NCHI za Afrika zimeambiwa kutegemea misaada kwa ajili ya maendeleo yao ni fedheha.
Hayo yalisemwa jana na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliyekuwa akizungumza na wanahabari kuhusu Afrika kuendelea kubaki nyuma kimaendeleo.
Alionya tabia ya viongozi wa Afrika kufikiria wapi pa kupata misaada, badala ya nini cha kufanya wao wenyewe na wananchi wao kujiletea maendeleo, huku akisisitiza kuwa Wazungu wanaotusaidia huwaza namna ya kututawala.
Alikuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu tatizo linalosababisha Bara la Afrika kuendelea kuwa nyuma kimaendeleo wakati lina maliasili za kutosha kujipatia maendeleo.
Kabla ya kujibu maswali hayo, Mkapa, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-Habitat), Profesa Anna Tibaijuka na Balozi wa zamani wa Uingereza nchini Ethiopia, Myles Wickstead, walikuwa wakizindua kwa mara ya pili Kamisheni ya Afrika.
Kamisheni hiyo iliandika ripoti iliyotumika kuangalia namna ya kukabiliana na changamoto za Afrika wakati wa Mkutano wa Nchi Tajiri Duniani (G8) mwaka 2005 na kuzinduliwa kwake kuna lengo la kuangalia kama mapendekezo ya ripoti hiyo yalitekelezwa.
“Nadhani tatizo ni kwa Waafrika kufikiria kuwa kuna watu wako mahali ambao wana jukumu la kuja kutuendeleza,” alisema na kurudia kauli hiyo mara mbili kuonesha kuwa hakukosea, bali anasisitiza.
“Hii biashara ya kutegemea wafadhili kuliko ilivyo kawaida inashtua na inadhalilisha, tunaangalia huku na huko kuangalia nani anatupa nini? “Mkitaka tuendelee, naweza kusema simameni wenyewe kwa miguu yenu, jipangeni na mjipe matumaini ya kufanikiwa, hiyo ndiyo iliyokuwa dhana ya kujitegemea,” alisema Mkapa kwa kujiamini.
Alimsifu Zenawi aliyekuwa katika mkutano huo, kuwa yeye anatumia fikra zake kwa nchi yake.
Kabla ya Mkapa kujibu, Zenawi alitaja baadhi ya mambo yanayosababisha Afrika kutoendelea kuwa ni pamoja na kuwa na miundombinu mibovu.
Baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa habari kuhusu kuzinduliwa kwa kamisheni hiyo, Mkapa aliendelea kuelezea namna Afrika inavyoweza kuendelea katika hali ya sasa ya utandawazi.
“Hawa Wazungu tulipambana nao wakati wa Ukoloni mpaka ukafikia wakati wakaamua kutupa,” alisema na kuongeza kuwa bora kushirikiana na Wachina kuliko Wazungu ambao wanataka kututawala.
“Wachina ni rahisi kushirikiana nao, hawana takataka za Ukoloni, wanajua tuko huru na wao wako huru,” alisema Mkapa.
Kauli hiyo ya Mkapa, iliungwa mkono na Profesa Tibaijuka ambaye alisema tatizo lingine la nchi za kiafrika ni utamaduni.
Alifafanua kwamba nchi zilizofanikiwa Bara Asia zilipata mafanikio baada ya kubadilisha utamaduni wao na kujijengea wa kujiamini zaidi.
No comments:
Post a Comment