MBUNGE wa Makunduchi Zanzibar, Abdisalaam Issa Khatib (70), amedai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwamba Ikulu ilitoa ridhaa ya kuendelea na mchakato wa kumpata mzabuni wa ukaguzi wa dhahabu.
Khatib, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Fedha 1995-2008, alidai hayo jana alipokuwa akijibu swali la wakili wa upande wa utetezi, Herbert Nyange, katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi inayowakabili mawaziri wa zamani; wa Fedha, Basil Mramba, wa Nishati na Madini, Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu Hazina, Gray Mgonja.
Nyange alimhoji shahidi huyo wa saba wa upande wa Jamhuri ambaye alidai alikaimu nafasi ya Waziri wa Fedha Mei 2003, baada ya kumwonesha barua iliyoko mahakamani kama kielelezo, ambayo inadaiwa Yona alimwandikia Rais akimwelezea mchakato wa kumpata mzabuni huyo na Rais kujibu kwa kuandika kwa kalamu “nakubali endeleeni haraka”.
Baada ya kumwambia asome maneno hayo, alimuuliza kama Rais akipokea ushauri wa Waziri Yona na kuufanyia kazi, uamuzi huo utakuwa ni wa nani kati ya Rais na Waziri, Khatib alijibu kuwa utakuwa wa Rais.
Wakati huo Rais alikuwa Benjamin Mkapa. Hata hivyo, kulingana na kauli hiyo, Mahakama ilihoji ili kujiridhisha kama kauli hiyo ilikuwa ikimaanisha nini na kuna uthibitisho gani kwamba uamuzi unakuwa wa Rais, Khatib alijibu kama Rais amekubali na amesaini, moja kwa moja ni uamuzi wake Rais.
Khatib pia alijibu kwamba hakuwahi kuona barua iliyoandikwa na Yona kwenda kwa Rais na jibu alilotoa Rais, hata hivyo alikiri hakuna shida yoyote kama Waziri ataamua kufanya mawasiliano na Rais bila kupitia kwa waziri mwingine.
Khatib awali alidai akiwa katika nafasi aliyokuwa akikaimu, Mei 17, 2003, alimwandikia barua Waziri Yona, akitoa ushauri kama wizara yake ilivyoombwa na Wizara ya Nishati na Madini kuhusu mchakato wa kupata mzabuni wa kufanya ukaguzi wa madini.
Katika kumjibu, Yona aliandika akitaka mchakato wa kuipata kampuni itakayofanya kazi hiyo usimame mpaka watakapokwenda wataalamu katika sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, kujifunza na kupata uzoefu kuhusu ufanyaji kazi na gharama zake, ili watakaporudi waweze kupata kampuni inayostahili.
Ushauri huo ulioandaliwa na Khatib baada ya kupata ushauri kutoka jopo la wataalamu waliokuwa katika wizara hiyo ulipomfikia, Yona alijibu Mei 20, 2003 akimfahamisha, kwamba kuna barua aliyoipata kutoka Ikulu ikitoa maelekezo kuhusu suala hilo.
Hata hivyo, kulingana na kielelezo kilichotolewa mahakamani hapo kikidaiwa kuwa ni barua iliyokuwa ikitoka kwa Yona kwenda Ikulu, Yona alijibiwa aendelee kabla hajaomba ushauri wa Wizara ya Fedha.
Nyange alimwuliza Khatib: “Ushauri wako kwa Yona ulikuwa na manufaa yoyote wakati Rais ambaye ni bosi wenu alikuwa ameshaamua?” Khatib alijibu kuwa hakujua hilo na kama angejua kama Rais alishaamua, angewarejea wataalamu na kuwaeleza ili kujua wajibu ulikuwa nini, akadai “nisingeweza kubadili uamuzi wa Rais.”
Shahidi wa nane katika kesi hiyo, Immanuel Mahendeka kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), alidai kuwa kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation, haikulipa kodi katika kipindi chote tangu iliposajiliwa na TRA Oktoba 3, 2003 na kama ingelipa, Serikali ingepata Sh bilioni 11.7 kuanzia 2004 hadi 2007.
Kesi hiyo iliyoko mbele ya jopo la mahakimu wakiongozwa na Hakimu John Utamwa; Mramba, Yona na Mgonja wanadaiwa kuruhusu kutolewa kibali cha Serikali kilichoisaidia kampuni hiyo kutolipa kodi tofauti na mapendekezo ya TRA, uamuzi ulioisababishia Serikali hasara ya Sh 11,752,350,148 kati ya mwaka 2002 na Mei 2005.
Kampuni hiyo inadaiwa kuidhinishwa kusimamia ukaguzi wa dhahabu nchini kwa ‘kubebwa’ bila kuzingatia ushauri na kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha. Kesi hiyo inaendelea leo.
No comments:
Post a Comment