya na Waisenye kusema kuwa wasimpe kura Mungoreme kwasababu wakati wa kura za maoni hawakuwapa kura wagombea wa makabila mengine. Bahati mbaya baadhi ya viongozi wa chama wakati wa kura za maoni walieneza ukabila hivyo ikawa ni vigumu kurudi tena kubadili upepo,” anasema kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM wilayani Serengeti.

Anaongeza: “Hata (anamtaja tena) alipoitwa kuja kuvunja makundi ya kura za maoni kwa kumnadi Kebwe alikuwa anasimama jukwaani kumwombea kura mgombea wa urais na wagombea wengine wa CCM. Hakutaka kumtaja mgombea ubunge wetu. Pia kamati ya siasa (CCM-wilaya) ilibaini alikuwa akitusaliti zaidi badala ya kutusaidia.

“Kwa hiyo ikaamua (kamati) kuwa atolewe kwenye kampeni na hata asiwepo hapa jimboni make alikuwa anatuharibia. Vilevile kuna kiongozi mmoja (anamtaja) naye ilionekana ana kigugumizi katika kumnadi mgombea wetu vizuri kwani kwenye kura za maoni alikuwa hamuungi mkono hivyo naye tulisema akae pembeni kidogo.”

Alipoulizwa juu ya hali hiyo Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Chandi Marwa, alikiri kuwapo kwa siasa za ukabila lakini akasema ni siasa zinazozidi kudorora kwa kadiri siku zinavyokwenda kwa kuhusisha juhudi za viongozi wa chama hicho.

“Ni kweli mwanzoni hali ya ukabila ilikuwa ni mbaya sana upepo wa upinzani ulikuwa mkali sana. Lakini sasa tumejitahidi kurekebisha mambo na Kebwe anakubalika hata kwa Wakurya na Waisenye. Unajua kuangusha mtu (Wanyancha) ambaye alikuwa Naibu Waziri lazima kutatokea mtikisiko make ni mbunge wa miaka kumi na alikuwa na wafuasi wake. Lakini niseme tu sasa hivi upepo (wa kisiasa) ni mzuri tu na tutashinda bila wasiwasi,” anasema Chandi ambaye ni ndugu wa Dk. Wanyancha.

Katika hatua nyingine amemtuhumu mgombea wa CHADEMA, Marwa Ryoba ambaye ni Mkurya kuwa ndiye anatumia siasa za ukabila kama mtaji wake wa kupata kura. Hata hivyo mgombea huyo alikanusha madai hayo akisema kuwa hayo ni matatizo ya ndani ya CCM kwani hategemei kura pekee za Wakurya kupata ushindi.

“Mimi nina kura nyingi Majimoto, Kisaka, Ringw’ani, Nyambureti na huko kote ni kwa Wangoreme. Hayo ni maneno ya watu wa CCM. Wao ndiyo wamevugana huko halafu wanataka kunisingizia mimi. Nikiwa mbunge nakuwa wa watu wote wa Serengeti hivyo siwezi kubagua kwa kutumia ukabila,” anasema.

Kwa upande wake Dk. Kebwe anakiri kuwepo na kampeni za ukabila ambazo zimeenezwa zaidi na waliokuwa wapinzani wake wakati wa kura za maoni ndani ya CCM.

“Ni kweli hilo lipo lakini kwa sasa limepungua. Hivi sasa wamebaki watu wachache hasa vijana lakini kwa wazee tumejitahidi kuongea nao na wametuelewa. Naweza kusema kwa sasa hilo siyo tatizo kubwa sana na tuna uhakika wa kushinda”. Anasema.

Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa mkuu wa wilaya hiyo Edward ole Lenga amekuwa akifanya kazi ya ziada kukutana na wazee wa Kikurya na Waisenye ili kuondoa ‘fitina’ hiyo ya ukabila.

Kadhalika juzi Jumatatu Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kutoka mkoa wa Mara alilazimika kuwaita baadhi ya wazee kutoka sehemu mbalimbali za jimbo hilo ili kuweka mambo sawa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi Jumapili ijayo.

Wakati jimbo la Serengeti likiwa limetawaliwa na ukabila, katika jimbo la Tarime, nguvu ya koo ndiyo imetawala kutokana na wagombea wote wenye nguvu kutokea koo moja.

Wagombea hao, Charles Mwera (CUF) ambaye ni mbunge aliyemaliza muda wake, Nyambari Nyangwine (CCM) na Mwita Waitara (CHADEMA) wanatoka koo ya Wairege (Ingwe) ambayo ndiyo ina idadi kubwa ya watu kuliko koo nyingine. Koo ya Wairege ina kata 9 kati ya kata 30 za jimbo hilo lenye zaidi ya koo 11.

Mgombea mwingine mwenye nguvu ni Peter Wangwe (NCCR-Mageuzi) ambaye ni mdogo wake marehemu Chacha Wangwe aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya kupata ajali na kufariki mwaka juzi. Huyu anatoka koo ya Watimbaru (Inchage).

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kuwa historia ya uchaguzi katika jimbo hilo huegemea zaidi katika koo hivyo kutokana na wagombea watatu wenye nguvu kutoka koo moja ya Wairege kunafanya mshindi kutotabirika mpaka sasa.

Wakazi kadhaa waliozungumza na Raia Mwema katika jimbo hilo wanasema kuwa mshindi atategemea zaidi anavyokubalika katika koo zingine kwani katika koo ya Wairege wote watatu watagawana kura.

Aidha uamuzi wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Mwera kuhamia CUF kutoka CHADEMA baada ya kushindwa na Waitara kwenye kura za maoni na hatua ya mdogo wake marehemu Chacha Wangwe kugombea kwa tiketi ya NCCR Mageuzi kunaelezwa kuwa kutafanya wapinzani kugawana kura hivyo kuinufaisha CCM.

“Ninavyoona wapinzani wanaweza kugawana kura halafu ukashangaa CCM inashinda make mwaka huu wote wenye nguvu wanatoka koo moja halafu kuna huyu wa NCCR naye anakubali kwenye koo yao na zile zingine ambazo siyo Wairege. Kule kwa Wairege Mwera anakubalika na Nyangwine lakini pia huyu wa CHADEMA naye ana watu make ndiyo chama tawala hapa (Tarime)”. Anasema mzee Mwita Chacha mkazi wa Nyamongo.

Anaongeza: “Huyu wa CCM anaweza kupata tabu kwenye koo ya Wanyabasi, Watimbaru, Wakira, Wanyachari, Wanyari, Wasweta na Walunyaga make kwenye kura za maoni alimshinda (Christopher) Kangoye ambaye ni Mnyabasi na wao wanadai alimfanyia hujuma hivyo wanaweza kupigia upinzani. Habari za uhakika kutoka ndani ya CCM wilayani Tarime zinasema kuwa Kangoye ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza ameitwa mara kadhaa kwenda kusaidia kuondoa mpasuko huo wa koo.

Mwera ambaye alikuwa pia diwani kata ya Nyanungu na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo bado ana ushawishi mkubwa jimboni humo na inadaiwa kuwa kama ilivyokuwa kwa marehemu Chacha Wangwe tofauti zake kimtizamo na mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA Freeman Mbowe ndiyo zilisababisha asiteuliwe kugombea kwa tiketi ya chama hicho hata kama alikuwa mshindi wa pili. Mwera pia anagombea udiwani wa kata ya Itiryo baada ya kata ya Nyanungu kugawanywa.

Hali ya kukosekana kwa mgombea mwenye nguvu kuliko wengine katika jimbo hilo pengine inaweza kuonekana kutokana na kukosekana na ule msisimko wa kisiasa ambao unakuwepo nyakati za uchaguzi.

Mgombea wa CHADEMA, Waitara anakiri kuwa uchaguzi huo umetawaliwa na nguvu ya koo huku akimtuhumu mgombea wa NCCR- Mageuzi kwa kutumia njia hiyo ili kujipatia kura.

“Tuna uhakika wa kushinda ingawa kuna hili tatizo la koo. Na wanaoneza haya maneno ya koo ni NCCR Mageuzi. Anasema eti kwavile wagombea wengine wote ni Wairege, koo zingine zimchague yeye Mtimbaru” anasema. Hatahivyo Wangwe hakuweza kupatikana kujibu tuhuma hizo.

Pengine katika mkoa wa Mara zile zinazoitwa siasa za Tarime hivi sasa zimehamia katika jimbo la Musoma Mjini ambako kuna mchuano mkali kati ya mbunge aliyemaliza muda wake Vedastus Mathayo Manyinyi na mgombea wa CHADEMA Vincent Kiboko Nyerere. Vincent ni mtoto wa Josephat Kiboko Nyerere ambaye ni mdogo wake Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Mpasuko mkubwa wa kisiasa ndani ya CCM mkoa wa Mara ndio mtaji mkubwa wa mgombea huyo wa CHADEMA huku kukiwa na taarifa kuwa anaungwa mkono na viongozi wandamizi wa CCM mkoani humo.

