MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imetoa amri ya kusimamisha kesi ya wizi wa Sh bilioni 3.9 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), inayomkabili mfanyabiashara maarufu, Jayantkumar Chandubhai Patel, maarufu kwa jina la Jeetu Patel na wenzake watatu, hadi kesi yao ya kikatiba Mahakama Kuu itakapotolewa maamuzi.
Uamuzi huo ulitolewa jana na jopo la mahakimu linaloongozwa na Hakimu Ignas Kitusi, ambaye alikubaliana na maombi yaliyowasilishwa na mawakili Martin Matunda na Mabere Marando wa upande wa utetezi katika kesi hiyo.
Jeetu alifungua kesi Mahakama Kuu akidai kuvunjiwa haki ya kikatiba na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya IPP, Reginard Mengi.
Mawakili wake wanadai kuwa Aprili 23, mwaka jana Mengi alitumia vyombo vya habari
kumuhukumu Jeetu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayosikiliza kesi dhidi ya mteja wao haijatoa hukumu.
Katika kesi hiyo mawakili hao wanaomba tafsiri ya kisheria kwani wanaamini haki ya mteja wao imevunjwa.
Jeetu pia anamshitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa madai kuwa kwa nafasi zao walishindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu baada ya Mengi kumuhukumu kupitia vyombo vya habari.
Katika kesi nyingine zinazofanana na hizo zinamkabili katika mahakama hiyo kwa mahakimu tofauti, mahakama hiyo ilitoa uamuzi kwamba kesi hizo zisimame ili kesi ya kikatiba iliyoko Mahakama Kuu iendelee.
Wakati huo mshtakiwa huyo ameukatia rufaa uamuzi wa Mahakama Kuu ulioamuru majalada ya kesi dhidi yake kurudi Mahakama ya Kisutu kutoka mahakama Kuu yalipokuwepo ili kuruhusu kesi dhidi yake na wenzake ziendelee.
Jeetu pamoja na wenzake Devendra Vinodbhai Patel, Amit Nady na Ketan Chohan wanakabiliwa na kesi nne za wizi wa fedha katika Akaunti ya EPA katika Mahakama ya Kisutu ambazo zilifunguliwa Novemba mwaka juzi.
No comments:
Post a Comment