Thursday, April 29, 2010

Baadhi wakataa matokeo ya utafiti wa Redet

UTAFITI uliofanywa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) kuhusu uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu, umewasha moto miongoni mwa wabunge na wanasiasa, wengi wao wakiuponda huku wabunge wengi wakijiamini kushinda katika majimbo.

Wabunge na wanasiasa hao walizungumza jana na HABARILEO kwa nyakati tofauti, wengi wao wakionesha wasiwasi juu ya utafiti huo, huku wanasiasa wa vyama vya upinzani wakisema utafiti huo umetengenezwa kwa manufaa ya CCM.

Mbunge wa Mkuranga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, aliliambia gazeti hili kuwa anashangazwa na jinsi utafiti huo ulivyofanywa jimboni mwake, ingawa alisema haujamshtua wala hautamnyima usingizi, kwa kuwa ana imani kuwa kazi aliyoifanya jimboni inampa dalili zote za kurudi.

“Nashindwa kuelewa hiyo asilimia wameitoa wapi, ila naichukulia kama changamoto kwangu, ninachofahamu mimi hawa Redet walikuja Mkuranga, wakapiga picha, jambo ambalo si sawa na mtu akiangalia mpira mwanzo mpaka mwisho, picha haisemi sana,” alisema Malima.

Alisema tangu kushika kwake madaraka Mkuranga hali ya mapato ya wilaya imeimarika kutoka makusanyo ya Sh milioni tisa hadi Sh milioni 100.

Kwa mujibu wa utafiti, asilimia 46.0 ya waliohojiwa katika jimbo hilo walisema hawatamchagua tena na asilimia 38.8 ndio waliothibitisha kumchagua.

Naye Mbunge wa Pangani, Mohammed Rished, alisema utafiti huo una walakini ingawa filimbi ya mwisho ni dakika 90 ambayo ni siku ya uchaguzi.

“Tusubiri uchaguzi ufike, kwa kuwa ninachojua, mimi sina tatizo jimboni kwangu, kama mbunge nimetekeleza Ilani ya chama changu na ziada.

Hivyo katika hili tuwaachie wananchi.” Asilimia 4.2 ya wahojiwa katika jimbo la Rished ndio watakaomchagua kwa mujibu wa utafiti, wakati asilimia 87.5 walisema watachagua mbunge mwingine.

Kwa upande wake, Mbunge Kasulu Mashariki, Daniel Nsanzugwanko, ambaye utafiti unaonesha asilimia 20 ya wahojiwa ndio watakaomchagua na asilimia 68 kumkataa, alisema utafiti huo haujaweka wazi ni jimbo gani ambalo linatajwa na wananchi, kwa kuwa katika wilaya hiyo kuna majimbo ya Kasulu Mashariki na Magharibi.

“Mwenzangu wa Magharibi, Kilontsi Mporogomyi ana vipindi vitatu vya ubunge katika jimbo lake, mimi viwili, waweke wazi ni nani anayetajwa na utafiti huu, hata hivyo kwa upande wangu nina kila dalili na vigezo vinaonesha nitarudi bungeni mwakani,” alisema Nsanzugwanko.

Naye Mbunge wa Tarime, Charles Mwera, alisema pamoja na kwamba hafahamu namna utafiti huo ulivyofanyika, lakini hawezi kupuuza matokeo.

“Inategemea ni akina nani walihojiwa, hasa kwa sisi wa vijijini ila kwa nafasi yangu nina imani nina nafasi nzuri ya kutetea nafasi yangu,” alisema Mwera ambaye asilimia 24.5 walionesha watamchagua huku asilimia 61.2 wakionesha kuchagua mwingine.

Pamoja na wabunge hao wengine wanaotajwa na utafiti huo wa Redet kuwa viti vyao si salama ni wa Njombe, Anne Makinda na Yono Kevela, wa Sumbawanga Mjini Paul Kimiti ingawa alishatangaza kutogombea na wa Iramba Mashariki na Magharibi, Mgana Msindai na Juma Kilimba.

Wengine ni wa Kiteto, Benedict Nangoro, Dodoma Mjini Ephraim Madeje ambaye pia ametangaza kutogombea; Wete, Mwadini Jecha; Micheweni, Shoka Khamis Juma; Chake Chake, Fatma Maghimbi; Mkoani, Ali Khamis Seif na Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo.

Wengine ni wa Liwale, Hassab Kigwalilo; Mtwara Mjini, Mohammed Sinani; Kigoma Mjini, Peter Serukamba; Iringa Mjini, Monica Mbega; Bukombe, Emmanuel Luhahula; Lushoto, Abdi Mshangama; Biharamulo Phares Kabuye ambaye alifariki dunia na wa Tabora Mjini, Siraju Kaboyonga.

Lipumba, alisema utafiti huo unaonesha ni wa kupikwa, kwa ajili ya kuipigia debe CCM. “Redet ilipaswa kuhamasisha demokrasia, lakini sasa inaikandamiza, matokeo haya ni kuhalalisha wizi wa kura kwenye uchaguzi ujao, inasikitisha sana.”

Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, alisema utafiti huo umeonesha jinsi Kikwete alivyo maarufu na kuwataka wenzake wajifunze kupitia hapo.

“Tujifunze jamani, mwaka jana utafiti kama huu tuliudharau na huu wa leo unaonesha yale yale.” Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Pius Msekwa, alisema pamoja na kwamba utafiti huo umeonesha asilimia kubwa ya wabunge ambapo wengi wa CCM wanaweza wasirudi mwakani kwenye majimbo yao, chama hicho hakiwezi kuathirika kwa kuwa rungu la kumteua mgombea wa jimbo kwa kura za maoni wamepewa wananchi.

Juzi akitoa matokeo ya utafiti huo wa 16, Dk Killian, alisema anafahamu kuwa utafiti huo utakuwa gumzo na kila mtu atasema lake, lakini wao wanataaluma wanaamini utafiti huo ni huru. “Hatuogopi kusema ukweli na tunafanya kazi yetu kwa misingi ya uwazi na taaluma, hatujali tunamgusa nani.”

Kwa mujibu wa utafiti huo, uliofanywa Machi mwaka huu, asilimia 61.7 ya wabunge walioko madarakani wako katika hatihati ya kurudi bungeni baada ya uchaguzi huo ambapo pia umeonesha kuwa asilimia 85 ya Watanzania waliohojiwa, wanaridhishwa na chaguo lao; Kikwete.

No comments: