RAIS wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad, wanatarajiwa kuzindua kampeni ya kueneza uelewa kuhusu umuhimu wa kupiga kura za maoni, maofisa wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wamesema.
“Tumepanga kufanya kampeni kubwa Zanzibar nzima kuelimisha wananchi kuhusu kura za maoni kabla ya kushiriki kwao katika kuchagua au kutokuchagua mpango wa kuwa na Serikali ya Mseto (GNU).
“Tumepanga kumualika Rais Karume na Maalim Seif kwa kuwa ndio waanzilishi wa mpango huu,” alisema Mwenyekiti wa ZEC, Khatib Mwinyichande katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Alisema tume hiyo bado haijamchagua mtu yeyote wa kuifanya kampeni hiyo na iwapo kwa sasa kuna mtu anafanya kampeni hiyo, atakuwa anakwenda kinyume na kanuni kwa kuwa ZEC ndio yenye mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa kura hizo za maoni.
Kumekuwa na fununu kwamba baadhi ya watu wameanza kampeni mitaani wakihamasisha wananchi kupiga kura dhidi ya GNU katika siku ya kupiga kura za maoni ambayo imepangwa kufanyika Julai 31, mwaka huu.
Hata hivyo maofisa wa tume hiyo wamesema iwapo fununu hizo ni za kweli, wanaofanya hivyo anafanya makosa. “Tunataka watu wapewe taarifa sahihi ili wachague wenyewe kwa uhuru wao kuhusu upigaji kura za maoni.”
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa ZEC, Sh bilioni 3.7 zitatumika kwa ajili ya upigaji huo wa kura za maoni ambao utafanyika kabla ya uchaguzi mkuu Oktoba 31, mwaka huu.
Iwapo Wazanzibari wengi wataipigia kura GNU, Rais ajaye wa Zanzibar atatakiwa kuunda serikali ya mseto na chama kitakachokuwa imekaribia kura za rais.
No comments:
Post a Comment