SERIKALI ya Tanzania imepanga kutumia Sh trilioni 11.1 katika bajeti yake ya mwaka ujao wa fedha.
Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo jana aliiambia Kamati ya Bunge ya Fedha, kwamba katika mwaka 2010/11, Serikali imeongeza Sh trilioni 1.6 ikilinganishwa na mwaka jana wa fedha.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkulo alisema kati ya fedha hizo, zinazotarajiwa kukusanywa ni Sh trilioni 6 ambazo ni za mapato ya ndani na Sh trilioni 2.8 misaada na mikopo kutoka kwa wahisani.
Alisema pia kati ya fedha hizo, Sh trilioni 1.1 ni mikopo ya ndani, Sh bilioni 983.7 mikopo ya masharti ya kibiashara na Sh bilioni 30 ni mapato kutokana na ubinafsishaji.
Waziri aliongeza kuwa vipaumbele katika bajeti hiyo vitakuwa ni katika kilimo, huduma za jamii kama elimu, afya na maji, ardhi na umwagiliaji, miundombinu ambayo ni reli, bandari, viwanja vya ndege na nishati.
“Hata hivyo, Serikali itatoa umuhimu wa kipekee katika bajeti yake ya mwaka 2010/11 kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, ili kuhakikisha unafanyika kama ilivyopangwa na mradi wa vitambulisho vya Taifa kutokana na umuhimu wake kiuchumi na kijamii,” alisema Mkulo.
Kulingana na kiasi hicho kinachotarajiwa kupatikana katika bajeti hiyo, alisema Serikali inatarajiwa kutumia Sh trilioni 7.8 kwa matumizi ya kawaida na Sh trilioni 3.2 kwa matumizi ya maendeleo.
Alisema kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka washirika wa maendeleo wanaochangia bajeti ya Tanzania, zinaonesha kuwa misaada na mikopo ya kibajeti kwa mwaka ujao wa fedha itakuwa dola za Marekani milioni 534, ikilinganishwa na milioni 840 zilizokuwa zikitarajiwa kupatikana mwaka huu wa fedha.
Alisema kiasi hicho cha fedha kinaonesha kuwa misaada na mikopo kutoka kwa wahisani kwa mwaka ujao wa fedha imepungua, kutokana na baadhi ya wafadhili kuondoa fedha zilizokuwa zimepangwa kutolewa mwaka ujao katika mwaka wa fedha unaoisha wa 2009/10 ili kuisaidia Serikali kupambana na msukosuko wa kiuchumi duniani.
Hata hivyo, alisema Serikali itaendelea kutumia mikopo nafuu na kuanzia mwaka ujao itatumia mikopo ya kibiashara kwa ajili ya kugharimia bajeti yake.
“Hata hivyo, kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya kuendeleza miradi ya miundombinu, tunatarajia kukopa kwenye soko la ndani Sh milioni 347.4 sawa na asilimia 1.0 ya pato la Taifa na mikopo ya kibiashara yenye thamani ya Sh bilioni 983.7 kwa ajili ya bajeti ijayo,” alisema.
Aliongeza kuwa mkopo huo wa kibiashara ni kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kuendeleza miradi ya maendeleo, lakini pia alisisitiza kuwa Serikali haitakopa mikopo yenye masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharimia matumizi ya kawaida.
Aidha, alisema kwa mwaka wa fedha 2010/11 Serikali inatarajia kukusanya mapato ya ndani yasiyopungua Sh trilioni sita, sawa na asilimia 17.3 ya pato la Taifa ikilinganishwa na mapato ya asilimia 16.4 ya pato la Taifa ya mwaka jana.
“Kati ya kiwango hicho, mapato ya kodi ni Sh trilioni 5.6 na yasiyo ya kodi yanatarajiwa kuwa Sh milioni 351.”
