MAKAMU wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein leo atakuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 20 ya Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA) zitakazofanyika Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Makamu wa Rais, katika sherehe hizo, Dk. Shein atapokea maandamano ya wanasheria hao yatakayoanzia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu saa tatu asubuhi na kumalizikia viwanja vya Mnazi Mmoja.
Aidha, Makamu wa Rais atazindua Mpango Mkakati wa TAWLA wa miaka mitano unaoanzia mwaka 2010-2015, unaolenga katika kuendeleza utoaji wa msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto.
Mpango Mkakati huo pia unalenga kutoa elimu kuhusu haki za wanawake kumiliki mali, utawala bora kwa ujumla wake, masuala ya haki na ajira kwa watoto na kuendelea kufanya tafiti na kuelimisha jamii juu ya sheria zinazomkandamiza mwanamke ili zifanyiwe marekebisho.
Katika kuadhimisha miaka 20 ya TAWLA, wanasheria hao wamepanga kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wiki nzima katika ofisi zao zilizopo Dar es Salaam na kwenye vituo vingine mikoani vya Tanga, Arusha, Dodoma na Pwani.
No comments:
Post a Comment