MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, amesema, takrima haijaruhusiwa na pia Rais Jakaya Kikwete hajaibariki.Tendwa amesema, vyombo vya habari vinaupotosha umma katika jambo hilo.
Tendwa amesema,anashangazwa na alichokiita usanii wa kisiasa kugeuza utani wa Rais Jakaya Kikwete alioutoa wiki iliyopita kwa viongozi wa dini na kuufanya ukweli na watu hao kutangaza kuwa amebariki takrima.
Msajili amesema Rais hana mamlaka ya kubadilisha takrima kwa matamshi, kama ilivyogeuzwa na baadhi ya wanasiasa kwamba alibariki takrima katika mkutano wa viongozi hao wa dini uliofanyika Dar es Salaam wiki iliyopita.
“Rais alizungumza kwa wanasemina wale, alipenda kuwa na urafiki, akatoa utani…mimi sikuona utata wala hakubariki takrima…huu ni usanii wa kisiasa,” alisema Tendwa jana Dar es Salaam katika mkutano na waandishi na habari.
Tendwa, amesema,utani hauna budi kuchukuliwa kama utani na mambo ya sheria yakachukuliwa kwa upande wake.
Msajili alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa swali likimtaka aeleze kilichojiri katika mkutano huo, kiasi cha kuibua mjadala katika baadhi ya vyombo vya habari vikinukuu wanasiasa wakimshutumu Rais.
Kwa mujibu wa Tendwa ambaye alikuwa miongoni mwa washiriki wa mkutano huo, Rais Kikwete aliwatania maaskofu kupitia kwa Askofu wa mkoa wa Kilimanjaro kwa kutumia mfano wa ‘kitochi’ kwa kusema sheria ya takrima ni ngumu, lakini akahitimisha kwa kuwasisitiza kwamba lazima ifuatwe.
Akiwashangaa waliochukulia utani huo kama hoja muhimu, Tendwa alisema Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi yamefuta ibara katika Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2007 zilizokuwa zikibariki takrima na Rais hana mamlaka ya kuzirejesha ibara na vifungu hivyo ili kuhalalisha takrima kama inavyodaiwa.
Katika Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi, ibara za 14 na 17 zinafuta mafungu ya 87, 97, 98 na 109 ya Sheria ya Uchaguzi yanayoruhusu utoaji takrima.
“Rais hana mamlaka ya kubadilisha takrima kwa matamshi … nanyi mkachukulia umuhimu; ni vizuri kujifunza mambo ya sheria. Inabidi kuchukua utani kama utani na sheria kama sheria,” alisema.
Akisisitiza kwamba kipindi hiki ni kigumu kisiasa, Tendwa alisema yapo mambo mengi ambayo yanasikika. “Niko tayari kwa hili, Rais hakubariki takrima na wala hana mamlaka wala uwezo,” alisisitiza.
Msajili pia kwa upande wake alisisitiza kwamba sheria ya gharama za uchaguzi ni nzuri na ni ngumu kuitekeleza, kutokana na utamaduni wa rushwa uliokwishajengeka miongoni mwa jamii.
Alisema elimu ya uraia ndiyo itakayokabili ugumu huo wa kutekeleza sheria husika. Kwa mujibu wake, Serikali imejipanga ifikapo mwishoni mwa Juni mwaka huu, elimu iwe imesambazwa nchi nzima.
Alisema kwa sasa wameshakamilisha utoaji elimu kwa viongozi wa madhehebu ya dini, Jeshi la Polisi na jana ilikuwa zamu ya makamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). Pia vyombo vya habari vitapewa semina.
Alisema kipaumbele cha ofisi yake ni kuhusu sheria hiyo hali ambayo aliamua kufanya Jumanne na Alhamisi kila wiki, kuwa siku za kukutana na waandishi wa habari kupokea madukuduku mbalimbali kutoka kwao.
Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2009 ilisainiwa mwaka huu na Rais.
Vitendo vinavyokatazwa ndani ya sheria visifanyike pamoja na matumizi ya fedha ni kufanya malipo kwa wapiga kura ili wamchague mgombea.
Mambo mengine yanayokatazwa ni kuahidi kazi au cheo au wadhifa kwa mpiga kura; kutoa zawadi, ahadi, mkopo au makubaliano yoyote kwa mpiga kura ili ashawishike kumchagua mgombea.
Sheria inakataza kutoa malipo kwa ajili ya takrima ya chakula, vinywaji au starehe yoyote ya kuwashawishi wapiga kura, kuwasafirisha na kuweka mkataba wowote wa pango kwa niaba ya wapiga kura.
Katika hatua nyingine, Tendwa aliwaambia waandishi wa habari kwamba masahihisho ya kanuni za uchaguzi yamekamilishwa na leo kuna kikao kitakachohusisha mawaziri wa Katiba na Sheria ambacho ndicho kitakuwa na mamlaka ya kupitisha kanuni hizo.
No comments:
Post a Comment