Siasa za makundi mkoani humo zinaonekana kumwelemea Mathayo ambaye baadhi ya viongozi wa chama hicho wanamtuhumu kwa ‘kukivuruga’ chama kwa nguvu yake ya pesa.

Inaelezwa kuwa viongozi waandamizi wa CCM mkoani humo hawajawahi kuhudhuria kampeni za kumnadi mgombea huyo mpaka pale alipofika mgombea urais Jakaya Kikwete na mgombea mwenza Dk Mohamed Gharibu Bilal na kwamba na hata walipopata fursa ya kuzungumza walitumia falsafa ya chama hicho ya mafiga matatu kwa kukwepa kutaja jina la Mathayo.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara Makongoro Nyerere ambaye ni kaka yake mgombea wa CHADEMA ameonekana katika baadhi ya majimbo nje ya ya mkoa huo akiwanadi wagombea wa chama chake lakini amekuwa adimu kwenye mikutano ya kampeni ya Mathayo.

Ni katika jimbo hili ambako ulinzi wa jeshi la polisi umeimarishwa katika mikutano yote ya kampeni na hata katika mitaa ya katikati ya mji kama ilivyokuwa kwenye chaguzi za Tarime na hivi karibuni wafuasi wa vyama hivyo vya CHADEMA na CCM walijeruhiana katika vurugu.

Chanzo: www.raiamwema.co.tz

Thursday, October 28, 2010

Kataeni kushawishiwa ama kuhusishwa katika fujo au vurugu - IGP Mwema

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini(IGP), Said Mwema amewaomba wananchi kuwa na ushirikiano katika kukataa kushawishiwa ama kuhusishwa katika uvumi, fujo au vurugu zozote zinazoweza kuingiza nchi kwenye machafuko yasiyo ya maana yoyote.

Aidha Mkuu huyo , amesema kuwa amani na usalama na utulivu hapa nchini vitadumishwa wakati wote kabla na baada ya uchaguzi, kwa kuhakikisha kwamba sheria , kanuni na taratibu za nchi zinafuatwa ipasavyo.

“Tukumbuke kwamba vitendo vyovyote vya uvunjwaji wa sheria, kabla na baada ya uchaguzi ni uhalifu.Sheria haina udhuru, inachukua mkondo wake mara moja endapo ukiukwaji umefanyika. Hivyo kutii sheria na taratibu za uchaguzi ni wajibu wa kila mpiga kura na kila mwananchi,” alisema Mwema.

Aliongeza kuwa baada ya kura kupigwa na zoezi hilo kufungwa rasmi, hatua inayofuata ni kuzichambua na kuzihesabu ili kupata matokeo, hivyo huo ndo wakati wananchi wanatakiwa kuwa na subira, kwa sababu zoezi hilo ni muhimu na linapaswa kuendeshwa kwa umakini wa hali ya juu ili, haki itendeke na kuepusha malalamiko.

Mkuu huyo alisema baada ya matokeo kutangazwa ni muhimu kutambua kwamba aliyeshinda ndiye aliyepigiwa kura nyingi na watu wengi.

“Wote tunawajibu wa kumkubali , kumtambua na kushirikiana naye ili kumsaidia kutimiza wajibu wake kama kiongozi wa watu wote,” alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarouk Abdulwakil aliwataka wananchi wote bila kujali itikadi au udini kuendelea kuwa na msukumo wa utaifa na kuacha maslahi binafsi ili amani, usalama na utulivu vidumu kabla ya baada ya uchaguzi.

Alisema wizara yake inawahakikishia wananchi kwamba nchi itakuwa katika hali ya amani, usalama na utulivu wakati wote huku, hivyo alisisitiza ushirikiano kutoka kwa wananchi.

Wednesday, October 27, 2010

‘Kubalini matokeo, msiporidhika fuateni sheria'

SERIKALI kupitia vikosi vya ulinzi na usalama, imetoa tahadhari kwa waliojipanga kuyakataa matokeo ya uchaguzi, wajiepushe na uvunjifu wa amani na kama hawatoridhika na matokeo hayo, wadai haki yao kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo.

Aidha, ili kuwahakikishia amani na utulivu Watanzania katika siku chache zilizobakia za kampeni na baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi, Jeshi la Polisi limetangaza kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Magereza na Mgambo.

Uthibitisho huo wa utulivu na amani wakati wa uchaguzi, umetolewa jana kwa nyakati tofauti na Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema na viongozi wengine wa serikali.

“Endapo matokeo yaliyotangazwa hayatokidhi matarajio ya mtu au kikundi chochote, ni vyema utaratibu wa kisheria ukafuatwa pasipo uvunjifu wa sheria,” alisema Mwema.

Alisema, ingawa wajibu wa usalama na amani pia ni wa wananchi, Polisi imejipanga kuhakikisha mikutano ya kampeni iliyobakia inamalizika kwa usalama, utaratibu wa kupiga kura unafanyika kwa amani na utulivu na vifaa vya kupigia kura vinalindwa ili visiibiwe, visitekwe wala kughushiwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil, alisema mchakato wa uchaguzi umekuwa shwari isipokuwa kuna matukio kadhaa yaliyotia dosari.

Aliyataja matukio hayo kuwa ni kuchana mabango ya wagombea, lugha chafu na wanachama wa vyama tofauti kushambuliana na kutoa taarifa za uvumi kwa njia ya simu na mtandao.
Masha ambaye alitoa taarifa yake mkoani Mwanza alisema: Wananchi wote wa Tanzania watapiga kura kwa amani na utulivu Oktoba 31 na wale watakaoleta vurugu, neno langu ni moja kwao ya kuwa wawe tayari kuvuna walichokipanda.”

Alisema, Serikali inawashukuru Watanzania kwa kuonesha ukomavu wa kisiasa katika kampeni na kuhakikisha hakuna mtu aliyepoteza maisha hadi wakati huu.

“Lakini kule Shinyanga mwanachama mmoja wa CCM kwa sababu tu alikutwa ameweka bango la CCM tayari ameuawa hivi tunaelekea wap?”

Alihoji na kuvitaka vyama vya siasa viongozi wao na wananchi kwa ujumla kuheshimu taratibu za uchaguzi.

Alisema serikali haimzuii mtu yeyote kufanya ushabiki ndani ya chama anachokipenda, lakini akasisitiza kuwa ushabiki huo sharti uzingatie sheria na utaratibu.

Rais Kikwete atukanwa 'live'

MALALAMIKO ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi ya kampeni za mgombea urais wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa kuwa zimejaa matusi, yalidhihiri jana pale kampeni za mgombea huyo zilipotumika kumtukana Rais Jakaya Kikwete na mama yake mzazi.

Kabla ya kuanza kumtukana Rais wa nchi ambaye pia ni mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Slaa mwenyewe alitamba kuwa katika viwanja hivyo vya Mwembeyanga, Temeke ndipo alipotoa tuhuma dhidi ya viongozi wengine bila kushitakiwa wala kukamatwa.

Dk. Slaa ambaye alianza hotuba yake kwa kutoa maneno machafu dhidi ya CCM na viongozi wake na kutumia muda kidogo kuelezea hoja za Ilani ya uchaguzi ya chama chake na kujibu hoja za wapinzani wake, kabla ya kumaliza alitoa nafasi kwa mgombea ubunge wa Temeke kuonesha umahiri wa kujenga hoja.

Mbali na kumpa nafasi mgombea huyo aoneshe umahiri huo kwa dakika mbili ili apimwe kama anaweza kutumia dakika tatu wanazopewa wabunge kujenga hoja bungeni, Dk. Slaa aliwaomba wananchi wampigie kura mgombea huyo, kwa kuwa kupitia wagombea wa ubunge wa Chadema akiwemo huyo, ndipo anapotarajiwa kumpata Waziri Mkuu na mawaziri wengine wasiozidi 20.

Hata hivyo mgombea huyo, Dickson Amos, alitumia nafasi hiyo kumtukana matusi ya kumdhalilisha Rais Kikwete na mama yake mzazi na kusababisha matangazo ya moja kwa moja ya TBC1 kutoka katika viwanja hivyo, kukatishwa ghafla ili kustahi ustaarabu wa jamii ya kitanzania.

Matusi hayo ambayo ni aibu kuyaandika, yalitolewa katika mkutano wa hadhara na uliokuwa ukisikilizwa na wasikilizaji mbalimbali wa TBC 1 nchi nzima.

Katika muda mfupi alioutumia kujibu hoja zilizoelekezwa kwake na wapinzani wake kisiasa, Dk. Slaa alisema hahitaji shahada ya uzamivu kwa ajili ya kusimamia masuala ya uchumi wa nchi.

