Tuesday, May 4, 2010

Rais Kikwete:TUCTA waongo

“TUCTA ni waongo! Tucta ni wanafiki! Tucta wana hiana!... wafanyakazi watakaogoma tarehe 5, watakuwa wamekiuka sheria na watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na kanuni za Serikali. Na wale wafanyakazi wataokwenda kazini lakini wasifanye kazi, pia watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Kiongozi bora ni yule anayewaeleza wananchi wake ukweli hata kama ukweli huo utakuwa unauma.”

Hiyo ni kauli nzito ya Rais Jakaya Kikwete, alipozungumza na Taifa kupitia wazee wa mkoa wa Dar es Salaam jana, kuhusu mgomo ulioitishwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kuanzia kesho, kwa madai kuwa Serikali imepuuza mapendekezo ya kuongezwa kwa kima cha chini ya mshahara kufikia Sh 315,000 kwa mwezi.

Rais alisema Serikali haiwezi kulipa kima cha chini cha Sh. 315,000 kutokana na mapato inayopata.

“Nimewasikia Tucta, wanasema huu ni mwaka wa uchaguzi, hawatanipigia kura kama sitalipa kima cha chini wanachokitaka, nipo tayari kuzikosa kura za wafanyakazi kuliko kuwadhulumu Watanzania walio wengi, wakakosa dawa, maji, barabara, elimu, pembejeo za kilimo na huduma nyingine,” alisisitiza Rais akionesha dhdhiri kukerwa na msimamo wa Shirikisho hilo.

Alisema pamoja na mazungumzo yanayoendelea sasa kwa lengo la kuboresha maslahi ya wafanyakazi ikiwamo mishahara, viongozi wa Tucta kwa makusudi, wameamua kuitisha mgomo wa wafanyakazi huku wakitoa madai ya uongo, kwamba Serikali haisikii na viongozi wa Serikali hawawajali wafanyakazi.

Alieleza kushangazwa na kauli za viongozi wa Tucta wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), kauli ambazo kimsingi alisema zinajenga taswira kwamba hakuna mazungumzo yoyote yanayoendelea baina ya Serikali, waajiri na wafanyakazi, kupitia vyama vyao ya kushughulikia maslahi yao na kujenga hisia mbaya kwa wafanyakazi kwamba Serikali haiwathamini.

“Si kweli, Serikalii inawajali na kuwathamini sana wafanyakazi. Zipo hatua ambazo imechukua na inaendelea kuchukua katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

“Tuliingia madarakani kima cha chini ya mshahara kikiwa Sh 65,000 lakini sasa ni Sh 104,000. Kwa makusudi viongozi wa Tucta wanawadanganya wafanyakazi kwamba Kikwete ameongeza Sh 4,000 tu tangu amekuwa Rais wa nchi, jambo ambalo ni uongo mkubwa,” alisema Rais Kikwete.

Alitoa mfano wa mazungumzo yaliyofanyika mwezi uliopita, ambapo pande hizo tatu; Serikali, waajiri na wafanyakazi, walikutana mara tatu Aprili 6, Aprili 26 na Aprili 27 kujadiliana kuhusu kima cha chini ya mshahara na wakashindwa kuafikiana kutokana na viongozi wa Tucta kuleta mapendekezo ya viwango vitatu vya kima cha chini cha mshahara baada ya Serikali kukataa kima cha chini cha awali cha Sh 315,000.

Alisema mazungumzo hayo yakapangwa kuendelea Mei 8 mwaka huu. “Wakati mazungumzo yamepangwa kufanyika tena Mei 8, ili wao waje na mapendekezo yao mengine ya kima cha chini cha mshahara, na sisi Serikali tulete mapendekezo yetu ili tujadiliane, viongozi hawa wa Tucta wanashindwa kusema ukweli na wanakana hata kile walichokisema na kupendekeza wao wenyewe ndani ya vikao halali,” alisema.

Rais alisistiza kuwa Serikali kwa upande wake, imekuwa ikiheshimu mapendekezo ya nyongeza ya kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi kupitia bodi nane za kisekta, na ndiyo maana kutokana na mazungumzo hayo, Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya, alitangaza kima kipya kwa sekta binafsi Aprili 30, mwaka huu, ambacho kilianza kutumika Mei Mosi.

Alisema pia Serikali kupitia majadiliano hayo, imekubali kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma, ongezeko ambalo litatangazwa katika bajeti ijayo ya mwaka wa fedha wa 2010/11, tofauti na kauli zinazotolewa na viongozi wa Tucta kwa wafanyakazi.

Aliongeza kuwa Serikali ina wafanyakazi 350,000 na endapo italipa kima cha chini cha mshahara cha Sh 315,000 italazimika kutumia Sh bilioni 6,852.93, fedha ambazo ni nyingi kuliko mapato ya Serikali, kwani katika bajeti ijayo, Serikali imepanga kukusanya Sh bilioni 5,757.3, na ili iweze kulipa kiasi hicho, italazimika kukopa jambo ambalo ni kichekesho.

“Kama tutalipa mishahara hii kama wafanyakazi wanavyotaka maana yake ni kwamba tutawaridhisha wafanyakazi hawa 350,000, lakini tutawadhulumu Watanzania milioni 39,650,000.

Hatutakuwa na pesa ya kuwanunulia dawa, kuwajengea barabara, kununua madaftari, kununua pembejeo za kilimo wala kuwapa maji safi na salama jambo ambalo siwezi kukubali litokee,” alisema.

Rais Kikwete katika hotuba hiyo iliyorushwa moja kwa moja na baadhi ya vituo vya redio na televisheni, alizungumzia pia mkutano mkubwa wa uchumi kwa Bara la Afrika, utakaofanyika kwa siku tatu Dar es Salaam kuanzia kesho, kwamba utasaidia kukuza na kutangaza jina la Tanzania.

Alisema viongozi na wakuu wa nchi 11 wamethibitisha kushiriki mkutano huo utakaoshirikisha zaidi ya watu 959 kutoka nchi 85 Duniani.

Alisema Tanzania kwa upande wake itanufaika kutangaza fursa ilizonazo katika vivutio vya utalii na uwekezaji.

1 comment:

Anonymous said...

Hata kama TUCTA wanadai visivyowezekana lakini JK kama rais kachemsha, hakutakiwa kuongelea suala hili kiushabiki vile kama mipasho! Tulimtegemea yeye kuwa ni mtu wa mwisho kuongea maneno yale.

Mike