Monday, May 31, 2010

'Wanawake acheni kutangaza sigara'

CHAMA cha Afya ya Jamii (TPHA), kimewataka wanawake kuacha kutumika kutangaza aina yoyote ya sigara ili kuzuia athari zitokanazo na matumizi ya tumbaku kiafya.

Msemaji wa chama hicho, Elizabeth Nchimbi alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumzia Siku ya Kupinga Uvutaji Sigara, inayoadhimishwa kitaifa Mwanza leo.

Ujumbe wa maadhimisho ya siku hiyo mwaka huu ni ‘Mkinge mwanamke na matumizi ya tumbaku’.

Alisema matangazo ya bidhaa hiyo yana lengo moja la kuwapasha habari wateja wake kuhusu ubora wake ili wanunue zaidi huku wakisahau athari zitokanazo na mvutaji.

Elizabeth alikumbushia kuwa moshi utokanao na jani la tumbaku una sumu kali ijulikanayo kama nikotini na wakati mtumiaji wa sigara akivuta, moshi huo huchanganyika na hewa na kuzaa sumu aina ya kabonimonoksaidi.

“Ili kuhakikisha kuwa ujumbe wa kuzuia utumiaji wa tumbaku unawafikia walengwa, kuzuia matumizi ya tumbaku kwa wanawake ni muhimu katika mkakati wa kupambana na matumizi ya tumbaku,” alisema Elizabeth.

Alisema wanawake wamekuwa wakitumika kama chombo cha matangazo ya sigara nchini, lakini maadhimisho ya siku ya kupinga matumizi ya tumbaku yanalenga kulinda hadhi pamoja na afya zao kwa ujumla kwani madhara yake humkuta mvutaji moja kwa moja na wengine walio karibu yake.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani alizozitaja Elizabeth, asilimia saba ya wanawake wanapenda sana kuvuta sigara huku wanaume wakiwa ni asilimia 12 na kwamba kati ya wavutaji bilioni mbili, milioni 200 ni wanawake.

“Ikiwezekana serikali ipige vita wanawake kutangaza bidhaa hiyo, ama kuzuia kabisa matumizi yake, bidhaa hiyo ipandishwe bei ili ifikie mahali wananchi washindwe kumudu gharama,” alisema Elizabeth.

Alisema Tanzania imetoa umuhimu mdogo sana kupinga madhara ya tumbaku na hata neno ‘onyo’ katika baadhi ya matangazo limeandikwa kwa maandishi yasiyoonekana kwa urahisi juu ya paketi za sigara.

1 comment:

Anonymous said...

I used to bе ѕuggеsted thiѕ ωebѕіtе
through my cousin. I am not surе whether or not thіs publish is ωrіttеn via him as nobody else
knоw such specіfіc аpproxіmately
mу problem. Yоu're incredible! Thank you!

My site - http://www.page1rankingdallas.com