Pia alisema Serikali inatarajia kukusanya Sh bilioni 1.7 kutoka kwenye vyanzo vya halmashauri ambapo pia imelenga kuendeleza mfumo wa makusanyo ya mapato ya ndani, kuimarisha usimamizi na udhibiti wa makusanyo, kuchukua hatua za kupunguza misamaha ya kodi, kutenga fedha kwa ajili utekelezaji wa kaulimbiu ya Kilimo Kwanza.
Akizungumzia suala la kupunguza misamaha ya kodi, alisema Serikali imekuwa ikijaribu kutimiza azma yake hiyo kupitia sekta ya madini, ambapo hata hivyo imejikuta ikikwama kutokana na kufungwa na mikataba iliyoingiwa awali.
“Hapa tumejaribu, lakini imekuwa ngumu, wapo wawekezaji wengine wamejaribu hata kutumia nchi zao iwapo tutaendelea kusisitiza ili tusipewe misaada, ila Serikali inafuatilia zaidi,” alisema.
Wakichangia matarajio ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha, wajumbe wa Kamati walionesha kusikitishwa na kiwango kidogo cha ukusanywaji wa fedha za mapato ya ndani na kuwapo kwa vyanzo vichache vya mapato na kuitaka Serikali iliangalie kwa makini suala hilo, kwa kuwa kwa sasa matumizi ni makubwa kuliko mapato.
Akitoa mchango wake, Kiongozi wa Upinzani bungeni, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), alisema mfumo wa bajeti unaonesha kuwa bado bajeti ya Serikali ni tegemezi, hali ambayo inapaswa kufidiwa katika kupunguza misamaha ya kodi ambayo kwa sasa imefikia dola milioni 600.
Mbunge wa Tabora Mjini, Siraju Kaboyonga (CCM), alisema tatizo la makusanyo ni kubwa na endapo Serikali haitalipa kipaumbele, Tanzania na wananchi wake wataendelea kuwa masikini.
“Bajeti bado haijatueleza ina mikakati gani ya kuondakana na tatizo hili la kutegemea misaada ya nje.”
Mbunge wa Mwibara, Charles Kajege (CCM), alisema mfumo uliowasilishwa, unaonesha Tanzania iko mahututi kiuchumi kutokana na fedha zake za ndani kuwa ndogo ambapo asilimia 60 ya mfumo huo wa bajeti matarajio yake ni fedha za nje.
Katika mwaka wa fedha wa 2009/10, matumizi ya Serikali yalikuwa Sh trilioni 9.5, matumizi ya kawaida yakiwa Sh trilioni 6.7 na ya maendeleo yakiwa Sh trilioni 2.8 ambapo vipaumbele vilikuwa ni elimu, afya, miundombinu, ardhi na kilimo.
Kwa mujibu wa bajeti hiyo, katika matumizi ya maendeleo, kiasi cha Sh trilioni 1.9 zilitokana na fedha za wahisani kupitia miradi na mifuko ya kisekta na kiasi kilichobaki cha Sh milioni 968,028 zilitokana na mikopo ya ndani na sehemu ya mchango wa wahisani kupitia misaada ya kibajeti.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Philip Marmo, amesema athari za wahisani kukataa kuchangia Bajeti ya Serikali mwaka huu, hazitarajiwi kuwa kubwa.
Marmo aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam kuwa athari hizo si kubwa kwa sababu uamuzi huo ni wa muda na unaweza kufutwa kabla ya mwaka wa fedha kuanza.
“Hili la wahisani kukataa kutoa dola milioni 200 athari zake zinaweza kuwa si kubwa sana, ni za muda na pengine zinaweza kumalizika kabla ya mwaka wa fedha kwa sababu masharti waliyotoa si makubwa,” alisema Marmo.
Hivi karibuni, baadhi ya wahisani walisema hawatatoa kiasi cha Dola milioni 200 (takriban Sh bilioni 250) katika Bajeti ya Serikali, kutokana na kutoridhishwa na usimamizi wa fedha za Serikali katika baadhi ya sekta.
No comments:
Post a Comment