Alikiri kweli yeye ni mbumbumbu wa uchumi kwa sababu amesomea sheria, lakini uchumi aliosoma mwaka 1972 unatosha kujua hali ya Mtanzania na jinsi ya kumsaidia.

Alikuwa akimjibu Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala aliyesema mgombea huyo hajui mambo ya uchumi na kumtaka aache kuyajadili.

Aliwataka Watanzania kumpatia wabunge wengi wa Chadema ambao watafuta sheria iliyopandisha bei ya bati na ya saruji na kudai kuwa Watanzania wanalipa kodi nyingi katika bidhaa zao kuliko hata ilivyo kwa nchi za Afrika Mashariki.

“Kama Dk. Kamala haelewi ninachosema akasome gazeti la East Afrika ukurasa wa tatu, ila nina mashaka kama anajua Kiingereza vizuri… na afahamu kuwa Dk. Slaa ni rais wa Watanzania na sio wa Afrika Mashariki,” alisema na kuongeza kuwa yuko tayari kufuta mikataba yote inayowaumiza wananchi.

Kuhusu elimu, alirudia ahadi ya Ilani ya chama chake kuwa akiingia madarakani elimu itakuwa bure kwa kuwa sasa kuna matabaka matatu katika elimu ambayo anataka kuyaondoa.

Alitaja matabaka hayo kuwa ni ya watu wenye uwezo wa kupeleka watoto wao shule za kimataifa, wengine shule za kata ambazo alidai hazina vitabu wala walimu na wengine ni wale ambao wazazi wanakosa hata kufikia kuwapeleka shule.

Akiwa katika viwanja vya Manzese, alitoa nafasi kwa mchumba wake ambaye ni mke wa mtu, Josephine Mushumbusi ambaye alisema kama urais wa Dk. Slaa ni wa familia, yeye angekuwa wa kwanza kumwambia mchumba wake akae nyumbani.

Alisema amezunguka naye nchi nzima na mambo aliyoyaona ya umasikini wa Watanzania, yamemfanya Dk. Slaa hata wakati mwingine kukosa usingizi na yeye kama mchumba amekuwa akimtia moyo.

“Nitahakikikisha Dk. Slaa analala vizuri, na ninamwahidi kumtunza ili aweze kutekeleza majukumu yake vizuri,” alisema Josephine.

Friday, October 15, 2010

Kikwete:Wakataeni wanasiasa wachochezi

KAULI za umwagaji damu katika majukwaa ya siasa nchini ndizo zitakazolazimisha vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuingilia kati kudumisha amani kwa kuwa ni kazi yao.

Sambamba na hilo, Watanzania wametakiwa kuwakataa wanasiasa wanaochochea umwagaji damu na ubaguzi wa dini, kabila na uchochezi wa chuki.

“Wanasiasa kama wanataka kuzuia vyombo vya ulinzi kuingilia ni kuacha kuzungumzia kumwaga damu, tuwaache wafanye kazi yao tusiwaingilie na sisi tuzungumzie barabara, madaraja, maji”.

Hiyo ni kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru zilizofanyika katika uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma jana, sambamba na maadhimisho ya miaka 11 tangu kifo cha Mwalimu Julius Nyerere.

Aliwataka Watanzania kukemea na kukataa wanasiasa wanaochochea na kupandikiza chuki, kugawa watu kwa udini, ukabila, rangi, jinsia na wanakotoka watu.

“Tuwakemee wanaopandikiza chuki, kuna watu sasa wanatuma ujumbe mfupi wa simu za mkononi wa hovyo, matusi na kuwabagua watu kwa dini, wanasiasa wanataka tuchaguliwe kwa umwagaji damu wakati katika uongozi wa Nyerere, hakukuwa na mgogoro wa Wahaya na Wachaga wala Wakristo na Waislamu.

“Lakini sasa kuna wanasiasa wanaotaka uongozi kwa chuki na wana uchu wa madaraka hawajali, potelea mbali hata damu ikimwagika wao wanataka uongozi … tuwaambieni mzee tunakuheshimu sana, lakini haya unayotwambia hatutaki …tumeona ya Burundi na Rwanda na hapa Kigoma mna uzoefu nayo, hivi kwetu kukitokea mauaji hata hawa wa Kasulu hawatoshi Burundi kutokana na ukubwa wa nchi yetu,” alisisitiza.

Alisema, Watanzania kwa asili si watu wenye matatizo, lakini viongozi wa kisiasa wakiwachochea kufanya fujo na kuwabagua, nao watafanya na kuwataka kuwa makini katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi, ambapo wanasiasa wako tayari kufanya lolote ili kupata uongozi.

Katika maadhimisho hayo yaliyopambwa na nyimbo na halaiki, Rais Kikwete alisema Serikali imejipanga kufanya kila iwezalo ili nchi iwe na amani na uchaguzi ufanyike kwa njia ya usalama na amani.

“Nimetoka mikoa ya Kusini kuna mgombea mmoja anasema watoto wakilalia vyandarua wanakufa … ni uongo wa mchana, hivi sisi wanasiasa hatuwezi kuomba kura bila uongo?
Tunatisha watu bure, hii si siasa bali ni ‘sihasa’…”, alisema Rais Kikwete ambaye pia ni mgombea urais kwa tiketi ya CCM.

Akizungumzia mipango ya Serikali kutokomeza malaria, alisema tayari mkoa wa Kagera umemaliza kupuliza dawa nyumba kwa nyumba na mwanzoni mwa mwezi huu, wameanza mkoani Mara, ambako lengo ni kupulizia dawa za kuua malaria katika mikoa yote.

Alisema Serikali ina mpango wa kupulizia dawa kwenye madimbwi ya maji ili kuua viluwiluwi na ifikapo mwaka 2015 malaria iwe imetokomezwa nchini.

Kuhusu tatizo la maji Kigoma, alisema kwa sasa kunajengwa matangi ya maji mapya yenye uwezo wa kuhifadhi maji meta za ujazo 16,000 wakati yaliyopo sasa yanahifadhi meta za ujazo 4,000.

Alisema kutawekwa mabomba mapya na mitandao mipya ya maji. Katika kuwezesha vijana, alisema katika halmashauri, kutaajiriwa maofisa vijana watakaokuwa na kazi ya kuwaendeleza vijana na kusimamia shughuli za kuwawezesha vijana kujiendeleza kiuchumi.

Wednesday, October 13, 2010

Waangalizi wa EU wasema hawatabeba chama chochote

Timu ya waangalizi 70 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) imewasili nchini kwa ajili ya kuangalia Uchaguzi Mkuu na kusema kuwa haitakipendelea chama chochote.

Kiongozi wa waangalizi hao, David Martin, alisema hawatarajii kupendelea chama chochote kwa kuwa sio moja ya kazi iliyowaleta.

Alisema wakiwa hapa nchini watatathmini kwa kina mchakato wa kampeni zinazoendelea na kuangalia kiasi gani uchaguzi huo unavyoheshimu kanuni za kimataifa.

Aidha, alisema wataangalia namna gani haki za kisiasa zinavyoheshimiwa na matamko mbalimbali ya kimataifa yaliyoridhiwa na serikali ya Tanzania ili mwishoni waweze kuandika ripoti yao na kuikabidhi kwa serikali ya Tanzania.

Martin alisema EU imewahi kushiriki katika uangalizi wa uchaguzi zaidi ya mara 80 katika nchi 50 duniani na kwamba wanao watalaamu wa kutosha ambao hawaegemei upande wowote.

Aliongeza kuwa wakiwa hapa nchini watakuwa wanawasiliana na wagombea wote, vyama vya siasa, mabalozi waliopo nchini na wapiga kura.

Alifafanua kuwa watatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia makubaliano kati yao na Tume ya Uchaguzi za Zanzibar (Zec) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

Chini ya makubaliano hayo, waangalizi hao watakuwa na uhuru wa kwenda mahali popote na kumhoji mtu yeyote wanayemtaka bila masharti.

Uhuru mwingine watakaokuwa nao ni kuzungumza na vyombo vyote vinayohusika na uchaguzi ikiwemo kuruhusiwa kuingia bila masharti kwenye vituo vya kuhesabia kura.

Alidha, Martin alisema watakuwa na haki ya kupata taarifa zozote kabla na baada ya kufanyika kwa uchaguzi.

Kuhusu vyombo vya usalama kutoa tamko dhidi ya wanasiasa wanaotaka kuvuruga amani lililotolewa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi, Martin alisema hana maoni yoyote juu ya suala hilo.

Akijibu madai ya kuwepo karatasi za kutoka nchi moja ya Asia ambazo inadaiwa mtu akipiga kura inabadilika na kuandika jana la mtu mwingine, alisema madai hayo hajawahi kuyasikia na kuongeza kuwa kama yalikuwepo, mwaka huu halitatokea kwa kuwa safari hii karatasi za uchaguzi zimetengezwa kwa ubora nchini Uingereza.

Udasa yaandaa mhadhara wa Nyerere

Jumuiya ya wanataalima ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(Udasa) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, wameandaa mhadhara utakaofanyika kesho kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka 11 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Mhadhara huo utafanyika chuoni hapo, katika ukumbi namba moja wa Nyerere.

Dk. Kitila Mkumbo, Makamu Mwenyekiti wa Udasa, alisema jana kuwa mada kuu itakayojadiliwa ni ”Mawazo ya Nyerere katika suala la uongozi”.

Aidha, Dk. Mkumbo alieleza kwamba jopo la watu wanne limeandaliwa kuzungumzia maeneo mbalimbali yanayoendana na mada hiyo, ambao ni Jenerali Ulimwengu,Dk. Adolf Mkenda, Joseph Butiku na Dk. Azaveli Lwaitama

Wakataohudhuria ni mabalozi toka katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Afrika kwa ujumla, wanataaluma na wadau toka katika nyanja tofauti.

Nipeni urais niwakomeshe wauaji wa maalbino, asema Prof. Lipumba

Mgombea urais kupitia Chama Cha Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kuwa akishaguliwa atahakikisha anachukua hatua madhubuti kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).

Mgombea huyo pia ameiponda serikali kwa kujenga vituo maalum kwa ajili ya kuhifadhi watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na kuahidi kuvifuta iwapo atachaguliwa.

“Nitahakikisha pia kwamba ninaondoa utaratibu wa sasa wa serikali kutenga maeneo maalum kwa ajili ya hifadhi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi kwa sababu siyo utaratibu mzuri wa kuwawekea kambi,” alisema jijini Mwanza wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika eneo la Pasiansi.

Profesa Lipumba alisema kuwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini yanashamiri kutokana na tabia ya baadhi ya vigogo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendekeza vitendo vya ushirikina.

Alisema vitendo hivyo visingeshamiri iwapo viongozi wa serikali ya CCM wangelikuwa na uchungu.

Lipumba alisema mfano unaodhihirisha serikali ya CCM kutokuwa makini ni kuwanadi katika majukwaa watuhumiwa wa ufisadi kwamba ni watu wasafi.

Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, akichaguliwa kuwa Rais atahakikisha watuhumiwa wa mauaji dhidi ya watu wenye ulemevu wa ngozi nchini wanakamatwa haraka na kesi zao kutolewa hukumu mapema.

Aidha, aliahidi kuwa atahakikisha kwamba kila mwanafunzi anakuwa na kompyuta moja, kuanzia elimu ya msingi. “Mkinichagua mimi nitahakikisha kwamba Tanzania inajiunga na utaratibu wa Kimataifa wa kila mwanafunzi kuwa na kompyuta moja ya kujifunzia,” alisema Profesa Lipumba.

Aliahidi pia kwamba akiwa Rais, atahakikisha kuwa anafumua mikataba yote ya madini pamoja na kupitia upya misamaha ya kodi kwa wafanyabiashara.

Profesa Lipumba jana aliendelea na kampeni katika Jimbo la Magu.


CHANZO: NIPASHE

Tuesday, October 12, 2010

Maalim Seif atoa tuhuma nzito

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimedai kuwapo viongozi waandamizi wa siasa, wanaopingana na maridhiano na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wenye malengo ya kutaka kuvuruga uchaguzi.

Hayo yamesemwa na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho, ambaye pia ni Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, katika mikutano ya kampeni kisiwani hapa mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Inasikitisha, kwamba tunakazania kudumisha amani, umoja na maridhiano, lakini kuna baadhi ya viongozi wanaofanya njama za chinichini kujaribu kuvuruga lengo hili na kuturudisha kwenye mgogoro.

Wanajaribu kujipenyeza katika mchakato wa uchaguzi na wapiga kura,” alisema Maalim Seif katika mikutano ya kampeni Pemba.

Alikwepa kuwataja majina au vyama vyao, lakini akawataka Wazanzibari kuwapuuza akisema wamekuwa wakikutana usiku kupanga mipango yao hiyo michafu, na kuhimiza amani na utulivu vilindwe.

Katika mikutano ya kampeni aliyoifanya katika uwanja wa Gombani, jimbo la Chake Chake na Pujini jimboni Chonga, Ijumaa na Jumamosi, Maalim Seif aliahidi kulinda maridhiano ya kisiasa akisema ni amali muhimu kwa maendeleo.

Aliwaomba wapiga kura kumpa nafasi ya kuwa rais wa Zanzibar, ili aiendeleze Zanzibar ikiwa ni pamoja na suala linalosubiriwa la uchimbaji wa mafuta na gesi asilia visiwani hapa.

Alifanya ziara fupi katika kijiji cha Tundaua ambako utafiti wa rasilimali hiyo ulifanyika mwaka 1961. Aliahidi kuendeleza kilimo na uvuvi ili kutengeneza ajira na kukomesha uzembe visiwani.

“Tunataka kuzalisha chakula cha kutosha; hii inawezekana kwa kuwa na mipango inayotekelezeka na kuwa na uongozi wenye ari.

Mimi ndiye ninayestahili kuongoza Zanzibar kupita katika kipindi hiki cha changamoto za kijamii, kiuchumi na kisiasa,” alisema.

Mgombea uwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, alisisitiza kwamba chama chake kitashirikiana na Serikali ya Muungano kutatua matatizo yaliyopo ya Muungano.

“Hakuna anayefikiria kuvunja Muungano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara. Hakuna shaka kwamba Muungano ni muhimu kwa maendeleo yetu,” Jussa alisema hayo katika mkutano wa hadhara Kikwajuni.

Aliwataka wanachama wa CCM kuchagua wagombea wa CUF na Seif kwa ajili ya maendeleo yao.

Naye Oscar Mbuza anaripoti kwamba Mkuu wa Mkoa katika Serikali ya Kwanza ya Rais Abeid Amaan Karume, Abdulazak Simai ‘Mzee Kwacha’, amechafua hali ya hewa kisiasa visiwani hapa.

Mzee Kwacha alifanya hivyo juzi baada ya kumtaka mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, kuwa makini na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa atakayoiunda.

Mzee Kwacha aliyepewa nafasi ya kumkaribisha Dk. Shein kwa niaba ya wazee wa mji wa Paje, mkoa wa Kusini Unguja, kabla ya mgombea huyo kuhutubia mkutano wa hadhara, aliwaacha midomo wazi maelfu ya watu waliohudhuria mkutano huo baada ya kumshambulia kwa maneno makali, Maalim Seif.

Huku watu wengi wakishikwa na butwaa kutokana na aina hiyo ya siasa kutoonekana kwenye kampeni za uchaguzi wa Zanzibar mwaka huu, Mzee Kwacha alimtaka Dk. Shein kuwa makini na Maalim Seif, akidai ataiuza Zanzibar akiingia madarakani.

Maneno ya mzee huyo, yalimfanya Dk. Shein aliyekuwa anamsikiliza kwa makini kuweka mikono kichwani akiwa kama vile haamini kusikia mzee huyo akitoa maneno hayo makali hadharani.

“Huyu tulikuwa naye ndani ya CCM na aliwahi kushika nyadhifa za juu sana, kwanza tulimpa uwaziri wa utalii, halafu tukamfanya kuwa Waziri Kiongozi, lakini hakutosheka ….

“Seif alitusaliti, tunakuomba uwe naye makini, sisi wananchi wa Zanzibar tutasimama kidete kuhakikisha hapati nafasi hata kidogo ya kuiyumbisha Serikali yako,” alisema Mzee Kwacha.

“Napenda kuwaambia hawa vijana wasiojua historia ya nchi yetu, Mzee Karume (Abeid), na viongozi wengine nikiwamo mimi tulipigania kuikomboa nchi hii, hatuwezi kukubali kuona watu wanataka kuirudisha Zanzibar kwenye Ukoloni tena.

“Angalia hapa Paje, leo hii maisha mazuri nyumba zinapendeza na barabara zinaboreshwa,” alisema.

Kauli ya mzee huyo iliwafanya maelfu ya wana CCM katika mkutano huo kulipuka kwa shangwe, lakini viongozi wakionekana kutopendezwa na kauli hiyo, katika kile
kilichotafsiriwa kuwa ni kutokana na maridhiano ya kisiasa baina ya CCM na CUF, ambayo yanaifanya Zanzibar kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, baada ya uchaguzi mkuu ujao.

Kutokana na maridhiano hayo, siasa za Zanzibar zimebadilika sana ikilinganishwa na miaka ya nyuma na maneno ya kashfa hayapewi nafasi katika mikutano ya kampeni ya CCM na CUF, badala yake vijembe vya kawaida vya siasa ndivyo vinavyotamba hivi sasa.

Monday, October 11, 2010

Synovate:Watanzania wanamuamini Kikwete

UTAFITI wa Kampuni ya Synovate uliodaiwa kuonesha mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa akiongoza, umetolewa rasmi jana ukiwa na tafsiri tofauti kuhusu sifa za uongozi kwa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, aliyeibuka mshindi katika kura hizo za maoni.

Sifa hizo za uongozi, ikiwemo ya kuaminika, ametajwa kuwa nayo na idadi ya Watanzania wanaompa sifa hiyo kuwa kubwa (84%) kuzidi matarajio ya tathimini ya awali ya ushindi wake kwa mujibu wa chama chake cha CCM ya asilimia 80 na sifa nyingine ya utendaji bora, akipewa na Watanzania wanaokaribia matarajio hayo (78%).

Hata hivyo, wakati Kikwete akipewa sifa hizo na idadi kubwa ya Watanzania waliohojiwa na kampuni hiyo kati ya Septemba 5 hadi 16, Watanzania hao walipoulizwa watamchagua nani katika uchaguzi wa Oktoba 31, awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, asilimia 61 tu ndio walisema watamchagua mgombea huyo wa CCM.

Lakini kati ya walioulizwa watampigia nani kura katika uchaguzi ujao, asilimia 13 ya waliohojiwa katika mikoa yote nchini, hawakupenda kutoa maoni yao kwa madai kuwa ni siri yao.

Meneja wa kampuni hiyo nchini, Aggrey Oriwo alipokuwa akitoa matokeo ya utafiti huo alisema endapo waliokataa kujibu swali hilo, wangepiga kura katika utafiti huo, asilimia 70 wangempigia Rais Kikwete, Dk Slaa asilimia 18 na Profesa Lipumba pamoja na vyama vingine vya siasa wangepata asilimia sita.

Oriwo mbali na kusisitiza kuwa kampuni yake haitambui matokeo yaliyotolewa na Chadema yakimpa ushindi Dk. Slaa, lakini pia alitetea utafiti wao kuwa unatoa matokeo yenye uhakika wa asilimia 95.

Utafiti mwingine wa Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pia ulitoa matokeo yanayoonesha sifa za ushindi wa mgombea huyo wa CCM.

Katika utafiti huo ambao umeshapingwa na CCM kuwa umewapunja ushindi wao na kupingwa pia na vyama mbalimbali vya upinzani kuwa umeipendelea CCM, ushindi wa Rais Kikwete ulionesha sura mbili tofauti.

Katika sura ya kwanza ya ushindi huo, Watanzania waliulizwa kama uchaguzi ungefanyika siku utafiti huo ulipofanyika, wangemchagua mgombea wa chama gani katika nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, asilimia 71 ya wahojiwa wakasema mgombea wa CCM.

Lakini wananchi hao katika utafiti huo wa Redet, walipotakiwa kutaja jina la mtu mmoja ambaye wangependa kumchagua ili awe Rais wa Tanzania, asilimia 68 walimtaja Rais Kikwete.

Matokeo hayo yalionesha tofauti ya ushindi wa Rais Kikwete kama mtu Watanzania wanayemtaka awe rais, na mgombea wa chama wanayemtaka kuwa rais.

Katika utafiti wa Synovate katika sifa ya ushindi wa kiongozi ya kuaminiwa na wananchi, Watanzania waliohojiwa na kampuni hiyo, waeleze ni kwa kiasi gani wana imani na taasisi au watu waliotajiwa, Rais Kikwete aliibuka na ushindi wa asilimia 84, huku Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Nchikavu na Majini (Sumatra) ikishika nafasi ya mwisho kwa kuaminiwa ya asilimia 44.

Nafasi ya pili ya mtu, au taasisi inayoaminiwa na Watanzania wengi imeshikwa na Baraza la Mawaziri (68%) na kufuatiwa na taasisi za fedha (52%), taasisi za huduma ya afya na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) zilizofungana kwa kupata asilimia 50.

Taasisi au mtu waliotajwa katika sifa ya kuaminiwa na Watanzania ni vyama vya upinzani (48), Shirikisho la Wafanyakazi (Tucta) na Mahakama zilizofungana kwa kupata asilimia 47, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) iliyoshika nafasi ya saba kwa asilimia 46 ya kuaminiwa huku Jeshi la Polisi likishika nafasi karibu ya mwisho kwa kupata asilimia 45.

Katika sifa ya utendaji bora, Watanzania hao 2,000 walipoulizwa, unatathimini vipi utendaji na viongozi na taasisi walizotajiwa, asilimia 78 walisema utendaji wa Rais Kikwete ni bora.

Makamu wa Rais na mgombea wa CCM wa urais Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein alipata asilimia 77 ya utendaji bora huku Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), likishika mkia kwa kuambulia asilimia 30.

Aliyeshika nafasi ya tatu katika utendaji bora wa mtu au taasisi ni Spika wa Bunge na mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Urambo Mashariki, Samuel Sitta na kufuatiwa na vyombo vya habari (72%), wanamuziki wa Tanzania (59%), Baraza la Mawaziri (58%).

Wengine katika ubora wa utendaji ni asasi zisizokuwa za kiserikali (57%), watumishi wa umma (41%), Tucta asilimia 40, taasisi za afya (39%), Sumatra iliyopata asilimia 37, Jeshi la Polisi likishika nafasi karibu na mwisho katika utendaji bora kwa kupata 33%.

Kuhusu mtu ambaye Watanzania watampigia kuwa rais Oktoba 31, Rais Kikwete aliongoza kwa kupata asilimia 61 na kufuatiwa kwa mbali na mgombea urais wa Chadema, Dk. Slaa (16%), mgombea urais wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba aliambulia asilimia 5 tu.

Alisema katika dodoso inayohoji juu ya utendaji wa serikali inayomaliza muda wake ya awamu ya nne, asilimia 50 ya waliohojiwa walionesha kuridhika na utendaji wa serikali hiyo huku asilimia 24 wakionesha kutoridhika na wengi wa wahojiwa walionesha kuridhika ni kutoka vijijini.

Oriwo alisema katika dodoso ya utendaji wa serikali katika kutoa huduma za jamii, asilimia 83 hawakuridhika na utolewaji wa ajira huku asilimia 72 wakionesha kutoridhika na bei ya vyakula ingawa waliohojiwa wengi walionesha kuridhika na utolewaji wa huduma ya elimu ya msingi na sekondari pamoja na hali ya usalama.

Alisema kwa upande wa waliohojiwa kuhusu ushiriki wao katika kupiga kura siku ya Oktoba 31, mwaka huu, asilimia 83 walisema watapiga kura, asilimia 16 walisema hawatopiga kura na kati yao asilimia 30 walitaja sababu za kutopiga kura kuwa hati zao hazijaboreshwa na asilimia 27 walisema ni kutokana na kuchoshwa na siasa.

Watanzania walipoulizwa iwapo wangepewa nafasi ya kuchagua baadhi ya vijana waliojitokeza na wenye vipaji vya uongozi katika nafasi ya urais, asilimia 38 walisema wangemchagua Zitto Kabwe, asilimia 15 walimtaja Dk Hussein Mwinyi na asilimia 12 Makongoro Nyerere.

Kwa upande wa umaarufu wa vyama vya siasa, utafiti huo ulionesha asilimia 64 ya wahojiwa waliitaja CCM, asilimia 22 Chadema, CUF asilimia saba na asilimia tano walitaja vyama vingine huku asilimia mbili wakisema hawajui.

Aidha kati ya watu hao waliohojiwa ni asilimia 38 ndio walikiri kushiriki katika mchakato wa kura za maoni za kuteua wagombea.

Alisema kuhusu utendaji wa wabunge katika Bunge lililovunjwa asilimia 20 walimtaja Zitto Kabwe kuwa alifanya vizuri, akifuatiwa na Dk Slaa kwa asilimia 11 na asilimia tatu walimtaja Harrison Mwakyembe, Anna Kilango na John Magufuli.

Friday, October 8, 2010

Redet:Kikwete yupo juu

ASILIMIA 68.5 ya Watanzania waliohojiwa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (Redet) wamesema wanataka mgombea urais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, achaguliwe kuwa Rais.

Mgombea anayefuatia kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo wa taasisi hiyo ni wa Chadema Dk Willibrod Slaa, ambaye amependekezwa na asilimia 11.9 ya waliohojiwa huku Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF akitajwa na asilimia 9.3.

Maoni hayo yamechukuliwa katika mikoa yote nchini katika utafiti ulioanza Septemba 20 hadi 28 ukishirikisha watu wapatao 2,600 kwa kutumia sampuli nasibu kwa wahojiwa kutoka katika kila wilaya mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti Mwenza wa Redet, Dk. Benson Bana, alisema matokeo hayo yanaashiria kwamba endapo uchaguzi ungefanyika Septemba CCM ingeshinda katika urais, ubunge na udiwani.

Licha ya Watanzania kupiga kura za kupenda kuongozwa na Kikwete, asilimia 71.2 walisema watachagua mgombea yeyote wa CCM, asilimia 12.3 wa Chadema, asilimia 10.1 wa CUF, huku vyama vingine vikipata idadi ndogo ya wahojiwa na asilimia 5.6 wakishindwa kuamua.

Dk. Bana alisema kwa upande wa ubunge, asilimia 66.7 ya wahojiwa walisema watachagua wa CCM, asilimia 11.7 wa CUF na asilimia 11.5 Chadema huku asilimia 7.8 walioshindwa kuamua.

Kwa madiwani, asilimia 66 walisema watachagua wa CCM, asilimia 11.5 wa CUF na asilimia 10.3 wa Chadema huku asilimia 10.4 wakikosa msimamo.

Alisema utafiti wa Redet wa Machi ulionesha wahojiwa wengi wangechagua mgombea yeyote wa CCM kwa asilimia 77.2 lakini katika utafiti wa Septemba walimkubali kwa asilimia 71.2 hivyo kupungua kwa asilimia sita na wabunge ilikuwa asilimia 68 na madiwani 68.2, hivyo kwa utafiti huu, CCM bado inaongoza, lakini kiwango cha asilimia za kura kimepungua.

Wakati kwa vyama vinne vya upinzani vikiongozwa na Chadema, vimeongeza idadi ya kura ambapo katika miezi sita, waliosema watachagua mgombea wa Chadema imeongezeka kwa asilimia nane, CUF asilimia 0.9, TLP imeongeza kutoka asilimia 0.2 hadi 0.4, NCCR-Mageuzi kutoka asilimia 0.2 hadi 0.3.

Kwa upande wa wabunge, wakati asilimia 68 ya wahojiwa walisema wangechagua mgombea wa CCM kama uchaguzi ungefanyika Machi; lakini kwa Septemba waliosema hivyo ni asilimia 66.7.

Chadema imeongeza kwa asilimia 2.9, CUF asilimia 1.5 , TLP asilimia 0.8 na NCCR-Mageuzi asilimia 0.8.

Alisema hata hivyo baada ya takribani mwezi mmoja wa kampeni za uchaguzi, kiwango cha uungwaji mkono cha CCM kinapungua wakati kile cha vyama vya upinzani hasa Chadema na CUF kinaongezeka, huku wananchi wengi wakitegemea redio kama chanzo kikuu cha taarifa za kampeni za vyama na wagombea.

Profesa Bana alisema waliohojiwa walitaka vyombo vya habari kutoa nafasi sawa kwa vyama vya siasa, huku wakitaka elimu kuwa suala la kupewa kipaumbele katika serikali ijayo ikifuatiwa na kilimo, afya na maji.

Walitoa angalizo kuwa matokeo ya utafiti huo ni kwa Septemba tu, hivyo katika kipindi cha kuelekea uchaguzi, mambo kadhaa yanaweza kutokea na kubadilisha mwelekeo na mtazamo wa wapiga kura.

Alisema waliohojiwa waliulizwa sifa kubwa itakayowafanya wampigie kura mgombea urais wakisema ni uzoefu katika uongozi (14.8%), anayejali wanyonge na masikini (14.1%), mgombea wa chama chao (14.1%), mgombea asiyeshiriki rushwa au ufisadi (9.9%) na mgombea mwenye elimu (1.9%).

Alisema, mgombea urais wa CCM alitajwa kuchaguliwa zaidi ya asilimia 50 katika wilaya 43 zilizofanyiwa utafiti huku katika wilaya tisa akitajwa chini ya asilimia 50 na wa Chadema akitajwa kwa zaidi ya asilimia 50 katika wilaya tatu za Kinondoni (64%), Kigoma Mjini(56%) na Babati (58%) na mgombea wa CUF kwa zaidi ya asilimia 50 anatajwa katika wilaya moja ya Mkoani kwa asilimia 68.

Kuhusu uchaguzi wa wabunge CCM inaungwa mkono zaidi ya asilimia 50 katika wilaya 40 zilizofanyiwa utafiti huku Chadema ikiungwa mkono kwa asilimia 50 katika wilaya ya Kinondoni asilimia 60, Kigoma Vijijini asilimia 58, Mvomero asilimia 50 na nyinginezo na CUF wakiungwa mkono Micheweni asilimia 49, Wete asilimia 42 na Lindi Mjini asilimia 36.

Walipoulizwa kuhusu utendaji kazi wa Chama tawala asilimia 57.4 walisema wanaridhika na utendaji kazi wa CCM,20.7 walisema wanaridhika kiasi, asilimia 12.3 hawaridhiki na asilimia saba hawaridhiki kabisa, upande wa utendaji kwa vyama vya upinzani asilimia 35.6 walisema wanaridhika sana, asilimia 22.6 wanaridhika kiasi, asilimia 23 hawaridhiki na asilimia 7.2 hawaridhiki kabisa.

Alisema,walipoulizwa kuhusu sababu za kuridhika kiasi au kutoridhika na utendaji kazi wa chama tawala, asilimia 12.7 walisema hawatimizi ahadi 7.7 wala rushwa, asilimia 4.3 hawaaminiki huku kwa upinzani asilimia 7.6 hawaaminiki, 6.5% havina sera, 6.2% vina migogoro na 5.3% havina uwezo wa kuongoza nchi.

Kuhusu chanzo kingine cha habari za kampeni za uchaguzi walisema mikutano ya hadhara inaongoza kwa asilimia 38, ndugu na marafiki 21%, vyama vyao vya siasa asilimia sita, mabango na vipeperushi asilimia nne huku kwa asilimia ndogo makanisa 0.6% na misikiti 0.3%.

Mtafiti Mkuu wa Redet, Dk. Bernadeta Killian, alisema sababu za kutoa utafiti huo sasa, ni utaratibu wao wa kawaida kila baada ya miezi sita huku akikanusha baadhi ya shutuma kuwa watafiti hupewa fedha kupendelea upande fulani.

Membe:Shimbo hakukosea

SERIKALI imesema vyombo vya usalama vina haki ya kutahadharisha wananchi juu ya jambo lolote tofauti na baadhi ya vyama vya siasa, wanaharakati na watu mbalimbali wanavyosema.

Aidha, imeelezwa kuwa kauli ya Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali Abdulrahman Shimbo, kuwa vyombo hivyo vimejiandaa kuhakikisha amani wakati wa uchaguzi, imepotoshwa na kukuzwa bila sababu za msingi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

“Tuache kukuza mambo, alichozungumza Shimbo ni sahihi na wala hakina utata wowote. Matamshi yake yametafsiriwa vibaya na kupotoshwa.

“Vyombo vya usalama sio vya chama fulani na wala havitetei maslahi ya chama chochote, ni kwa ajili ya amani na utulivu wa kila mmoja na nchi kwa ujumla,” alisema Membe na kuongeza:

“Kazi ya vyombo hivi ni kutahadharisha, kuonya na ikilazimika kukamata, sasa sioni ni wapi vilikosea, wahusika warejee kauli ya Shimbo au wasome ujumbe huo kwa sababu haukutolewa kiholela, uko wazi na hauna utata wowote.”

Alisema ameshuhudia uchaguzi katika nchi nne tofauti duniani na kauli za tahadhari zenye kusisitiza utulivu na amani kama ya Shimbo hutolewa bila kuleta utata.

“Ni aibu na siogopi ninathubutu kusema tunatia aibu, vitu vidogo tunavikuza na kuvishabikia sana. Nilikuwa Brazil Septemba 3, mwaka huu wakati wakipiga kura katika uchaguzi mkuu wao, vyombo vya usalama viliheshimiwa kufanya kazi yake ya kulinda amani ikiwa ni pamoja na kutoa kauli mbalimbali za tahadhari,” alisema.

Thursday, October 7, 2010

Upepo wageuka Pemba

TAMBO, vijembe, kejeli na hata vurugu zilizokuwa zikitokea wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu visiwani hapa siku za nyuma, havipo tena katika uchaguzi wa mwaka huu na inadaiwa kupunguza nguvu ya CUF.

Hali hiyo imetokana maridhiano ya kisiasa na uamuzi wa CCM kumteua Dk Ali Mohamed Shein ambaye ni mzaliwa wa hapa, kuwa mgombea urais wa Zanzibar. Dk. Shein amezaliwa kijiji cha Chokocho, Mkanyageni, Kusini Pemba.

Baadhi ya wakazi wa hapa waliozungumza na HABARILEO katika viwanja vya Fire Chanjaani mjini hapa, muda mfupi kabla ya mgombea urais wa CCM Tanzania, Rais Jakaya Kikwete, kuhutubia mkutano wa kampeni juzi jioni, walisema maridhiano ya kisiasa na kuteuliwa kwa Dk. Shein kumepunguza nguvu ya CUF Pemba.

Maridhiano ya kisiasa yalifikiwa baada ya Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kufanya mazungumzo na kukubaliana kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, inayojumuisha vyama hivyo vyenye ushawishi mkubwa wa
kisiasa baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu.

Makubaliano hayo yalibarikiwa na Halmashauri Kuu za Taifa za vyama hivyo na Baraza la Wawakilishi na kisha kupelekwa kwa wananchi kupitia kura ya maoni, ambapo asilimia kubwa ya wananchi waliafiki na maridhiano hayo kukubalika rasmi.

Akizungumza wakati akimkaribisha Rais Kikwete kuhutubia mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mbelwa Hamad Mbelwa, alisema: “Mheshimiwa Mwenyekiti (Rais Kikwete), Pemba ya juzi si Pemba ya leo.

“Napenda kukufahamisha kuwa CCM sasa Pemba ina hali nzuri, usalama na amani vimeongezeka sana.

Miaka ya nyuma wakati kama huu wa kampeni ilikuwa ni hatari sana, lakini sasa ni amani na utulivu na hii inatokana na maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa hivi karibuni,” alisema Mbelwa.

Mkazi wa Mtambile, Ally Hamad Seif, akizungumza na gazeti hili bila kutaja ni mwanachama wa chama gani, alisema: “Mimi naona CCM ndio wamefaidika zaidi na maridhiano, maana kwa miaka mingi Pemba ni ngome ya CUF.

“Naona sasa kama vile CUF wamevunjwa nguvu kiasi na haya maridhiano na ni kama vile wamerudi nyuma, wakati kwa upande mwingine naona kama CCM wanakuja juu zaidi na kushika kasi huku Pemba,” alisema Seif.

Mkazi wa Wete, Zuhura Majid Mbarouk, alisema nguvu ya CUF Pemba kwa kiasi kikubwa inatokana na ushawishi mkubwa wa kisiasa alionao Maalim Seif na hivyo hatua ya kiongozi huyo kusimamia maridhiano ya kisiasa na Rais Karume, kumefanya Wapemba wengi kumwunga mkono na kujenga umoja na mshikamano baina ya CCM na CUF.

“Miaka ya nyuma wakati kama huu ilikuwa ni vurugu sana, tulikuwa hatuwezi kuzikana hata tunapofiwa. Sasa ni amani na utulivu, ni kama vile mwezi huu hakuna uchaguzi, maana Pemba imepoa sana hata nashangaa.

“Nadhani nguvu kubwa ya CUF iko kwa Maalim Seif, sina hakika na nguvu za chama hiki, Maalim Seif akistaafu siasa,” alisema.

Akizungumza katika mkutano huo, Rais Kikwete alijisifu kwa kusimamia maridhiano hayo na kusema ni ahadi aliyoitoa alipohutubia Bunge mara ya kwanza Desemba 30, 2005 baada ya kuchaguliwa kuwa Rais ambapo alieleza kutoridhishwa na mpasuko wa kisiasa baina ya Zanzibar na Pemba.

Alisema hatua hiyo ndiyo ilimfanya asimamie mazungumzo ya kutafuta suluhu ambayo yalikabiliwa na vikwazo vya hapa na pale kabla Rais Karume na Maalim Seif hawajahitimisha na kufanikisha kufikiwa kwa maridhiano ya kisiasa, yanayovifanya visiwa hivi sasa kuwa

na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, baada ya uchaguzi mkuu ujao. “Leo hii nyie ni mashahidi wa namna Pemba ilivyo na amani na utulivu.

Leo mwana CCM anavaa sare yake ya chama bila woga wa kufanyiwa vurugu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Kampeni ni za amani na utulivu. Msione vinaelea vimeundwa,” alisema Rais Kikwete.

Kikwete ambaye aliwasili hapa juzi akitokea Songea, Ruvuma, ambako alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za Siku ya Walimu Duniani, aliwataka wagombea wa CCM kutembea kifua mbele.

Mgombea huyo alisema wagombea wa CCM hawana sababu ya kuendesha kampeni zao kinyonge, kwa sababu CCM imefanya mengi Pemba, kama ilivyo katika maeneo mengine nchini.

“Pambaneni, msibabaike wala kutishika kwa sababu hakuna kisichowezekana,” aliwaambia wagombea hao wa ubunge, uwakilishi na udiwani kupitia CCM.

Katika mkutano wake na wagombea hao juzi mjini hapa, alisema mazingira ya kisiasa yamekuwa bora zaidi Pemba na yanatoa fursa nzuri kwa wagombea wa CCM kupata ushindi.

“Mazingira ni mazuri sasa. Mazingira yamekuwa tulivu na mnaweza kusikilizwa sasa. Naambiwa sasa kuwa picha ya mgombea wa chama kimoja inaweza kubandikwa kwenye nyumba ya shabiki wa chama kingine bila kubanduliwa au kuchanwa.

“Sisi lazima tuendeshe kampeni zetu kwa nguvu moja – tumefanya mengi. Uhodari wenu ni katika kuwaeleza wananchi mafanikio hayo.

“Hatuna unyonge, kwa sababu kama barabara tumejenga, kama skuli (shule) zipo, kama umeme tumeleta, kama maji yanapatikana, kama ni afya hakuna mkazi wa Pemba anayetembea zaidi ya kilometa tano kusaka huduma za afya,” alisema.

Akiwa katika kampeni Unguja katika Uwanja wa Demokrasia maarufu kama Kibanda Maiti, mkoani mjini Magharibi, Rais Kikwete alisisitiza umuhuimu wa kuendeleza Mapinduzi ya Zanzibar na kuleta maendeleo zaidi.

Alisema ataleta maendeleo zaidi katika miaka mitano ijayo na kwamba atashangaa kama wananchi watashindwa kumpigia kura nyingi.

Rais Karume ambaye alikuwepo katika msafara huo, alimuombea kura Rais Kikwete na Dk. Shein.

Tuesday, October 5, 2010

Makachero watumwa kumdhibiti Dk. Slaa

MGOMBEA Urais wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa ametangaza kuwapo kwa mkakati mahususi wa kulazimisha ushindi kwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwa ni pamoja na kusambaza makachero nchi nzima kutimiza azma hiyo.

“Tuna taarifa za kusambazwa kwa makachero nchi nzima ambao wamepewa jukumu la kuhakikisha kwamba Kikwete anashinda kwa gharama zozote,” anasema Dk. Slaa alipozungumza na Raia Mwema, mara baada ya mkutano na waandishi wa habari jana Jumanne.

Katika mkutano huo, CHADEMA pia walitangaza kupata ushahidi kwamba kampuni ya Synovate ilifanya utafiti kuhusu wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwamo urais, tofauti na hatua ya hivi karibuni ya kampuni hiyo kukanusha kuwapo kwa utafiti huo.

“Tumepata ushahidi kwamba Synovate walifanya utafiti kuhusu umaarufu wa wagombea na walipata matokeo ambayo hawajayatangaza. Tunawataka sasa waende mahakamani,” alisema Dk. Slaa.

CHADEMA wanasema kwamba hata watafiti waliokwenda kufanya utafiti huo wako tayari kubainisha usiri wa kampuni hiyo uliofanywa kwa maslahi ya CCM.

Hivi karibuni vyombo vya habari wiki hii vilimnukuu Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe akisema kuwa chama chake kina matokeo ya kura za maoni za Synovate yanayoonyesha kuwa Dk. Slaa anakubalika kwa asilimia 45 akifuatiwa na Rais Kikwete mwenye asilimia 41, kauli ambayo ilikanushwa na Synovate.

Akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita Meneja wa Synovate Limited, Aggrey Oriwo alisema taarifa hizo ni za kughushi, hazina ukweli wowote na zinaupotosha umma kwa kuwa hawajawahi kufanya utafiti wowote unaohusu kukubalika kwa wagombea wa urais.

Oriwo alisema kwa kawaida kampuni yao hufanya utafiti wa hali ya kisiasa kila baada ya miezi mitatu na kwamba wanatarajia kufanya hivyo kabla ya Oktoba 31 na kutoa taarifa yao. Mbali na Synovate, Taasisi ya Mpango wa Utafiti na Elimu Demokrasia Tanzania (Redet) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nayo imeeleza kuwa wataalamu wake kujiandaa kufanya utafiti wa mgombea urais anayekubalika.

Dk. Slaa anaanza awamu ya pili ya kampeni zake mkoani Morogoro Alhamisi wiki hii huku akiwa na imani kwamba sehemu kubwa ya wananchi wanamuunga mkono.

Mgombea huyo wa CHADEMA amenukuliwa akisema kwamba maeneo yote ambayo amepita sehemu kubwa ikiwa ni vijijini, wananchi wameonyesha mwamko wa hali ya juu na wamekuwa wakikusanyika bila kujali mbinu chafu za kuwalaghai ili wasihudhurie mikutano yake ya kampeni.

