Tuesday, May 11, 2010

Wanasheria: Serikali ya Tanzania ni sikivu

WAKATI Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) likiituhumu Serikali kutosikiliza madai yao kuhusu nyongeza ya kima cha chini cha mshahara, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kimeipongeza kwa kuwa sikivu kutekeleza haki za binadamu na utawala bora.

Pamoja na pongezi hizo, pia Tawla imeitaka Serikali kuthamini hoja na mapendekezo ya asasi na vyama vya kiraia, katika mchango wa mabadiliko ya sera na sheria za nchi, kwa kuviwezesha kifedha na maoni yao kuzingatiwa ipasavyo.

Mwenyekiti wa Tawla, Maria Kashonda, alisema hayo jana kwa nyakati tofauti katika sherehe za maadhimisho ya miaka 20 ya chama hicho, katika viwanja vya Mnazi Mmoja ambako mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein.

Katika sherehe hizo, pia Shein alizindua Mpango Kazi wa chama hicho wa miaka mitano (2010 – 2015) ambao pamoja na mambo mengine, unalenga kuendeleza huduma ya msaada wa kisheria kwa wahitaji, ikiwa ni pamoja na wajane na watoto.

Kashonda aliliambia gazeti hili mara baada ya sherehe hizo, kuwa ushirikiano baina ya
Tawla, vyama vingine na Serikali, umekuwa mkubwa kiasi cha kuwezesha kuona uhakika kuwa nchi inatekeleza haki na kuzingatia utawala bora.

“Katika kipindi hicho chote, tunajivunia mambo mengi ambayo yamewezekana kufanyika kwa kuwa Serikali ilikuwa nasi, miongoni mwayo ni marekebisho ya sheria mbalimbali ikiwamo ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA) ya mwaka 1998 na marekebisho ya mwaka 2002,” alisema Kashonda.

Alizitaja sheria nyingine ambazo walishirikishwa katika maboresho kuwa ni pamoja na Sheria ya Ardhi, Sheria ya Vijiji iliyowezesha kuundwa kwa Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Vijiji, Sheria ya Mtoto na mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971.

Mwenyekiti huyo alibainisha pia kuwa Tawla inajivunia ushirikiano mzuri, si na serikali pekee, bali na vyama na asasi zingine kama Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP), Chama cha Wanasheria Tanganyika
(Tanganyika Law Society) na asasi zingine.

Kashonda alisema ni kutokana na ushirikiano huo wamefanikiwa kufikia watu zaidi ya 10,000 katika mikoa kadhaa nchini na kuwapa msaada wa kisheria, hasa wanawake na watoto, na pia kuunda madawati 28 ya jinsia, ambayo yapo katika vituo vya Polisi kuwawezesha watu wa ndoa na matatizo ya uhusiano, kusikilizwa kwa faragha wafikapo Polisi.

Akitoa hotuba katika sherehe hizo, Dk Shein alisema Serikali wakati wote imekuwa ikitambua mchango wa vyama vya kisheria na asasi za kiraia, kwa maendeleo ya nchi na utekelezaji wa haki na utawala bora, hivyo maombi yao kuhusu kutengewa fungu kutoka serikalini, atayafanyia kazi.

“Serikali tunategemeana nanyi katika kutafuta haki kwa wananchi wetu, bila haki hakuna amani, hivyo ninyi ndio mnaiwezesha Serikali kutekeleza haki, juhudi za kulinda amani zinafanikiwa kwa sababu yenu,” alisema Shein.

Alisema Tawla ina haki ya kujivunia uwezo mkubwa iliowajengea wanawake kujua haki zao na matunda yanaonesha kuwa wanawake wanaweza, kwa kuwa miongoni mwao kama Dk Asha-Rose Migiro (Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa), Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mwanaidi Maajar na majaji kadhaa, ni matunda ya chama hicho.

Shein aliitaka Tawla kutoridhika kwa mafanikio hayo bali miaka hiyo 20 iwe chanzo cha kujitathimini upya na kurekebisha upungufu wao ili kuwezesha ufanisi zaidi kwao na kuleta manufaa kwa wananchi wanaohitaji msaada wao.

Katika sherehe hizo pia watu mbalimbali walitunukiwa vyeti vya kutambua mchango wao katika kuanzishwa Tawla hadi ilipofika ambapo Jallya Katende, alitoa ushuhuda wa jinsi chama hicho kilivyomwezesha kupata haki zake baada ya kutalikiana na mumewe mwaka 2005.

No comments: