Jumatano ya tarehe 25/03/2009, katika kuadhimisha wiki ya maji (16/03 – 22/03), semina za GDSS walifanya tathimini ya kampeni ya maji ambayo ilizinduliwa mwaka 2005 kufuatiwa na sera ya ubinafsishwaji wa maji. Lengo la tathimini hiyo ilikuwa ni kuangalia kampeni hiyo iliyokuwa ikiongozwa na TGNP, FemAct, na wanaharakati wengine imefikia wapi mpaka sasa. Muwasilishaji wa mada hii alikuwa ni Badi Darusi (KWYDP). Mwezeshaji aliweza kueleza Chimbuko, Mafanikio na Changamoto zilizotokana na utekelezaji wa kampeni hiyo.
Chimbuko la kampeni ya maji ya mwaka 2005 ilikuwa ni sera ya mpya ya Ubinafsishaji wa maji ambayo ilishinikizwa na IMF/WB kwa serikali za nchi masikini kama masharti ya kupatiwa mikopo/misaada. Sera hiyo ambayo ilitaka kutambua maji kama bidhaa zingine na iuzwe kama huduma zingine zinavyouzwa, ilipelekea wanaharakati waanzishe kampeni ya kupinga sera hiyo na kuishinikia serikali iachane na mipango hiyo ya kuuza maji kwa raia wake. Kauli mbinu ya kampeni hii ilikuwa ni “Maji Sio Bidhaa, Maji ni Uhai”
Ahadi za Rais wa Nne katika Kampeni za uongozi, ambaye aliahidi 65% ya wananchi kupata maji ndani ya mita 30 ifikapo mwaka 2010 ilichochea wanaharakati kuwa na kampeni hii ili kuweza kufanya tathimini ya hali ya maji nchini. Katika Kampeni hii wanaharakati walikuwa na madai saba ambayo ni;
1. Maji yatambulike kama haki muhimu ya binadamu.
2. Haki za kimataifa ziweze kutambua mchango wa wanawake katika utafutaji wa maji.
3. Kupinga shinikizo la IMF na WB kwa serikali la kubinafisha sekta ya maji.
4. Kuwepo na mjadala wa kitaifa kuhusiana na swala zima la maji.
5. Ongezeko la Bajeti ya Maji.
6. Uchangiaji wa huduma ya maji usitishwe.
7. Kuwa na wizara ya maji inayojitegemea.
Mwaka 2005/06 TGNP na wanachama wa GDSS walifanya utafiti katika baadhi ya maeneo ya Mabibo, Kigogo, Kisarawe, Mwanayamala, Salasala, Tabata, na Kiwalani. Utafiti ambao ulionyesha baadhi ya maeneo hayana miundo mbinu ya maji, ama iliyopo ni chakavu, ama haitoshelezi, wakazi kutegemea maji yanayouzwa katika magari, au kuchota umbali mrefu. Bado katika maeneo mengi wanawake ndio watafutaji wa maji na wanatumia muda na umbali mrefu kutafuta na kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Utafiti huo ulisaidia kutengenezwa kwa mpango kazi kwa vikundi vilivyoshiriki, ambapo walikubaliana yafuatayo; kufanya tafiti ndogondogo katika mitaa yao; kuangalia na kushirikiana na kamati za maji katika maeneo yao; kuandaa mikutano ya hadhara juu swala la maji ili kupata maoni ya wananchi; na kupeana mirejesho juu ya kinachoendelea katika maeneo mbalimbali mara kwa mara.
Changamoto zilizojitokeza ni pamoja na;
Muingiliano wa Shughuli za maendeleo na siasa –kwa mfano, wenyeviti wa serikali za mitaa kutumia mikutano ya maji kujinadi; Uwiano usio sawa wa jinsia katika kamati za maji-ambapo kamati nyingi zina wanaume watupu; Ufinyu wa raslimali kwa vikundi vinavyofanya kampeni hizi; Ufinyu wa elimu ya ushawishi na utetezi kwa vikundi; Ushirikiano mdogo kati ya serikali za mitaa na vikundi vya wanaharakati; na kuwepo kwa mianya ya rushwa katika baadhi ya maofisa wa serikali za mitaa.
Tufanye nini?
• Tuchambue muongozo wa bajeti wa mwaka huu na kuangalia ni jinsi gani maji yalivyotengewa fedha na zitatumika vipi, wapi na kwa akina nani, ili tuweze kufanya kampeni mapema kushinikiza serikali kuongeza bajeti ya maji katika mwaka huu wa fedha wa 2009/10 kuhakikisha bidhaa hii adimu inawafikia walengwa.
• Wanaharakati wakae na kamati za maji za mitaa yao na waweze kuwafichua wahujumu wa maji katika mitaa yao kwa kupiga kura za siri ama njia yoyote itakayoleta mafanikio kuwafichua wahujumu wa maji.
• Wanaharakati wametakiwa kufanya vitendo vya utekelezaji na kuacha maneno mengi kama inavyoonekana sasa, hivyo wanapaswa kuchukua hatua katika maadhimio wanayofikia kila mara.
Kama wanaharakati tunashiriki vipi katika kuhakikisha Maji yanapatikana kwa wananchi wote na kwa urahisi?
1 comment:
wananchi wasipoungana na kupambana na sera hizi za unyonyaji dhidi yao, ni vigumu kwa watu wengine kutoka nje kuja kuwasaidia, ukombozi wowote unaanzia kwa anayekandamizwa kukataa na kuchukua hatua dhidi ya manyanyaso yoyote juu yake.
Kupata maji safi ni haki ya kila raia wa nchi hii.. Wananchi wote waungane na kudai huduma bora za jamii kutoka kwa serikali yao bila kuangalia itikadi ya siasa.
Post a Comment