“Awamu ya kwanza ya kampeni zetu sehemu kubwa tumetembelea vijijini na huko wananchi wamekuwa wakifika wenyewe bila kubebwa na magari kama wenzetu. Wananchi sasa hawaogopi tena askari wa FFU wenye silaha ambao wamekuwa wakifika wakiwa wamejiandaa kwa mapambano ili kuwatisha, huu ni mwamko mkubwa sana,” alisema.

Alisema tofauti na uchaguzi wa mwaka 2005, uchaguzi wa mwaka huu CHADEMA imesimamisha wagombea wengi makini zaidi na ambao wamejitokeza wenyewe bila kushinikizwa na hivyo kuongeza nguvu ya kukubalika kwa umma ikiwa ni ishara ya ushindi katika uchaguzi wa mwaka huu.

“Unapoona sasa wasomi hadi DC (Mkuu wa Wilaya), wahandisi, wanasheria na watu wa kada nyingine wanakuja wenyewe kutaka kugombea kwa chama cha upinzani, ujue sasa nchi imejiandaa kwa mabadiliko, wakati wa CCM kuondoka umefika,” anasema.

Katika ziara yake, Dk. Slaa anasema amewaahidi wananchi kwamba ndani ya miaka mitatu ya utawala wake atahakikisha kwamba Tanzania inaondokana na aibu ya kuagiza chakula nje ya nchi wakati ina ardhi ya kutosha.

“Maisha ya Watanzania nimekuta ni mabaya sana na hii ni vijijini na mijini. Miaka 50 ya Uhuru wananchi wanaishi katika nyumba za ajabu, wakati nchi kama Rwanda zimefanikiwa kupunguza tatizo la makazi kwa watu wake.

“Suala la makazi si tu linagusa umasikini bali linahusu afya zao maana makazi mabovu yanachangia afya mbovu na ndio maana suala la kusaidia wananchi wapate nyumba bora si la mzaha, nitahakikisha naondoa kodi katika vifaa vya ujenzi ili wananchi waweze kujenga makazi bora,” anasema.

Anasema suala la elimu ameliwekea msisitizo na kwamba atahakikisha elimu ya lazima inakuwa hadi kidato cha sita na wananchi wengi waliohojiwa wanakubali kwamba inawezekana pamoja na CCM kubeza mpango huo.

Dk. Slaa anasema kwa miaka mitano ya utawala wa Jakaya Kikwete, asilimia 75 ya bajeti ya serikali imekuwa ikienda kwenye matumizi ya kawaida, sehemu kubwa yakiwa ni anasa na kuacha sekta muhimu kama afya, elimu na miundombinu zikitegemea zaidi wafadhili.

Wakati huo huo, CHADEMA wametangaza vigezo watakavyotumia kuteua wagombea wa Vitimaalumu kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mratibu wa Uchaguzi wa CHADEMA, Kitila Mkumbo, alisema vigezo hivyo ni pamoja na elimu, uzoefu wa uongozi wa kisiasa na uzoefu wa mgombea nje ya siasa.

Mkumbo alivitaja vigezo vingine kuwa ni pamoja na uwezo wa mgombea anayegombea katika jimbo, mchango wa mgombea katika operesheni na katika kampeni zinazoendelea pamoja na umri wa uanachama wa mgombea husika.

Monday, October 4, 2010

Dewji amfagilia Kikwete

Mgombea ubunge wa Jimbo la Singida Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mohamed Dewji, amesema Mgombea urais wa chama hicho, Rais Jakaya kikwete ameiongoza nchi na CCM vizuri tangu achukue madaraka mwaka 2005.

Alisema hayo juzi alipokuwa anasoma mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa miaka mitano iliyopita na kusema wananchi wa Singida wamenufaika na mengi hata wakati wa mtikisiko wa uchumi na upungufu wa chakula walipata msaada kutoka serikalini.

Kwenye upande wa upatikanaji wa maji safi na salama, Dewji alisema sasa maji safi yanapatikana kwa asilimia 85, ukilinganisha na miaka mitano iliyopita.

Vilevile kwenye elimu, alisema sasa Singida Mjini ina shule za sekondari zaidi ya 20 ikilinganishwa na shule mbili tu miaka mitano iliyopita.

Hata hivyo alisema changamoto iliyopo kwa upande wa elimu ni ujenzi wa shule za kidato cha tano na sita ili wanafunzi wengi zaidi watakaofaulu kidato cha nne wapate nafasi ya kidato cha tano na sita.

Changamoto nyingine ni upande wa afya na ugonjwa sugu wa macho (mtoto wa jicho), ambao alieleza unatokana na hali ya hewa ya mji wa Singida. Alisema amefanya jitihada kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali na hadi sasa wagonjwa 500 wamefanyiwa upasuaji kati ya wagonjwa 2,000.

Aliwataka wakazi wa Singida Mjini wafanye maamuzi mazuri ya kuchagua viongozi bora kipindi cha uchanguzi.


CHANZO: NIPASHE

OCD Kyela agoma kulinda helikopta ya Dk. Slaa

Mvutano mkubwa uliibuka jana kati ya mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kyela (OCD), aliyetambulika kwa jina moja la Male, baada ya kutoa taarifa ya kukataa kuilinda helikopta inayotumiwa na mgombea huyo.

Mvutano huo ulianza saa 11:00 jioni jana baada ya Dk. Slaa kuwasili katika uwanja wa Mwakangale mjini Kyela kuhutubia mkutano wa kampeni.

Mkutano huo ulikuwa ni wa mwisho baada ya kuhutubia mikutano mitano ya kampeni katika maeneo kadhaa mkoani Mbeya katika wilaya za Mbarali na Kyela. Mgombea huyo alipangiwa kulala Kyela.

Baada ya kuhitimisha mkutano wa Kyela, Dk. Slaa aliwaeleza wananchi kwamba helikopta hiyo ingelala uwanjani hapo, lakini baadaye akawaambia kuwa alipata taarifa kutoka kwa OCD kwamba polisi hawatailinda kwa maelezo kuwa helikopta hiyo si mali ya serikali bali mali ya mtu binafsi.

Taarifa hiyo ilimfanya Dk. Slaa aje juu na kutoa sauti kali kwamba anataka apewe taarifa hiyo kwa maandishi ili aipeleke kwa Inspekta jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema.

Pamoja na Dk. Slaa kutaka ampe taarifa kwa maandishi, OCD huyo alimwonyesha saa akimtaka ateremke jukwaani kwa kuwa muda wa mkutano ulikuwa umekwisha hivyo ashuke akamshitaki kwa kujiongezea muda wa kampeni. Wakati huo ilikuwa saa 12:10 jioni.

Hali hiyo ilimlazimisha mchumba wa Dk. Slaa, Josephin Mushumbusi na wafuasi wengine wa Chadema waliokuwa wamepandwa na jazba kumfuata OCD, ambaye baada ya kuona hivyo, alianza kuondoka uwanjani hapo.

Kufuatia hali hiyo, Dk. Slaa alimuita jukwaani askari anayemlinda na kuwatangazia wananchi kuwa alipewa askari huyo na IGP amlinde wakati wa kampeni.

“OCD anasema hatalinda ndege yetu wakati mshahara anaolipwa unatokana na kodi zetu,” alisema huku watu wakiitikia kwa kuonyesha kukerwa na kitendo hicho.

Ilimlazimu askari anayemlinda Dk. Slaa kumfuata OCD huyo na kuondoka naye wakiteta kwa faragha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, akizungumza kwa simu na NIPASHE kama anahusiana na tukio hilo, alisema kitendo cha OCD ni chake binafsi na hakiwakilishi Jeshi la Polisi.

Nyombi alisema wao wana maelekezo ya namna ya kutoa ulinzi kwa wagombea wote wa urais na kuahidi kuwa itaendelea kulindwa.

Katika hatua nyingine, Dk. Slaa amesema akiingia madarakani atakagua Sh. bilioni 21, maarufu kama “Mabilioni ya JK” zilitolewa na serikali kwa wajasiliamali kila mkoa, ili kujiridhisha kama ziliwanufaisha walengwa (wananchi) au la.

Amesema atafanya hivyo kwa vile fedha hizo ni mali ya umma na kwamba, kuna taarifa zinazodai kuwa zimewanufaisha watu wachache.

Dk. Slaa alitoa ahadi hiyo wakati akihutubia mkutano wa kampeni za kuusaka urais wa Jamhuri ya Muungano, mjini Songea juzi jioni.

“Rasilimali zinagawiwa ovyo tu bila mpangilio. Hizi fedha ni za umma, lakini hakuna anayejua nani kanufaika nazo. Nitazishughulikia na kuhakikisha zinarudishwa katika matumizi ya umma,” alisema Dk. Slaa na kushangiliwa na umati watu waliofurika katika mkutano huo.

Aliitaka serikali kutaja makampuni yaliyofaidika na Sh. trilioni 1.3 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kuokoa makampuni dhidi ya mtikisiko wa kiuchumi duniani.