Friday, May 14, 2010

Watoro shule kusakwa

WAKUU wa wilaya nchini wanatakiwa kuendesha msako wa nyumba kwa nyumba kubaini waliofaulu kuingia kidato cha kwanza mwaka huu, lakini wako nyumbani.

Katika msako huo ulioagizwa jana na Rais Jakaya Kikwete, mzazi atakayeshindwa kujieleza ni kwa nini mwanawe haendi shule, atawajibishwa. Hakueleza hatua atakazochukuliwa mzazi huyo.

Kikwete alitoa agizo hilo mwanzoni mwa wiki hii akiwa Masasi, na kutaka msako huo ufanyike kwa mtindo unaofanana na wa kukusanya kodi uliotumika zamani, kwa nia ya kuhakikisha wanafunzi hao wanakwenda shuleni.

Kwa mujibu wa taarifa aliyosomewa Mtwara, asilimia 35.6 ya watoto 12,843 waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana na kuchaguliwa kuingia sekondari, hawajaripoti shuleni.

Katika ripoti hiyo ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Anatoli Tarimo, ilielezwa kuwa asilimia 64 sawa na watoto 8, 278 walioripoti na kuanza masomo ya sekondari wakati watoto 4,565 hawajaripoti shuleni na hawajulikani waliko.

Katika idadi hiyo, Wilaya ya Mtwara ndiyo inayoongoza kwa kuwa na asilimia 54 ya wasioripoti, ikifuatiwa na Nanyumbu (48%), Masasi (35%), Tandahimba (32%), Mikindani (22%) na Newala asilimia 21.

Moja ya sababu za utoro, Rais Kikwete aliambiwa ni baadhi ya wanafunzi kupata mimba, kuozwa au kuzuiwa na wazazi. “Hizi takwimu ni za juu sana.

Haiwezekani tukaendelea kudhulumu watoto wetu maisha bora, kwa kuwazuia kwenda shule wakati zipo, nafasi zipo na kila kitu kipo.

“Tafuteni majina ya watoto hawa wote, wazazi wao waitwe, wajieleze na kama hawana majibu wawajibishwe.

Afuatwe mtoto mmoja baada ya mwingine bila kumwacha mtu. Na njia rahisi ufanywe msako wa nyumba kwa nyumba, kama ilivyokuwa zamani wakati wa kukusanya kodi,” alisema Rais Kikwete

Alisisitiza kuwa wakati wa mahojiano wazazi wa watoto hao wasihojiwe sababu za kuzuia watoto, bali mahojiano yahakikishe watoto wanapelekwa shuleni mara moja na kazi hiyo ifanyike katika kila wilaya nchini na kusimamiwa na wakuu wa wilaya.

No comments: