MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Enos Mfuru, ameagiza kufanyika msako mkali dhidi ya wanafunzi walioolewa badala ya kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.
Hadi sasa wanafunzi 3,173 sawa na asilimia 13.4 waliochaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari mkoani Mara hawajulikani walipo, kwa mujibu wa Kanali Mfuru.
“Wanafunzi 3, 173 walitakiwa kuwa shuleni lakini hawapo. Wilaya inayoongoza ni Rorya kwa kuwa na wanafunzi 700 ambao hawajaripoti,” Kanali Mfuru alisema juzi.
Mkuu wa Mkoa aliwataka wakuu wa wilaya, kusaka wanafunzi hao na kuhakikisha wanakuwa shuleni kabla ya mwezi huu kumalizika.
“Itumike nguvu ya ziada kwa mzazi na hata mwanafunzi na wote ambao wameolewa warudishwe shuleni,” aliagiza Mfuru alipozungumza na viongozi waandamizi kutoka wilaya zote za mkoa huo juzi.
Aliongeza: “Mwisho wa mwezi huu wote wawe shuleni na hili halina mjadala”. Alitaja wilaya zingine na idadi ya wanafunzi ambao hawajaripoti kwenye mabano kuwa ni Musoma Vijijini (633), Tarime (567), Serengeti (431), Bunda (369) na Musoma Mjini (357).
Kanali Mfuru alisema wazazi waliopeleka watoto kwenye shule zisizo za Serikali, walitakiwa kutoa taarifa badala ya kukaa kimya kana kwamba wapo.
Hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete, aliagiza wakuu wa wilaya kusaka nyumba kwa nyumba, wanafunzi ambao wamechaguliwa kidato cha kwanza mwaka huu, lakini wajaripoti.
No comments:
Post a Comment