Thursday, May 20, 2010

Mimba zakatisha masomo ya watoto wa kike 400

Zaidi ya watoto wa kike 400 wa shule za msingi na sekondari mkoani Ruvuma wamekatisha masomo yao kutokana na kupata mimba kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kati ya hao waliopata mimba kwa kipindi cha kuanzia Februari 2009 hadi 2010 wa shule za sekondari walikuwa 301 na 98 wa Shule za Msingi.

Tatizo la mimba ni kubwa zaidi katika Wilaya ya Mbinga ambayo hadi mwishoni mwa Februari mwaka huu, jumla ya wanafunzi 149 walikuwa wamesitisha masomo baada ya kubainika kuwa wamepata ujauzito.

Taarifa za uhakika zilizohakikiwa na kufanyiwa uchunguzi na Gazeti la Nipashe kupitia vyanzo vyake mbalimbali ikiwemo taarifa za elimu za Wilaya na Mkoa, zinaonyesha kwamba Wilaya zenye hali tete ni Mbinga na Songea Vijijini.

Katika taarifa ya elimu ya Mkoa wa Ruvuma ambayo wiki chache zilizopita iliwasilishwa kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa huo (RCC), inaeleza kwa kuna mapungufu ya namna kesi zinazohusiana na watuhumiwa waliowapa mimba vijana hao, zikishughulikiwa kwa kasi ndogo na maofisa watendaji wa kata, huku zilizopo mahakamani zikiwa bado hazijapatiwa ufumbuzi.

Tatizo la mimba katika kila wilaya na idadi ya wanafunzi waliopata mimba kwenye mabano ni Songea Vijijini (106), Tunduru (77), Namtumbo (41) na Manispaa ya Songea (26).

Tatizo hilo linaonekana kuwa kubwa kutokana na wahusika wa elimu mkoani hapa kutowajibika kuielimisha jamii ipasavyo kuachana na mila potofu dhidi ya mtoto wa kike.

Aidha, taarifa hiyo inafafanua kuwa hadi sasa ni mashauri 10 yamefikishwa mahakamani, 16 yapo Polisi, wakati 58 yanashughulikiwa katika ngazi za Kata na Vijiji.

Akitoa ufafanuzi kuhusu tatizo hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma (RAS) Salehe Pamba, alisema Serikali imechukua hatua kukabiliana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuzielekeza Mahakama kushughulikia haraka kesi hizo sanjari na kuwahimiza maofisa Watendaji wa Kata na Vijiji kuzisukuma katika vyombo vya dola ili watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria.

“Kuna hatua ambazo uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Ruvuma umechukua kukabiliana na hali hiyo kwanza ni kuhakikisha mahakama inazishughukia kesi zote haraka ili kupunguza kasi ya watoto hao kupata mimba…Watendaji wa Kata na Vijiji tumewaelekeza kuzisukuma kesi hizo haraka kwenye vyombo vya dola ili zipatiwe ufumbuzi wa kudumu lakini pia kuielimisha jamii kuhusiana na mila potofu dhidi ya mtoto wa kike.

CHANZO: NIPASHE

No comments: