WALA rushwa wakubwa wanapaswa kuchukiwa kama Wakoloni wapya wanaopindisha kila jema linalojaribiwa ndani ya nchi na kufanya sera za siasa zionekane sawa na debe tupu.
Hayo yalisemwa jana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, Samuel Sitta, wakati akifungua kongamano la kitaifa la wadau wa kuzuia nakupambana na rusghwa nchini.
Sitta ambaye alimtaka Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) asinyooshewe vidole pekee kwa kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni ya kila mtu, alisema dawa ya rushwa haiko mahakamani.
“Viongozi wenzetu wanaosema eti dawa ya rushwa ni Mahakama, hawana tofauti na watu wanaopuuzia kinga na kuhubiri tiba katika mazingira ambapo maradhi yanaongezeka kusambaa,” alisema Sitta.
Alisema ili rushwa iweze kutokomezwa, hapana budi kila mtu aunganishe nguvu zake katika hilo, la sivyo mapambano hayo yatakuwa ni sawa na bure.
Alisema jamii imekuwa ikifikiri kuwa mapambano ya rushwa ni ya Takukuru peke yake, suala alilosema ni dhana potofu na ambalo baadaye linaweza likaleta madhara makubwa.
“Hatupaswi kuiachia Takukuru peke yake katika mapambano haya,tena siku hizi watu hawasemi Takukuru bali kila mmoja Hoseah, Hoseah … kwa hilo tutakuwa hatusongi mbele, ni vema sote tukashirikiana kuitokomeza,” alisema Sitta katika mahojiano na waandishi wa habari baada ya ufunguzi.
Akitoa sababu ya kuifananisha rushwa na ukoloni, Sitta alisema sababu ni kwamba inaliwezesha kundi dogo la walafi wa mali na madaraka, kupindisha kila jema ndani ya nchi, hali inayochangia maisha ya wananchi kudidimia huku umasikini ukiongezeka.
Akizungumzia dawa ya rushwa kutokuwa mahakamani, Sitta alisema tatizo ni athari zake kuanzia mifumo mingine ya nyuma hadi kesi kufika mahakamani.
“Wapo wangapi ambao wametuhumiwa na makosa mbalimbali lakini hatujawaona kufikishwa mahakamani? Hivyo tiba si mahali hapo bali sote tukishikamana kwa pamoja na kuikataa rushwa,” aliongeza Sitta.
Dk Hoseah alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa nchini yanahitaji nguvu zaidi na za pamoja ili kupata matunda mazuri.
Alisema siku zote jamii imekuwa ikipiga kelele za rushwa kila mahali, lakini tatizo hilo litaendelea kuathiri uchumi wa nchi kama mshikamano wa pamoja hautokuwapo.
Kongamano hilo la siku moja, lilikuwa na lengo la kutathmini mchango, changamoto za kila mmoja dhidi ya rushwa kwa mwaka jana sambamba na kuweka mikakati ya kuzikabili changamoto hizo mwaka huu.
No comments:
Post a Comment